Kilimo cha Pilipili Hoho - sehemu ya kwanza (Growing Bell Peppers - Part one)


KILIMO CHA PILIPILI HOHO SEHEMU YA KWANZA

Pilipili hoho ni moja ya mazao ya viungo ambalo hulimwa kwa wingi hapa nchini Tanzania. Zao hili hutumika kama kiungo kwenye vyakula mbalimbali. Vile vile hutumika katika katika kutengeneza kachumbari na huweza kukaushwa na kusagwa ili kupata unga.

Viinilishe vinavyopatikana katika pilipili tamu/Hoho ni vitamini A, B, C na madini aina ya chokaa na chuma.

MAZINGIRA
Zao hili hukua vizuri kwenye hali ya hewa yenye joto la waztani ( nyuzi joto 18 hadi 20) za Sentigredi, joto likizidi vichomozo, maua na matunda huanguka.

Huhitaji mwinuko wa kuanzia usawa wa bahari hadi mita 1500 na mvua za wastani kiasi cha milimita 600 hadi 1500.

Udongo unaofaa kwa zao hili ni ule wenye rutuba, mboji nyingi, kina kirefu na usiotuamisha maji.

AINA
Kuna aina nyingi za pilipili hoho. Baadhi ya aina zinazostawishwa nchini ni California Wonder, Emerald Giant, Sweet Neapotitan, Yolo Wonder, Pimiento na Keystone Resistant Giant. Aina nyingine ni kama vile Ruby King, Ruby Giant, Libert Bell na Tolo Wonder B.

KUPANDA MBEGU
Mbegu zinaweza kupandwa moja kwa moja shambani au kuoteshwa kwanza kwenye kitalu na baadaye kuhamishiwa shambani.

Kuoteshwa Mbegu Kitaluni:
Kabla ya kusia mbegu tengeneza tuta lenye upana wa mita moja. Urefu wa tuta utategemea eneo la shamba linalotarajiwa kupandwa. Weka mbolea za asili zilizooza vizuri kiasi cha ndoo mbili kubwa au zaidi katika eneo la mita mraba moja. Changanya mbolea na udongo vizuri, kisha tengeneza vifereji vyenye nafasi ya sentimita 10 hadi 15 kutoka kifereji hadi kingine. Kina cha kifereji kiwe sentimita moja hadi mbili, Sia mbegu kiasi cha gramu mbili hadi tatu katika eneo hilo, kiasi hiki kitatoa miche ambayo itatosha kupandikiza katika eneo la mita mraba 100.

Baada ya kusia fukia kwa kutumia udongo laini au mbolea za asili zilizooza vizuri. Weka matandazo na kisha mwagilia maji. Endelea kumwagilia kitalu kila siku asubuhi na jioni hadi mbegu zitakapoota. Mbegu huota baada ya siku sita hadi 10. Mara zitakapoota ondoa matandazo. Endelea kumwagilia maji hadi wakati miche inakuwa tayari kwa kupandikizwa.

KUTAYARISHA SHAMBA
Tayarisha shamba vizuri mwezi mmoja kabla ya kupandikiza miche. Katua ardhi katika kina cha kutosha sentimita 30 kwenda chini. Weka mbolea za asili kiasi cha tani 10 hadi 15 kwa hekta, kiasi hiki ni sawa na debe moja kwa eneo la mita mraba moja. Au kipindi cha kupandikiza weka kiganja kimoja au viwili cha mbolea hizo zilizooza viziri kwenye kila shimo. Changanya mbolea na udongo vizuri. Ikiwa eneo hilo lina upungufu wa madini aina ya fosiforasi kama itakavyothibitishwa na wataalam, weka mbolea ya chokaa aina ya TSP. Kiasi kinachotakiwa ni kilo 200 kwa hekta. Lainisha udongo siku tatu au tano kabla ya kupandikiza miche.

KUPANDIKIZA MICHE
Miche huwa tayari kwa kupandikizwa shambani baada ya wiki nne hadi 10. Wakati huu huwa na majani sita hadi manane na urefu wa sentimita 10 hadi 15.

Pandikiza miche katika nafasi ya sentimita 40 hadi 50 kutoka shimo hadi shimo na sentimita 60 hadi 75 kati ya mstari na mstari. Ikiwa mbolea za asili hazikuwekwa wakati wa kutayarisha shamba, weka kiasi cha nusu kilo hadi moja au viganja viwili vya mkono katika kila shimo la kupandia.

Siku moja kabla ya kung'oa miche, mwagilia tuta ili kulainisha udongo. Ng'oa miche pamoja na udongo wake kisha pandikiza katika kina cha sentimita mbili zaidi kuliko ilivyokuwa kwenye kitalu. Pandikiza miche wakati wa asubuhi au jioni. Mara baada ya kupandikiza mwagilia maji ya kutosha.


Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 26/11/2016

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم