KILIMO CHA BILINGANYA
SEHEMU YA 2
KUHAMISHA MICHE
Miche huwa tayari kwa kupandikizwa shambani baada ya wiki sita hadi nane. Wastani huu huwa na urefu wa sentimita 15 mpaka 20 (sawa na urefu wa karamu ya risasi)
Mwezi mmoja kabla ya kupandikiza miche, rutubisha udongo kwa kuweka mbolea za asili zilizooza vizuri. Mbolea hizi ni kama samadi, mbolea za vundz na mbolea za kuku. (Rejea Kanuni za ukuzaji wa mbogamboga nilizochapisha kwenye blogi hii, kuzipata kwa urahisi nenda sehemu ya juu ya blog hii iliyoandikwa "TAFUTA MADA UITAKAYO HAPA" Andika unachotafuta...mfano: "Kanuni za ukuzaji wa mbogamboga" halafu bofya "Search" baada ya hapo utaona matokeo kadhaa chini yake, ndipo utakapochagua makala unayotaka.)
Weka kiasi cha tani 10 hadi 20 kwa hekta. Kiasi hiki ni sawa na kuweka ndoo moja hadi mbili zenye ujazo wa Lita 20 katika eneo la mita mraba moja. Lakini kutokana na uhaba wa upatikanaji wa mbolea hizi za asili unaweza ukaweka mbolea hizi kwa kila shimo litakalopandikizwa mche wa bilinganya kwa kiasi cha Kiganja kimoja au viwili. Kuweka kila shimo itakusaidia kutumia mbolea kidogo kwa eneo kubwa. (Rejea kanuni za ukuzaji wa mbogamboga >>> SEHEMU YA 1, SEHEMU YA 2 na SEHEMU YA 3)
Mbolea ya mchanganyiko aina ya N.P.K yenye uwiano wa 20:10:10 huwekwa kwenye shimo wakati wa kupandikiza mche. Kiasi kinachohitajika ni gramu tatu hadi tano (sawa na kizibo kimoja cha soda).
Nafasi ya kupanda hutegemea aina ya bilinganya. Aina ndogo hupandikizwa katika nafasi ya sentimita 80 mpaka 100 kutoka mstari hadi mstari na sentimita 50 mpaka 60 kutoka mche hadi mche. Aina kubwa hupandikizwa katika nafasi ya sentimita 80 mpaka 100 kutoka mstari mpaka mstari na sentimita 80 mpaka 90 kutoka mche hadi mche. Kazi ya kuhamisha miche ifanyike kwa uangalifu mkubwa ili kuepuka kuikata mizizi.
KUTUNZA SHAMBA
1. Kuweka Matandazo
Mara baada ya kupandikiza miche, tandaza nyasi kavu. Matandazo husaidia kuhifadhi unyevu, huzuia magugu yasiote na huongeza rutuba ya udongo.
2. Palizi
Hakikisha shamba ni safi wakati wote ili kuzuia ushindani wa chakula, maji na mwanga kati ya mimea na magugu. Usafi wa shamba pia huondoa maficho ya wadudu waharibifu na huzuia kuenea kwa magonjwa.
3. Mbolea
Mbolea ya kukuzia aina ya CAN au S/A huwekwa wiki tatu baada ya mmea kuanza kutoa maua. Weka kiasi cha kizibo kimoja cha soda kuzungukia kila mche. Mbolea iwekwe katika umbali wa sentimita tano kutoka kwenye shina. Hakikisha mmea haugusi mche.
4. Kukata Kilele
Wiki mbili baada ya kupandikiza miche, kata sehemu ya juu ya mmea (Kilele) kama umepanda aina ndefu ya bilinganya. Hii itasaidia kupata matawi matatu hadi manne na mmea kutengeneza umbile la kichaka. Matawi yakizidi manne yaondolewe ili kupata mazao mengi na bora.
5. Kumwagilia
Zao la bilinganya hustawi vizuri likipata maji ya kutosha. Umwagiliaji ufanyike kila siku asubuhi na jioni kutegemea hali ya hewa.
Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 04/09/2016
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
إرسال تعليق