Kilimo cha Bilinganya - Sehemu ya Kwanza (Growing Eggplant - Part one)


KILIMO CHA BILINGANYA 
SEHEMU YA 1

Bilinganya imo katika jamii ya mimea inayohusisha nyanya, pilipili na viazi mviringo. Mboga hii ina viinilishe muhimu kama vile madini aina ya chokaa na chuma, vitamini A, B na C, wanga, protini na maji. Mboga hii hutumika kutengeneza supu au kama kiungo katika vyakula mbalimbali. Vile vile huweza kuhifadhiwa kwa kukatakata vipande na kuwekwa kwenye makopo.


MAZINGIRA
Zao hili huhitaji hali ya joto la wastani, udongo wenye kina kirefu na rutuba ya kutosha na usiotuamisha maji. Kwa kawaida bilinganya hulimwa zaidi ya msimu mmoja lakini katika nchi za kitropiki (joto) zao hili hulimwa msimu mmoja.

AINA
Aina za bilinganya zinazolimwa kwa wingi katika nchi za ukanda wa joto ni kama zifuatazo;


1. Black Beauty
Aina hii huzaa sana, matunda yake ni meusi, makubwa, na ya mviringo.

2. Florida Market
Matunda ya Florida Market yana umbo la yai. Aina hii pia huzaa sana, lakini hushambuliwa sana na ugonjwa wa mnyauko bakiteria (Bacteria wilt)

3. Florida High Bush
Matunda yake ni makubwa yenye umbo la yai na rangi yake ya kijani kibichi iliyochanganyika na nyeusi.


4. Newyork Spineless
Matunda yake ni ya mviringo, makubwa na yana rangi ya zambarau.


5. Peredeniya
Aina hii huzaa sana, matunda yake ni makubwa kiasi na yana umbo la yai.

Aina zingine za bilinganya ni Matale, Kopek na Rosita. Aina hizi huvumilia sana mashambulizi ya ugonjwa wa mnyauko bacteria.


KUOTESHA MBEGU
Mbegu huoteshwa kwanza kwenye kitalu na baadaye miche huhamishiwa shambani. Kabla ya kusia mbegu, tengeneza tuta lenye upana wa mita moja na urefu wowote. Weka mbolea za asili kama vile samadi au takataka za majani yaliyooza vizuri kiasi cha ndoo moja kubwa ya Lita 20 katika eneo la mita mraba moja. Sia mbegu kiasi cha gramu mbili mpaka tatu (nusu kijiko cha chai chenye ujazo wa gramu tano) katika eneo hilo.

Gramu 500 za mbegu zinatosha kupandikiza katika eneo la hekta moja. Nafasi kati ya mastari na mstari iwe sentimita 10 hadi 15, na kina kiwe sentimita 1.5. Baada ya kusia mbegu fukia na tandaza nyasi kavu na kisha mwagilia maji. Endelea kumwagilia kitalu kila siku, asubuhi na jioni, hadi mbegu zitakapoota. Mbegu huota baada ya siku 10 hadi 12.



Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 04/09/2016

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم