AINA
Kuna aina tatu za nanasi ambazo
hupandwa maeneo mengi yenye joto nchini Tanzania na Afrika mashariki kwa
ujumla;
1. Smooth Cayenne
Aina hii hupendwa na wakulima
wengi, ina utamu wa wastani na huzaa sana.
2. Queens
Aina hii ni ndogo na ni tamu sana
kuliko Smooth Cayenne
3. The Red Spanish
Aina hii haina magamba kama aina
zingine, ukubwa wake na utamu upo katikati kati ya Smooth Cayenne na Queens.
MAZINGIRA
Zao la nanasi hufanya vizuri
maeneo yenye hali ya hewa ya joto la wastani sio joto kali. Kiwango cha joto
ridi kinachohitajika ni kuanzia nyuzi joto 18°C hadi 45°C.
Zao hili huvumilia hali ya baridi kwa muda mfupi, hali ya baridi ikizidi
husababisha zao la nanasi kudumaa na kuchelewa kukomaa na tunda la nanasi kua
na tindikali nyingi.
Kiwango cha mvua kinachohitajika
kwa zao hili ni kuanzia mm 650 hadi mm 3800 kwa mwaka, kama unatumia
umwagiliaji hususani kwa kipindi cha kiangazi hakikisha unatumia njia sahihi ya
kumwagilia, kwani sio njia zote zinafaa kwa zao hili. Njia zinazofaa kwa zao
hili ni kwa kutumia njia ya matone (Drip Irrigation) na kwa kutumia vifaa
maalumu vinavyoitwa 'Sprinkler', njia hii humwagilia mithili ya mvua. Njia ya
umwagiliaji isiyofaa kwa zao hili ni kwa kufurisha maji shambani (Flooding
Irrigation) kwa sababu zao hili halipendi ardhi inayotwamisha maji (Waterlogging).
Pia zao hili huathiriwa na muinuko kutoka usawa wa bahari,
mara nyingi zao hili hufanya vizuri kuanzia mita 0 hadi mita 1800 kutoka usawa
wa bahari, Muinuko zaidi ya mita 1800 husababisha nanasi kuwa na ladha ya
chumvichumvi na tindikali nyingi.
Zao la nanasi hupendelea udongo tifutifu usiotwamisha maji,
wenye kiasi kikubwa cha mboji au maozea. Pia inatakiwa ardhi ilimwe kina cha
kutosha. Kiasi cha tindikali ya udondo (pH) kinachohitajika ni kuanzia pH ya
4-5, Ardhi yenye vichuguu vya sisimizi wakubwa haifai kwa zao hili kwani huwa
na kiasi kikubwa cha tindikali (pH).
KUANDAA SHAMBA
Ardhi ya kupanda zao hili
inatakiwa iandaliwe vizuri kwa sababu mizizi ya zao hili ni mifupi (Shallow
roots). Mizizi hii ni hatari kuharibiwa na shughuli mbalimbali za Shamba kama
Palizi n.k. Ardhi ikiandaliwa vibaya haitoi mavuno mazuri. Maeneo ambayo yana
udongo mfinyanzi ni muhimu kulima wakati wa kiangazi ili kusaidia mizizi ya
nanasi kupenya vizuri kwenye udongo. Lima kina cha kutosha hadi kufikia sm 45,
ukishalima sawazisha shamba kwa kulima mara ya pili (Harrowing) ili kuufanya
udongo kuwa laini.
KUPANDA
Zao la nanasi halipandwi kwa mbegu
kama mazao mengine bali kwa kutumia vikonyo (Vegetative propagation), Vikonyo
hivi vipo vya aina tatu, navitaja kwa lugha ya kingereza navyo ni; Crowns,
Slips na Suckers. Yafwatayo ni maelezo ya kina kuhusiana na vikonyo hivi pamoja
na muonekano katika picha;
1. Crowns
Haya ni majani yanayoota juu ya
tunda la nanasi, huchukua miezi 22 hadi 28 kutoa matunda.
2. Slips
3. Suckers
Ili kuhakikisha uotaji uliosawia, ni vyema kutumia vikonyo
vya aina moja wakati wa kupanda. Kabla ya kupanda vitunze vikonyo vyako ndani
kwenye giza kwa kuvigeuza juu chini ili kwa muda wa miezi mitatu, baada ya hapo
vipande kwenye udongo laini ulio mkavu, kama unategemea mvua panda mwezi wa 11
wakati mvua zinakaribia kunyesha (Kalenda hii ni kwa maeneo mengi nchini
Tanzania).
MUHIMU
Kama una upungufu wa vikonyo vya
kupandia (Crowns, Slips au Suckers), unaweza ukagawa kila kikonyo kimoja kwa
kuvikata katikati kutoa vipande 2 au 4 vilivyosawa, vikiwa na sehemu ya mzizi
kila kipande, Ili kuepuka vipande hivyo kupata maambukizi ya magonjwa
mbalimbali inatakiwa uvitunze kwenye chumba chenye giza mpaka utakapoona kuwa
zile sehemu zilizokatwa zimekauka kabisa (Vikikaa wiki moja ndani). Baada ya
hapo unaweza ukavitibu vikonyo vyako kwa kutumia maji ya moto yenye nyuzi joto
50°C viloane kwa muda wa
nusu saa hadi saa moja, ili kuua vimelea vya magonjwa ya ukungu na wadudu kama
Mealybugs na minyoo ya kwenye udongo (Nematodes). Ukishavitibu vikaushe
kivulini ili kuepuka magonjwa ya ukungu alafu vipande shambani, Panda vikonyo
mara tu mvua za muda mrefu zinapoanza kunyesha.
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
إرسال تعليق