Kilimo cha karoti - sehemu ya pili (Growing Carrot - Part two)


KILIMO CHA KAROTI SEHEMU YA 2

KUTUNZA SHAMBA

1. Kumwagilia maji
Hakikisha udongo una unyevu wa kutosha hasa siku za mwanzo. Karoti zilizokosa maji kwa muda mrefu huzaa mizizi midogo midogo. Pia udongo mkavu ukipata maji mengi ghafla husababisha karoti kupasuka. Hivyo mwagilia shamba mara kwa mara kuhakikisha udongo una unyevu wa kutosha wakati wote, kama hali ya hewa ni ya jua kali.

2. Kupunguza miche
Mimea ya karoti inahitaji kupunguzwa mara mbili. Mara ya kwanza hupunguzwa ikiwa na majani matatu mpaka manne au wiki mbili tangu kupandwa na kuachwa katika nafasi ya sentimita tano mpaka saba. Mara ya pili hupunguzwa ikiwa na urefu wa sentimita 10 mpaka 13, na kuachwa katika nafasi ya sentimita 10 mpaka 15. Karoti zinazopunguzwa zinaweza kutumika kwa chakula.

3. Palizi
Zao la karoti linahitaji kupaliliwa mara kwa mara. Palilia kwa kupandishia udongo na kuwa mwangalifu ili usikate mizizi.

4. Mbolea
Weka mbolea ya chumvichumvi aina ya S/A kama mbolea za asili hazikutumika wakati wa kupanda. Kiasi kinachotakiwa ni kilo 100 kwa hekta. Weka kilo 50 kwa hekta iwapo mbolea za asili zimetumika. Mbolea iwekwe wakati wa kupunguza miche mara ya pili. Weka katikati ya mistari na kwenye mifereji na kisha fukia.

5. Kuzuia Magonjwa na Wadudu waharibifu:

A. Magonjwa
a. Madoajani (Leaf Spot):
Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hutokea wakati karoti zina urefu wa sentimita 13 mpaka 15. Hushambulia majani na kuyafanya yawe na madoa yenye rangi nyeusi iliyochanganyika na kijivu au kahawia. Sehemu zinazozunguka madoa haya hubadilika rangi na kuwa njano. Ugonjwa ukizidi majani hukauka. 


Zuia ugonjwa huu kwa kunyunyizia dawa zozote za ukungu zenye viua sumu vifuatavyo;
(i) Mancozeb na metalaxyl
i.e Ivory M 72 WP, Linkmil M 72 WP etc
(ii) Copper
i.e Blue copper, Copper Hydroxide (Kocide)

b. Kuoza mizizi (Sclerotinia Rot)
Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hushambulia mizizi na majani. Dalili zake ni kuoza kwa mizizi na majani. Baadaye sehemu hizi hufunikwa na uyoga mweupe. Kwenye uyoga huu huota siklerotia kubwa zenye rangi nyeusi.


Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia yafuatayo;
(i) Epuka kustawisha karoti kwenye maeneo yaliyoshambuliwa na ugonjwa huu.
(ii) Nyunyiza dawa ya ukungu yenye Viua sumu vya [Mancozeb na Metalaxyl] au Copper

c. Karoti kuwa na mizizi Mingi (Folking)
Hii hutokea kama karoti zimepandwa kwenye udongo wenye takataka nyingi na usiolainishwa vizuri. Vile vile utumiaji wa mbolea za asili zisizooza vizuri unaweza kusababisha karoti kuwa na mizizi mingi. Hali hii inaweza kuzuiwa kwa kulainisha udongo vizuri na kutumia mbolea za asili zilizooza vizuri.

d. Madoa Meusi (Black Leaf Spot)
Huu pia ni ugonjwa na ukungu unaoshambulia majani na mizizi. Majani yaliyoshambuliwa huwa na rangi ya manjani ambayo baadaye hubadilika na kuwa kahawia. Mizizi huwa na madoa meusi yaliyodidimia. Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kwa kutumia mbegu zilizothibitishwa kitaalamu, kubadilisha mazao na kuepuka kujeruhi karoti wakati wa kupalilia, kuvuna au kusafirisha.


B. Wadudu
a. Minyoo Fundo
Minyoo hii hushambulia mizizi na kuifanya iwe na vinundu. Hali hii husababisha mmea kudumaa na kupunguza mavuno. Minyoo fundo huweza kuzuiwa kwa kubadilisha mazao. Baada ya kuvuna usipande mazao ya jamii ya karoti kama vitunguu au mazao yanayoshambuliwa na wadudu hawa. Unaweza kupanda mazao ambayo hayashambuliwi na minyoo fundo kama vile mahindi. Pia hakikisha shamba ni safi wakati wote.


b. Inzi wa Karoti
Mashambulizi hufanywa na funza ambaye hutoboa mizizi. Ili kuzuia wadudu hawa tumia dawa za wadudu zilizopo kwenye maduka ya pembejeo za kilimo. Pia badilisha mazao na wakati wa kupalilia pandishia udongo kufunika mizizi.



KUVUNA
Karoti huwa tayari kwa kuvuna baada ya wiki 10 hadi 12 tangu kupandwa kutegemea hali ya hewa. Wastani wa mavuno kwa hekta moja ni tanu 25 au zaidi.


*** MWISHO WA MAKALA HII ***

***ENDELEA KUFWATILIA MAKALA ZINGINE***

Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 26/11/2016

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم