KILIMO CHA NYANYA SEHEMU YA 4
Magonjwa
a. Magonjwa ya Bakajani (Eary and Late Blight)
Magonjwa haya husababishwa na ukungu. Hushambulia majani, shina na matunda
(i) Bakajani (Early Blight)
Dalili za ugonjwa huu huanza kuonekana kwenye kingo na pembe za majani. Kingo za majani huwa na madoa ya rangi nyeusi iliyochanganyika na kikahawia. Pembe zake huwa za njano. Shina huwa na madoa yanayofanana na yale yanayotokea kwenye majani lakini huwa yamesambaa na kuonekana zaidi. Baadae madoa haya hupanuka na kuwa mabaka makubwa yenye rangi nyeusi. Kwa kawaida mabaka haya huwa makavu na yaliyodidimia. Ugonjwa ukizidi mmea hudumaa na huvunjika kwa urahisi.
Matunda huwa na madoa meusi ya mviringo. Madoa haya huonekana zaidi kwenye kikonyo cha tunda na kwenye sehemu iliyopasuka. Kadri tunda linavyozidi kuiva, madoa haya huongezeka zaidi.
(ii) Bakajani (Late Blight)
Dalili za ugonjwa huu huanza kuonekana kwenye jani la chini. Majani na shina huwa na mabaka makubwa yenye rangi nyeusi au kikahawia nzito. Katika sehemu zenye hali ya hewa ya unyevuunyevu, majani huoza na hatimaye uyoga mweupe huonekana chini ya jani. Majani haya baadae hukauka na kuwa kama yaliyounguzwa na moto.
Matunda yaliyopatwa na ugonjwa huu huwa na madoa ya rangi ya kijani iliyochanganyika na kikahawia. Baadae madoa haya huwa makubwa na hatimae huoza. Ukipasua tunda lililoathiriwa utaona weusi. Nyanya zenye ugonjwa huu zikihifadhiwa kwenye sehemu yenye unyevu mwingi hutoa uyoga mweupe. Magonjwa ya bakajani yanazuiwa kwa kuzingatia yafuatayo:-
-Kubadilisha mazao
-Kuweka matandazo shambani
-Kupanda aina ya nyanya zinazovumilia mashambulizi ya magonjwa haya.
-kuweka shamba katika hali ya usafi kwa kuondoa masalia ya mazao shambani baada ya kuvuna.
-kupunguzia matawi na kuondoa majani yote yaliyoshambuliwa.
-Kutumia dawa za ukungu zenye viua sumu vya aina mbili yaani "Mancozeb na Metalaxyl" kama Linkmil M 72 WP, Ivory M 72 WP, Dithane - M 45, Ridomil, Topsin M 70. Pia inaweza kutumia dawa zenye "copper" kama Blue copper, Cupric Hydroxide (Champion) na Copper Oxychloride (Cupro).
b. Mnyauko Bakteria (Bacterial Wilt)
Ugonjwa huu husababishwa na vijidudu vya bakteria. Mmea ulioshambuliwa na ugonjwa huu hunyauka ghafla hasa wakati wa jua kali. Baadae mmea hudumaa, majani na vikonyo vyake hukunjamana. Kama shina likikatwa karibu na usawa wa ardhi, rangi ya kikahawia nzito huonekana kwenye sehemu zinazosafirisha maji. Sehemu iliyokatwa ikiwekwa kwenye maji, maji yenye rangi ya maziwa huchuruzika.
Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia yafuatayo:-
-kupanda nyanya kwenye sehemu ambayo haina ugonjwa huu.
-Kubadilisha mazao
-Kuepuka kuweka mbolea nyingi ya samadi au chumvi chumvi
-Kuotesha mbegu kwenye kitalu ambacho hakina ugonjwa huu.
-Kupanda nyanya zinazostahimili ugonjwa huu.
c. Mnyauko Fuzari (Fusarium Wilt)
Huu pia ni ugonjwa wa ukungu na kuvu. Husababisha majani yawe na rangi ya njano na mmea kunyauka hasa wakati wa jua kali. Majani yaliyoshambuliwa huvunjika kwa urahisi. Kama ganda la shina likinyofolewa karibu na usawa wa ardhi, rangi ya kikahawia huonekana. Ugonjwa huu huzuiwa kwa kuzingatia yafuatayo:-
-Kupanda aina za nyanya zinazostahimili ugonjwa kama ganda la shina kama ROMA na VFM
-Kung'oa mimea iliyoshambuliwa na kuichoma au kuifukia.
-Kutumia dawa kama vile Topsin M 70. Dawa hii iwekwe au inyunyuziwe kwenye udongo.
d. Ugonjwa wa Madoajani (Septoria Leaf Spot)
Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hushambulia majani. Majani yaliyoshambuliwa huwa na madoa meusi na kingo zake huwa na rangi ya kijivu ilioambatana na madoa madogo meusi. Zuia ugonjwa kwa kutumia dawa mbalimbali za ukungu kama Dithane - M 45, dawa zenye copper kama Blue copper na nyinginezo.
e. Batobato (Tobacco Mosaic Virus)
Huu ni ugonjwa unaosababishwa na virusi. Hushambulia majani machanga na yaliyozeeka. Majani machanga yaliyoshambuliwa hukunjamana na kudondoka. Halikadhalika majani yaliyozeeka hukunjamana, huvunjika kwa urahisi na huwa na rangi nyeusi, kijivu au kikahawia chini ya jani. Mwishowe majani hunyauka na kufa. Ugonjwa huu unazuiwa kwa kuzingatia yafuatayo:-
-Kung'oa na kuchoma mimea yote iliyoshambuliwa
-Kupanda mbegu zilizothibitishwa kitaalam
-Kupanda aina za nyanya zinazostahimili magonjwa ya batobato.
-Kuepuka kuhudumia mimea ambayo haina ugonjwa baada ya kuhudumia mimea yenye ugonjwa. Ikiwezekana osha mikono kabla ya kuhudumia mimea mingine.
-Kutovuta sigara ndani ya shamba la nyanya.
-Kusafisha vifaa vyote kama vile visu, mikasi kwa maji na sabuni baada ya kuvifanyia kazi.
f. Tomato Yellow Leaf Curl
Ugonjwa huu husababisha majani kujifunga kuelekea ndani. Kilele cha mmea huonyesha rangi ya njano. Mmea hudumaa na baadae hushindwa kutoa matunda mengi. Jani hupoteza umbo lake la kawaida na kuwa kama ufagio. Ugonjwa huu huenezwa na inzi weupe (white flies), hivyo zuia wadudu hawa kwa kutumia dawa za kuua wadudu waharibifu kama Actellic 50 EC na nyinginezo. Vilevile usivute sigara ndani au kando kando ya shamba.
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
إرسال تعليق