Kilimo cha Kabichi - Sehemu ya pili (Growing Cabbage - Part two)


KILIMO CHA KABICHI SEHEMU YA 2

KUTAYARISHA SHAMBA
Shamba litayarishwe mwezi mmoja kabla ya kupandikiza miche kwa kukatua ardhi hadi kufikia kina cha sentimita 30. Lainisha udongo na tengeneza matuta. Lainisha udongo na tengeneza matuta. Weka mbolea za asili zilizooza vizuri kiasi cha ndoo moja hadi mbili, kwa eneo la mita mraba 10. Mbolea hii iwekwe katika kila shimo, kiasi kinachotakiwa ni kiganja kimoja cha mkono kilichojaa au viwili. Hii ni sawa na tani 10 hadi 20 kwa hekta. Katika sehemu zenye upungufu wa madini ya fosforasi mbolea aina ya N.P.K yenye uwiano wa 5:15:5 itumike. Kiasi kinachotakiwa ni kizibo cha soda kimoja au kijiko kimoja cha chai chenye gramu 5 kwa kila shimo la mche.

KUPANDIKIZA MICHE
Miche huwa tayari kwa kupandikizwa shambani baada ya majuma 3 hadi 5 tangu kuotesha mbegu, kutegemea aina ya kabichi. Wakati huu miche huwa na urefu wa sentimita 15 mpaka 20 au urefu uliosawa na kalamu ya risasi.

Ng'oa miche kwa uangalifu na pandikiza kama ilvyokuwa kitaluni. Wakati wa kuweka miche shimoni hakikisha mizizi haipindi.

Nafasi ya kupandikiza inategemea aina ya kabichi zenye vichwa vikubwa kama vile Drumhead zipandikizwe katika nafasi ya sentimita 60 kati ya mche na mche na sentimita 75 kati ya mstari na mstari. Aina yenye vichwa vidogo kama vile Oxheart zipandikizwe katika nafasi ya sentimita 40 hadi 50 kutoka mche hadi mche na sentimita 60 kutoka mstari hadi mstari. Nafasi kati ya tuta na tuta lingine ni sentimita 60. Wakati mzuri wa kupandikiza ni asubuhi na jioni. Baada ya kupandikiza weka matandazo kama vile nyasi kavu ili kuzuia magugu yasiote na kuhifadhi unyevu wa udongo.


KUTUNZA BUSTANI

Palizi
Kabichi ni zao ambalo mizizi yake haina kina kirefu, hivyo palizi haina budi kufanyika juu juu ili kuepuka kuikata mizizi. Punguza palizi ya mara kwa mara kwa kuongeza matandazo hasa kabichi zinapoanza kufunga.

Umwagiliaji
Kabichi hustawi vizuri zaidi iwapo kuna maji ya kutosha kwenye udongo. Mwagilia mara mbili au zaidi kwa wiki kutegemea hali ya hewa na aina ya udongo. Kabichi ambazo hazikupata maji ya kutosha huchelewa kufunga na huwa na vichwa vidogo. Zikikosa maji kwa muda mrefu na zikapata maji mengi ghafla, Vichwa hupasuka.

Mbolea
Mbolea ya kukuzia (S/A) au CAN huwekwa shambani katika wiki ya nne hadi ya sita baada ya kupandikiza miche na kabla ya vichwa kufunga. Weka kiasi cha kilo 200 kwa hekta. Mbolea hii iwekwe mara mbili, kilo 100 ziwekwe katika wiki ya nne hadi ya sita baada ya kupandikiza miche, kutegemea aina ya kabichi. Kiasi kinachobakia kiwekwe mwezi mmoja baadae. Kiasi kinachohitajika kwa mche mmoja ni kizibo kimoja cha soda ambacho huwa na gramu tano. Mbolea iwekwe kuzunguka shina umbali wa sentimita 10 kutoka kwenye shina, kwa aina ya vichwa vikubwa. Aina ya vichwa vidogo umbali uwe sentimita 5.

ZINGATIA
Epuka kuweka mbolea nyingi. Kwani husababisha vichwa visifunge vizuri (Kabichi zinakua nyepesi).



Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 18/11/2016

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم