Kilimo cha kabichi - sehemu ya tano (Growing Cabbage - Part five)


KILIMO CHA KABICHI SEHEMU YA 5

4. Uvimbe wa Mzizi (Clubroot)
Huu pia ni ugonjwa unaosababishwa na kuvu na ukungu. Hushambulia mizizi na dalili zake ni kudumaa kwa mmea na majani kukunjamana. Baadae mmea huoza.
Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kubadilisha mazao.





5. Madoajani Meusi (Black Leaf Spot)
Chanzo cha ugonjwa huu ni ukungu. Dalili zake ni kuonekana kwa madoa madogo ya mviringo yenye rangi ya njano kwenye majani. Baadae madoa haya huwa makubwa na hugeuka kuwa meusi.





Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia yafuatayo;
(a) Badilisha mazao
(b) Hakikisha shamba ni safi wakati wote.
(c) Ikibidi tumia dawa za ukungu kama vile Blue copper (Copperhydroxide, "Kocide" au Copper Oxychloride, "Cupro")

6. Ubwiri Vinyonya (Downy Mildew)
Huu ni ugonjwa wa ukungu ambao hupendelea sana hali ya unyevuunyevu na baridi kali na huonena zaidi kwenye kitalu. Dalili zake ni majani kuwa na mabaka ya mviringo yenye njano upande wa juu. Baadaye mabaka haya hubadilika na kuwa na rangi ya zambarau iliyochanganyika na nyeupe upande wa chini wa majani.



Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kutumia njia zifuatazo;
(a) Kilimo cha kubadilisha mazao
(b) Hakikisha udongo hautwamishi maji na kitalu ni kisafi wakati wote.
(c) Nyunyizia dawa za ukungu kama vile Blue copper (Copperhydroxide, "Kocide" au Copper Oxychloride, "Cupro"), Dithane M - 45, Ivory 72 WP, Linkmil 72 WP na nyinginezo.

7. Kuoza shina au Kinyaushi (Damping off or End Wire Stem)
Husababishwa na ukungu na hushambulia miche michanga. Miche iliyoshambuliwa huonyesha dalili za kunyauka, baadae huanguka na kukauka. Miche mikubwa huonyesha dalili za kudumaa. Sehemu ya shina iliyokaribu na ardhi hulainika na kuwa na rangj ya kikahawia.





Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kutumia njia zifuatazo;
(a) Punguza miche kama imesongamana.
(b) Nyunyiza dawa za ukungu kama Dithane M - 45, Linkimil 72 WP au Ivory M 72 WP (zenye mchanganyiko wa viua sumu vya Metalaxyl na Mancozeb)


KUVUNA NA KUHIFADHI
A. Kuvuna
Kabichi hukomaa na huvunwa baada ya siku 60 mpaka 120 kutegemea aina iliyostawishwa tangu kupandikiza miche. Uvunaji hufanyika kwa kukata shina sentimita mbili hadi tatu kutoka kwenye kichwa kwa kutumia kisu. Ondoa majani ya nje na acha majani mawili au matatu ya kijani kwa ajili ya kuzuia kabichi zisikwaruzike na kuoza wakati wa kusafirisha.

Punguza nusu ya urefu wa majani ya nje ili kurahisisha ufungaji. Kwa kawaida uvunaji hufanyika wakati wa asubuhi au jioni. Kiasi cha tani 40 au zaidi za kabichi kwa hekta hupatikana kama zao limetunzwa vizuri. Ondoa kabichi zilizooza au kuharibika wakati wa kuvuna. Kisha panga zilizobaki kufuata daraja kama vile ndogo, za kati na kubwa.

B. Hifadhi
Kabichi ni zao linaloharibika kwa haraka, hivyo halina budi kutumika mapema iwezekanavyo baada ya kuvuna. Kabichi kwa ajili ya kuuzwa zisafirishwe mara moja kwa walaji. Kama usafiri ni mgumu, zihifadhiwe kwenye sehemu yenye ubaridi na hewa ya kutosha. Wakati wa kusafirisha, ziwekwe kwenye matenga au visanduku vya mbao vilivyo na matundu yanayoingiza hewa ya kutosha.


*** MWISHO WA MAKALA HII ***

***ENDELEA KUFWATILIA MAKALA ZINGINE***

Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 26/11/2016

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم