Kilimo cha kabichi - sehemu ya tatu (Growing Cabbage - Part three)


KILIMO CHA KABICHI SEHEMU YA 3

Wadudu waharibifu na Magonjwa

A. Wadudu

1. Viwavi wa Kabichi (Diamond Backmoth)
Viwavi hawa huwa na rangi ya kijani kibichi na alama ya mstari wa kung'aa mgongoni. Nondo hataga mayai chini ya jani na baada ya kuanguliwa viwavi hula sehemu ya chini ya jani na kuacha ngozi nyembamba mfano wa dirisha la kioo. Ni muhimu kuuwa viwavi kwa sababu ndio wanaoleta madhara makubwa.

Piga dawa za kuuwa wadudu hawa zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo, kama Karate, Actellic, Selecron na nyinginezo.






2. Inzi wa Kabichi (Cabbage Sawfly)
Mashambulizi hufanywa na kiluwiluwi mwenye rangi ya kijani kibichi au bluu. Hula majani yote ya kibichi na kubakisha vena au vishipa vya majani.

Inzi wa kabichi wanaweza kuzuiwa kwa kutumia dawa mbalimbali ikiwemo Karate, Actellic, Selecron na nyinginezo




3. Sota (Cutworms)
Hawa ni funza wakubwa wenye rangi ya kijivu. Hupendelea kujichimbia katika udongo wakati wa mchana na kukata miche michanga karibu na usawa wa ardhi wakati wa usiku.





Zuia wadudu hawa kwa kutumia majivu au dawa kama vile Selecron, Actellic au dawa zingine zenye viua sumu vya Carbaryl, Fenvalerate, na Deltramethrin mara baada ya kupanda. Kama mche utakatwa, mtoe mdudu huyu kwa kumfukua au kumuua kisha pandikiza mche mwingine.

4. Vidukari au Wadudu Mafuta (Cabbage Aphids)
Wadudu hawa ni wadogo sana wenye rangi ya kijani, nyeusi au khaki. Baadhi yao wana mabawa na wengine hawana. Hufyonza utomvu wa mimea na husababisha majani kubadilika rangi na kuwa meupe au njano iliyopauka. Mmea hudumaa na hatimaye hufa.

Wazuie wadudu hawa kwa kunyunyiza dawa zenye viua sumu vifuatavyo; Fenvalerate, Dimethoate, Lambda - Cyhalothrin (Karate) na Dichlorvos.





5. Minyoo Fundo (Root Knot Nematodes)
Hawa ni wadudu wadogo waishio ardhini na ambao hawaonekani kirahisi kwa macho. Hushambulia mizizi na kusababisha kabichi kudhoofu na kushindwa kufunfa vizuri. Mimea iliyoshambuliwa mizizi yake huwa na nundunundu.



Wadudu hawa wanaweza kuzuiwa kwa kuzingatia yafuatayo;
(a) Utumiaji wa mbolea za asili kila msimu hupunguza kuzaliana kwa wadudu hawa.
(b) Usipande Kabichi mfululizo kwenye sehemu ileile wala jamii yake kama vile kabichi ya kichina na Koliflawa, ila badilisha kwa kupanda mazao mengine kama vile mahindi, karoti, radishi na vitunguu
(c) Ondoa masalia yote shambani ambayo yanaweza kueneza wadudu na yachome moto.

6. African Mole Cricket (Gryllotalpa Africana)
Hawa ni aina ya panzi ambao hujificha kwenye nyufa za udongo mchana. Hujitokeza juu usiku kwa kuchimba udongo kutumia miguu ya mbele. Wadudu hawa huharibu mizizi na hula majani ya miche michanga.




Zuia wadudu hawa kwa kutumia dawa yenye kiua sumu cha Carbaryl. Changanya gramu 50 ( vijiko vitano vikubwa vya chakula) vya dawa pamoja na kilo moja ya mchele, mtama au pumba za mahindi au ngano. Ongeza maji kidogo kwenye mchanganyiko huo na kisha mwaga kwenye njia wanazopita wadudu hawa.

<<< BOFYA HAPA KUSOMA SEHEMU YA PILI <<<


Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 26/11/2016

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم