Kilimo cha kabichi - sehemu ya nne (Growing Cabbage - Part four)


KILIMO CHA KABICHI SEHEMU YA 4 

B. Magonjwa
1. Kuoza Shingo (Bacterial Softrot)
Ugonjwa huu husababishwa na vijidudu vya bacteria ambavyo viko kwenye udongo. Hushambulia kabichi na kuzifanya zibadilike rangi, kuoza na kutoa harufu mbaya. Vijidudu vidogo vidogo pia huonekana kwenye sehemu iliyooza.


Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia yafuatayo;
(a) Epuka kujeruhi kabichi wakati wa kuvuna
(b) Vuna kabichi wakati hakuna mvua.
(c) Usilundike kabichi kwa wingi na kwa muda mrefu
(d) Hifadhi kwenye sehemu ya ubaridi na yenye kuingiza hewa ya kutosha
(e) Ng'oa masalia, choma moto na lima shamba mara moja baada ya kuvuna.
(f) Badilisha mazao.

2. Uozo mweusi (Blackrot)
Huu pia ni ugonjwa unaosababishwa na vijidudu vya bacteria na hushambulia sana kabichi. Dalili kubwa za ugonjwa huu ni majani kugeuka rangi na kuwa ya njano na baadae kikahawia. Majani huanza kunyauka toka kwenye kingo zake na kuacha alama ya "V". Kingo zinakua na rangi nyeusi isiyokolea. Baadaye majani yaliyoshambuliwa hudhoofika na kupukurika. Kama ukikaka jani au shina, mviringo mweusi huonekana kwenye vena. 



Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kuzingatia yafuatayo;
(a) Badilisha mazao kwa muda wa miaka miwili usipande kabichi na jamii yake.
(b) Panda kabichi kwenye sehemu ambayo haituamishi maji
(c) Kitalu na mazingira yawe safi daima.
(d) Punguza miche ili kupunguza msongamano
(e) Ondoa masalia yote ya kabichi shambani baada ya kuvuna na yachome moto.
(d) Panda mbegu zilizothibitishwa na wataalamu.

3. Kuoza Shina (Black leg)
Ugonjwa huu chanzo chake ni ukungu. Dalili kubwa za ugonjwa huu ni kuwepo kwa madoa yaliyodidimia yenye rangi ya kikahawia kwenye shina karibu na usawa wa ardhi, ikifuatiwa na kuvimba kwa shina. Baadaye uyoga mweusi huonekana kwenye uvimbe huo, Pia uozo wa rangi ya kikahawia huonekana ndani ya shina. Kwenye majani huonekana madoa meusi ya mviringo yaliyozungukwa na uyoga mweusi. 





Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia yafuatayo;
(a) Panda katika sehemu ambayo haituamishi maji.
(b) Badilisha mazao: kwa muda wa miaka mitatu usipande zao la kabichi na jamii yake kama kabichi ya kichina na koliflawa.
(c) Lima shamba mara baada ya kuvuna ili kuwezesha masalia ya mazao kuoza haraka kabla ya kupanda.
(d) Ondoa kabichi zote zilizoshambuliwa shambani.
(e) Tumia dawa za kuzuia magonjwa ya ukungu kama Linkmil 72 WP, Ivory 72 WP, madawa ya ukungu yanakua na viua sumu vya aina mbili yan Metalaxyl na Mancozeb. Dawa zenye kiua sumu cha mancozeb tu huwa sio nzuri kutumia kwa sababu Zikipigwa kwenye mmea zinabakia juu ya mmea tu (Contact), hazitibu mpaka ndani ya mmea. Kwa hiyo Dawa zenye Mancozeb pekee siyo nzuri kutumia, Tumia Dawa zenye mchanganyiko wa viua sumu viwili yan Mancozeb + Metalaxyl, Metalaxyl ni kiua sumu ambacho hupenyeza mpaka ndani ya mmea (Systemic) na hutibu vimelea vya ukungu kwa haraka na hubakia kwenye tishu za mmea kwa muda kidogo ambapo huzuia vimelea vya magonjwa pale vinapoanza tena. 

Dawa ya ukungu inayofaa ni ile yenye mchanganyiko wa viua sumu viwili (Mancozeb + Metalaxyl). Kwa hiyo chunguza pakiti au chupa ya dawa kutazama viua sumu hivyo, hakikisha vinakua viua sumu viwili (Mancozeb + Metalaxyl), Dawa yenye kiua sumu cha Mancozeb pekee zinafaa kutumiwa ila dawa zenye ziada ya Metalaxyl zina nguvu zaidi. Dawa zenye viua sumu viwili (Mancozeb + Metalaxyl) ni nyingi na zina Majina mengi mfano; Ivory 72 WP, Linkmil 72 WP, Mapato 72 WP na nyinginezo nyingi. Hivyo basi mbali na kuwepo majina mengi ya kibiashara hakikisha unachunguza kwenye pakiti au kopo uwepo wa viua sumu hivyo (Mancozeb + Metalaxyl).

<<< BOFYA HAPA KUSOMA SEHEMU YA TATU <<<


Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 26/11/2016

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم