KILIMO CHA KAROTI SEHEMU YA 1
KILOMO CHA KAROTI
Karoti hustawi vizuri kwenye sehemu zenye joto la wastani (nyuzi joto 15 hadi 27 za Sentigredi).
Kiasi cha mavuno yanayoweza kupatikana na ubora wa karoti, hutegemea sana aina ya udongo. Hivyo karoti hustawi vizuri katika udongo mwepesi, wenye rutuba ya kutosa, kina kirefu na usiotuamisha maji.
AINA
Kuna aina nyingi za karoti. Zifuatazo ni aina zinazolimwa hapa Tanzania.
1. Nantes
Karoti za Nantes ni ndefu, huvunjika kwa urahisi, zina umbo la kuchongoka na ncha kali. Aina hii hupendwa sana kutafunwa na walaji, kutokana na ladha yake tamu. Karoti za Nantes hazifai kwa kusindikwa.
2. Chantenay Red Core
Hizi ni nene kwa umbo, na zenye ncha butu. Unene wa nyama ya nje na ndani hulingana hivyo zinafaa sana kwa kusindikwa.
Huwa na rangi ya machungwa iliyofifia na ladha yake siyo tamu. Aina hii hustawi zaidi kwenye udongo mzito.
3. Oxheart
Karoti za Oxhert ni fupi na nene. Huvunwa baada ya mfupi kulinganisha na aina zingine.
4. Cape Market
Aina hii hupendwa sana kutafunwa zikiwa mbichi pia zinafaa kusindikwa.
5. Flacoro
Aina hii huzaa sana na mizizi yake ni mirefu. Hufaa kwa kuhifadhiwa na kusafirishwa, kwa sababu haziharibiki haraka.
6. Top Weight
Aina hii ina sifa kama za Flacoro.
KUTAYARISHA SHAMBA
Ili kupata mavuno mengi na bora, eneo la kupanda halina budi kutayarishwa vizuri. Iwapo shamba ni jipya, miti na visiki vyote vikatwe. Visiki na takataka zote ziondolewe shambani, Baada ya hapo shamba lilimwe vizuri na katika kina cha kutosha. Lainisha udongo ili kurahisisha uotaji wa mbegu za karoti ambazo ni ndogo sana.
Kama eneo lina udongo wa mfinyanzi au wa kichanga ni muhimu kuweka mbolea za asili zilizooza vizuri. Mbolea hizi hufanya udongo wa mfinyanzi uwe mwepesi wa kuweza kuruhusu maji na hewa kupenya kwa urahisi.
Endapo karoti zitastawishwa wakati wa mvua nyingi zipandwe kwenye matuta yaliyoinuliwa.
KUPANDA
Karoti hupandwa moja kwa moja shambani katika matuta au sesa. Kiasi cha gramu 80 (sawa na vijiko vidogo vya chai 16) kinatosha kupanda eneo la mita mraba 100. Hekta moja huhitaji kilo 8 za mbegu.
Hakikisha mbegu unazopanda zina uwezo wa kuota kwa kuzifikicha. Mbegu zenye uwezo wa kuota hutoa harufu kali unapozifikicha. Ili mbegu ziote haraka ziloweke katika maji kwa saa 24. Baada ya hapo changanya mbegu hizo na mchanga, kwa kiasi kinacholingana ili kupata mtawanyiko mzuri wa mbegu wakati wa kupanda.
Kama utapanda karoti katika matuta, tengeneza matuta yaliyoinuliwa kidogo, kiasi cha sentimita 10 mpaka 15. Matuta haya yawe na upana wa sentimita 60 na urefu wowote. Sia mbegu katika mistari yenye nafasi ya sentimita 30 mpaka 40 kati ya mstari na mstari na kina cha sentimita moja mpaka moja na nusu. Iwapo utapanda katika sesa tumia nafasi ya sentimita 40 mpaka 50, kati ya mstari na mstari.
Nafasi ya kupandia inategemea aina ya karoti inayokusudiwa kustawisha. Baada ya kupanda, weka matandazo kama vile majani makavu na kisha mwagilia maji asubuhi na jioni mpaka mbegu zitakapoota. Umwagiliaji utategemea hali ya hewa. Mbegu huota baada ya siku 10 mpaka 15. Zikishaota ondoa matandazo.
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
إرسال تعليق