Mara nyingi wakulima waliowengi hutumia kikonyo aina ya
Crowns kupanda zao hili. Crowns ni majani yaliyoota juu ya tunda la nanasi.
Uzuri wa kikonyo hiki, mkulima au mtu wa kawaida anaweza kuvikusanya baada ya
kununua tunda la nanasi sokoni au baada ya kula tunda la nanasi, ni tofauti na
aina nyingine za vikonyo kama Slips na Suckers ambavyo mpaka vipatikane
shambani.
Zao la nanasi hupandwa kwa nafasi, nafasi inayotakiwa ni
kama ifuatavyo; Shina hadi shina sm 30 na mstari hadi mstari sm 60, pia unaweza
ukapanda kwa kuacha sm 120 kila baada ya mistari miwili (inayoachana kwa sm
60). Kwa nafasi hii kutakua na wastani wa mimea 36,350 kwa Hekta moja.
Photo Credit: www.plantopedia.com
Hatua kwa Hatua namna ya kupanda*
- Kata kikonyo chako kilichopo juu ya tunda la nanasi (Crowns), ondoa sehemu ya tunda iliyobakia kwenye kikonyo kwani huwa na sukari nyingi.
- Acha vikonyo vyako vikauke ndani ya chumba chenye giza kwa muda wa wiki 1 hadi 2. Unapovipanga hakikisha unavigeuza juu chini. Sehemu iliyokatwa iangalie juu.
- Baada ya kukauka lowanisha vikonyo vyako kwenye dawa ya ukungu na dawa ya wadudu.
- Panda vikonyo vyako kwa nafasi ya sm 30 shina hadi shina na sm 60 mstari hadi mstari, vikonyo hivyo vizame ardhini kina cha sm 3, pia unaweza ukachimba mashimo yenye kina cha sm 7 au 10. Baada ya hapo sindilia udongo kiasi.
- Mwagilia maji kama udongo ni mkavu ili kuharakisha kikonyo kutoa mizizi.
- Itachukua muda wa miezi 15 hadi 24 kuvuna nanasi.
KUWEKA MBOLEA
Zao la nanasi huitaji mbolea hususani kirutubisho cha
nitrojeni, Baada ya kikonyo cha nanasi kutoa machipukizi, weka mbolea jamii ya
NPK juu ya ardhi karibia na shina la nanasi.
Kirutubisho cha Nitrojeni hufaa
sana kuongeza ukubwa wa matunda na mavuno kwa ujumla, Pia ni vyema ukatumia mbolea za asili pamoja
na za kisasa. Kiasi cha mbolea za asili kinachohitajika kwa Hekta moja ni Tani
5 hadi 10. Pia kirutubisho cha Phosphate (P) huitajika ili kuboresha mizizi na
kuongeza uzalishaji, hivyo mbolea jamii ya NPK hufaa sana kwa zao hili.
Pia mbolea za kwenye majani
(Foliar fertilizer) hufaa sana kwa zao hili, Ingawaje kirutubisho cha Nitrojeni
(N) kikizidi sana husababisha matunda ya nanasi kuwa na maji mengi kuliko
utamu.
Pia kirutubisho cha Potassium (K) hufaa sana kwani husaidia
matunda kukomaa mapema na kua bora sana. Tumia mbolea jamii ya NPK ili kuupa
mmea kirutubisho cha Potassium (K).
PALIZI (WEEDING)
Hakikisha shamba lako linakua safi wakati wote kwa kuondoa
magugu shambani aidha kwa kutumia jembe la mkono au kwa kutumia madawa ya kuua
magugu (Herbicides). Njia hii ya kutumia kemikali za kuua magugu hufaa sana kipindi
cha awali cha uandaaji shamba, yaani kabla ya kupanda, kwa sababu lazima tuwe
na tahadhari ya kiafya ili tupate matunda ya nanasi yasiokua/yaliyo na kiasi
kidogo cha masalia ya kemikali (Pesticides residue)
Kuondoa magugu shambani hasaidia kupunguza kiwango cha
wadudu waharibifu na magonjwa, kwani magugu hayo ndio makazi ya wadudu
waharibifu na chanzo cha vimelea vya magonjwa mbalimbali ya mmea.
WADUDU WAHARIBIFU NA MAGONJWA
A: WADUDU WAHARIBIFU
1. Nematodes/Minyoo Fundo (Meloidogyne
javanica and Pratylenchus brachyurus)
Kama umetembelea makala zangu zilizopita utakua umekutana na
maelezo ya kina kuhusiana na mdudu huyu kwenye mazao mengine. Jinsi anavyofanya
uharibifu kwenye mizizi ya mazao mengine ndivyo anavyofanya kwenye nanasi.
Namna ya Kudhibiti
- Uwe na tabia ya kubadirisha mazao
- Hakikisha shamba lako linakua safi wakati wote
- Kama utaweza tumia mazao yoyote ya mti wa mwarobaini (kama Unga uliosagwa kutokana na majani, matawi au magome ya mwarobaini) kwa kuweka kwenye udongo.
2. Pineapple mealybug (Dysmicoccus brevipes)
Hawa ni wadudu wenye umbile kama yai, wana rangi ya pinki,
wanakua na urefu hadi mm 3 na wanatengeneza unato mweupe kwenye mwili wake
wote. Mdudu huyu ni hatari sana kwa uzalishaji wa nanasi kwani husambaza
ugonjwa wa virusi wa nanasi uitwao "Mealybug or Pineapple Wilt Virus"
(Ugonjwa wa mnyauko).
Wadudu hawa mara nyingi huwa kwenye mizizi ya nanasi na
huzaliana sana kwenye shina la nanasi. Baada ya kuzaliana sana kwenye shina la
nanasi, baadae huenea kwenye maua, matunda madogo na matunda yaliyokomaa, pia
hufika kwenye majani ya juu ya tunda la nanasi (Crown leaves).
- Wakila kwenye majani husababisha rangi ya njano kuanzia mwishoni mwa jani (leaf tips), baadae njano hiyo husambaa hadi jani zima na hatimae majani hukauka.
- Wakila maua husababisha majeraha ambayo mara nyingine hukumbana na chavua (Spores) ambazo zina ugonjwa wa ukungu (Fungal disease), hatimae husababisha ulemavu unaoitwa 'Black Spot'
- Wakila mizizi husababisha mizizi kuoza na baadae mmea kunyauka.
Wadudu hawa (Mealybugs) huishi
salama kwenye maeneo yao na kuongezeka kwa sababu huishi pamoja na jamii
mbalimbali ya sisimizi (Ants). Sisimizi hawa, hususani sisimizi wenye kichwa
kikubwa (Pheidole megacephala) hawamdhuru mealybug bali hula unato kama asali
unaotoka kwenye mwili wa mealybug, hali hii husaidia kuwapunguzia utando huo
ambao ukizidi kwa mealybug wadogo husababisha mwili wa mealybug kukakamaa.
Sisimizi hawa (Ants) wanapokua
wanakula unato wa mealybugs (Honeydew), huwabugudhi wadudu wengine wanaokula
mealybugs (Natural enemies), kwa hiyo mealybugs hupona kuliwa kwa sababu ya
uwepo wa sisimizi hao (Ants). Vilevile sisimizi hawa huwasambaza mealybug
kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa kuwabeba kwenye midomo yao.
Namna ya kudhibiti
Tumia dawa mbalimbali za wadudu
zinazoweza kuwaangamiza hao sisimizi (Ants), wakishaangamia mealybug wanakosa ulinzi hivyo huangamizwa kirahisi na wadudu wengine (Natural enemies).
Njia nyingine ni kutibu
vipandikizi au vikonyo hususani Crowns kwa kutumia maji ya moto yenye nyuzi
joto 50°C kwa dakika 30 (Loweka
vikonyo hivyo kwenye maji hayo ya moto kwa dakika 30). Njia hii husaidia
kuondoa mazalia ya melybug na kusaidia mmea utakaoota kutokua na wadudu hawa
pia kutokuwepo kwa uwezekano wa mmea kupata ugonjwa wa mnyauko "Mealybug /
Pineapple Wilt Virus" unaosababishwa na virusi vinavyosambazwa na wadudu
hawa.
Post a Comment