Kilimo bora cha Nanasi - Sehemu ya Kwanza (Growing Pineapple - Part One)


SEHEMU YA KWANZA

Nanasi (Pineapple) ni zao la kitropiki linalopandwa maeneo mengi barani Afrika, ikiwemo Tanzania. Zao hili hulimwa maeneo yenye joto, kwa nchi zenye baridi kama Uingereza, zao hili hupandwa kwenye greenhouse zinazotoa joto.

AINA
Kuna aina tatu za nanasi ambazo hupandwa maeneo mengi yenye joto nchini Tanzania na Afrika mashariki kwa ujumla;

1. Smooth Cayenne
Aina hii hupendwa na wakulima wengi, ina utamu wa wastani na huzaa sana.


2. Queens
Aina hii ni ndogo na ni tamu sana kuliko Smooth Cayenne
3. The Red Spanish
Aina hii haina magamba kama aina zingine, ukubwa wake na utamu upo katikati kati ya Smooth Cayenne na Queens.



MAZINGIRA
Zao la nanasi hufanya vizuri maeneo yenye hali ya hewa ya joto la wastani sio joto kali. Kiwango cha joto ridi kinachohitajika ni kuanzia nyuzi joto 18°C hadi 45°C. Zao hili huvumilia hali ya baridi kwa muda mfupi, hali ya baridi ikizidi husababisha zao la nanasi kudumaa na kuchelewa kukomaa na tunda la nanasi kua na tindikali nyingi.

Kiwango cha mvua kinachohitajika kwa zao hili ni kuanzia mm 650 hadi mm 3800 kwa mwaka, kama unatumia umwagiliaji hususani kwa kipindi cha kiangazi hakikisha unatumia njia sahihi ya kumwagilia, kwani sio njia zote zinafaa kwa zao hili. Njia zinazofaa kwa zao hili ni kwa kutumia njia ya matone (Drip Irrigation) na kwa kutumia vifaa maalumu vinavyoitwa 'Sprinkler', njia hii humwagilia mithili ya mvua. Njia ya umwagiliaji isiyofaa kwa zao hili ni kwa kufurisha maji shambani (Flooding Irrigation) kwa sababu zao hili halipendi ardhi inayotwamisha maji (Waterlogging).

Pia zao hili huathiriwa na muinuko kutoka usawa wa bahari, mara nyingi zao hili hufanya vizuri kuanzia mita 0 hadi mita 1800 kutoka usawa wa bahari, Muinuko zaidi ya mita 1800 husababisha nanasi kuwa na ladha ya chumvichumvi na tindikali nyingi.

Zao la nanasi hupendelea udongo tifutifu usiotwamisha maji, wenye kiasi kikubwa cha mboji au maozea. Pia inatakiwa ardhi ilimwe kina cha kutosha. Kiasi cha tindikali ya udondo (pH) kinachohitajika ni kuanzia pH ya 4-5, Ardhi yenye vichuguu vya sisimizi wakubwa haifai kwa zao hili kwani huwa na kiasi kikubwa cha tindikali (pH).

KUANDAA SHAMBA
Ardhi ya kupanda zao hili inatakiwa iandaliwe vizuri kwa sababu mizizi ya zao hili ni mifupi (Shallow roots). Mizizi hii ni hatari kuharibiwa na shughuli mbalimbali za Shamba kama Palizi n.k. Ardhi ikiandaliwa vibaya haitoi mavuno mazuri. Maeneo ambayo yana udongo mfinyanzi ni muhimu kulima wakati wa kiangazi ili kusaidia mizizi ya nanasi kupenya vizuri kwenye udongo. Lima kina cha kutosha hadi kufikia sm 45, ukishalima sawazisha shamba kwa kulima mara ya pili (Harrowing) ili kuufanya udongo kuwa laini.

KUPANDA
Zao la nanasi halipandwi kwa mbegu kama mazao mengine bali kwa kutumia vikonyo (Vegetative propagation), Vikonyo hivi vipo vya aina tatu, navitaja kwa lugha ya kingereza navyo ni; Crowns, Slips na Suckers. Yafwatayo ni maelezo ya kina kuhusiana na vikonyo hivi pamoja na muonekano katika picha;

1. Crowns
Haya ni majani yanayoota juu ya tunda la nanasi, huchukua miezi 22 hadi 28 kutoa matunda.

Photo Credit: www.carminereddarter.wordpress.com

2. Slips
Haya ni majani yanayoota kwenye shina la nanasi, huchukua miezi 20 hadi 24 kutoa matunda.
3. Suckers
Haya ni majani yanayoota sehemu ya chini ya mmea usawa wa mizizi, hutoa mavuno mengi, huwa na ugumu sana kwenye kupanda huchukua miezi 17 hadi 22 kutoa matunda.




Ili kuhakikisha uotaji uliosawia, ni vyema kutumia vikonyo vya aina moja wakati wa kupanda. Kabla ya kupanda vitunze vikonyo vyako ndani kwenye giza kwa kuvigeuza juu chini ili kwa muda wa miezi mitatu, baada ya hapo vipande kwenye udongo laini ulio mkavu, kama unategemea mvua panda mwezi wa 11 wakati mvua zinakaribia kunyesha (Kalenda hii ni kwa maeneo mengi nchini Tanzania).

MUHIMU
Kama una upungufu wa vikonyo vya kupandia (Crowns, Slips au Suckers), unaweza ukagawa kila kikonyo kimoja kwa kuvikata katikati kutoa vipande 2 au 4 vilivyosawa, vikiwa na sehemu ya mzizi kila kipande, Ili kuepuka vipande hivyo kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali inatakiwa uvitunze kwenye chumba chenye giza mpaka utakapoona kuwa zile sehemu zilizokatwa zimekauka kabisa (Vikikaa wiki moja ndani). Baada ya hapo unaweza ukavitibu vikonyo vyako kwa kutumia maji ya moto yenye nyuzi joto 50°C viloane kwa muda wa nusu saa hadi saa moja, ili kuua vimelea vya magonjwa ya ukungu na wadudu kama Mealybugs na minyoo ya kwenye udongo (Nematodes). Ukishavitibu vikaushe kivulini ili kuepuka magonjwa ya ukungu alafu vipande shambani, Panda vikonyo mara tu mvua za muda mrefu zinapoanza kunyesha.


Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post