Kilimo Bora cha Alizeti - Sehemu ya Pili (Growing Sunflower - Part Two)


SEHEMU YA PILI

KUDHIBITI WADUDU WAHARIBIFU NA MAGONJWA

A: WADUDU WAHARIBIFU

1. Cutworms
Hawa ni jamii ya viwavi wenye rangi ya kijivu, kahawia au nyeusi. Hufanya mashambulizi wakati wa usiku, mchana wanajificha kwenye udongo. Viwavi hawa hukata mashina ya miche michanga usawa wa ardhi.

Photo Credit: www.legendseeds.net

Photo Credit: www.legendseeds.net

Namna ya kuwadhibiti
  • Hakikisha usafi wa shamba kwa kuandaa na kulima shamba lako vizuri, ukilima shamba lako vizuri unafanya mayai ya viwavi hawa kuwa juu ya ardhi hatimae huharibiwa na mwanga wa jua au kwa kuliwa na wadudu hivyo kupunguza wingi wao.
  • Tumia dawa za kuua wadudu zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.
2. Semiloopers
Hawa ni viwavi wanaokula majani.

Photo Credit: www.eagri.org

Namna ya kuwadhibiti
  • Tumia dawa mbalimbali za kemikali zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.
3. African bollworms
Hawa pia ni jamii ya viwavi wanaokula majani na vichwa vya alizeti.

Photo Credit: www.infonet-biovision.org

Namna ya kuwadhibiti
  • Tumia dawa za kuua wadudu zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.
4. Ndege (Birds)
Ndege husababisha hasara kubwa ya upotevu wa mavuno ya alizeti, kuzidi wadudu waharibifu wengine. kwa sababu ndege hawa wanapenda sana kula mbegu za alizeti. Inatakiwa mkulima atumie nguvu kubwa kuwadhibiti ndege hawa.


Photo Credit: www.allbirdcage.com

Namna ya kuwadhibiti
  • Wafukuze ndege hawa kwa kutumia vitu mbalimbali kama; kutengeneza midoli mfano wa binadamu na kuisimika shambani, kuweka au kusimika vinguo au vikaratasi vya nailoni vinavyopepea, kuweka nyuzi zinazotoa sauti mara upepo unapopita  n.k.
  • Panda alizeti muda ambao wakulima wenzako wengi wanapanda, hii itasaidia kupunguza hasara, maana wakati inakomaa alizeti yako basi alizeti za wenzako zitakua zinakomaa pia, kwa hiyo ndege watatawanyika maeneo yote hivyo kupunguza hasara kwa mkulima mmoja mmoja.
B: MAGONJWA

1. Sclerotinia wilt (Mnyauko)
Huu ni ugonjwa wa mnyauko unaovamia mizizi, shina na kichwa. Ugonjwa huu ukizidi mmea hunyauka na kufa.

Photo Credit: www.grainews.ca

Photo Credit: www.grainews.ca

Dalili za ugonjwa
  • Sehemu zilizoathiriwa husinyaa na kuoza.
Namna ya kudhibiti
  • Badirisha mazao
  • Tumia mbegu bora za alizeti zilizothibitishwa kitaalamu (Certified seeds)
  • Mimea iliyougua itoe shambani na kuichoma moto.
2. Downy Mildew
Huu ni ugonjwa wa ukungu husababisha majani kuwa na utando wa unga unga mweupe kwa sehemu ya chini ya jani, hali hii huathiri ukuaji wa mmea na kusababisha mmea kudumaa.

Photo Credit: www.grainsa.co.za

Namna ya kudhibiti
  • Badirisha mazao
  • Tumia mbegu bora za alizeti zilizothibitishwa kitaalamu (Certified Seeds)
  • Tumia dawa za ukungu zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo kama Ridomil, Linkmil, n.k. Tumia dawa hizi kwa mimea michanga.
3. Charcoal rot
Huu ni ugonjwa wa kuoza mashina. Mashina huwa na rangi nyeusi sehemu ya chini usawa wa ardhi, ugonjwa ukizidi shina huoza na mmea hufa.

Photo Credit: www.sunflowernsa.com

Namna ya kudhibiti
  • Badirisha mazao
  • Tumia mbegu bora za alizeti zilizothibitishwa kitaalamu.
MAVUNO
Alizeti huwa tayari kwa mavuno baada ya siku 90 (miezi mitatu) au 120 (miezi minne) au 160 (miezi mitano) itategemeana na mbegu uliyopanda. Inatakiwa mkulima avune alizeti yake wakati wakati imekomaa vizuri, Alizeti inakua imekomaa vizuri wakati kichwa chake kimekauka na kimekua na rangi ya njano iliyoiva.
Wakati wa kuvuna kata vichwa vya alizeti na vikusanye sehemu moja juu ya turubai ili kuepuka alizeti yako kuchangamana na uchafu. Kisha piga au twanga na miti vichwa hivyo, ichambue vizuri, ipepete na ungo halafu ianike juani.

MUHIMU
Hakikisha unavuna kwa wakati, usisubiri mpaka majani yote ya alizeti yakauke ndipo uvune, ukishaona kichwa kimebadilika rangi na kuwa njano iliyoiva basi alizeti yako imekomaa na unatakiwa kuivuna, ukisubiri sana ndege watapunguza mavuno.

Kwa shamba lililotunzwa vizuri na kutumia mbegu bora, Hekta moja hutoa mavuno wastani wa Tani 3 hadi 4 (3 - 4 tonnes/Ha.) sawa na Tani 1.2 hadi 1.6 kwa ekari moja (1.2 - 1.6 tonnes/acre). Tani hizo hapo juu ni sawa na magunia 50 hadi 67 ya kilo 60 kwa Hekta moja, sawa na magunia 20 hadi 27 ya kilo 60 kwa ekari moja.

NB:
Hekta moja ni sawa na ekari mbili na nusu (2.5 acres).

UTUNZAJI BAADA YA KUVUNA
Ni muhimu kwa mkulima kutunza mazao yake vyema baada ya kuvuna, yafuatayo ni mambo muhimu ya kuyafanya mara baada ya kuvuna.

1. Kukausha alizeti
Zianike alizeti zako juani kwa kuzitandaza juu ya turubai safi. Zikaushe kwa siku 3 hadi 5 mpaka mbegu ziwe nyepesi.
Inatakiwa alizeti zako ziwe na unyevu (Moisture content) chini ya asilimia 10% kabla ya kuzitunza ghalani.

2. Kutunza Ghalani (Storage)
Tunza alizeti zako kwenye chumba au ghala lenye mwanga na hewa ya kutosha. Unaweza ukakamua mafuta ili kuongeza thamani ya alizeti zako.

<<< SEHEMU YA KWANZA

** KAMA UNATAKA UMSHIRIKISHE MWENZAKO MAKALA HII KWENYE MITANDAO YA KIJAMII KAMA FACEBOOK, TWITTER, N.K. BOFYA HAPO CHINI

**MWISHO WA MAKALA HII**

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

4 تعليقات

إرسال تعليق

أحدث أقدم