Kilimo cha Pilipili Hoho - sehemu ya tatu (Growing Bell Peppers - Part three)


KILIMO CHA PILIPILI HOHO SEHEMU YA 3

B. Magonjwa
(i) Magonjwa ya virusi
Magonjwa haya hutokana na virusi. Husababisha majani kudumaa, kukunjamana, na kuwa na rangi ya njano. 


Ili kuzuia magonjwa haya, zingatia yafuatayo;
- Panda aina ya pilipili zinazostahimili mashambulizi ya magonjwa haya.
- Ng'oa miche inayoonyesha dalili za magonjwa haya.
- Zuia wadudu wanaoeneza magonjwa ya virusi kwa kutumia dawa kama Actellic 50 EC, Diazinon, Dimethoate na dawa zinginezo nyingi.
- Badilisha mazao. Baada ya kuvuna pilipili hoho/pilipili tamu, zao linalofuata lisiwe la jamii ya zao gili kwa mfano nyanya na bilinganya.

(ii) Chule (Anthracnose)
Ugonjwa huu husababishwa na ukungu. Hushambulia matunda na kuyasababisha kuwa na makovu ya mviringo yenye rangi nyeusi iliyochanganyika na kahawia.



Zuia ugonjwa huu kwa kunyunyiza mojawapo ya dawa zifuatazo: Dithane M45, Topsin, Ridomil au Kocide, au dawa zingine zenye viuasumu vifuatavyo;
- Mancozeb na Metalaxyl
- Copper i.e Blue copper

(iii) Madoa Bakteria (Bacterial Leaf Spot)
Ugonjwa huu husababishwa na viini vya bacteria. Hushambulia majani machanga na baadaye matunda. Dalili zake ni kuonekana kwa madoa ya njano kwenye majani na matunda. Zuia ugonjwa huu kwa kupanda mbegu zilizothibitishwa na wataalamu.


(iv) Kuoza Mizizi (Root Rot)
Huu ni ugonjwa wa ukungu unaoshambulia mizizi na kusababisha kuoza. Mimea hunyauka na hatimaye hufa. Ugonjwa huu hupendelea sana hali ya unyevuunyevu na joto jingi, hivyo zuia hali hii kwa kuepuka kupanda pilipili kwenye sehemu inayotuamisha maji.



(v) Mnyauko Verticilium (Verticilium Wilt)
Huu pia ni ugonjwa unaoletwa na ukungu ambao hupatikana kwenye udongo. Hushambulia shina na kulisababisha libadilike rangi na kuwa ya kahawia. Baadaye mmea hunyauka na kufa. Unaweza kuzuia ugonjwa huu kwa kubadilisha mazao.


KUVUNA
Pilipili hoho huwa tayari kwa kuvunwa baada ya wiki 10 hadi 14 tangu kupandikiza miche. Uvunaji huendelea kwa muda wa wiki nane hadi 10. Muda wa kuvuna hutegemea aina na matumizi. Pilipili kwa ajili ya matumizi ya nyumbani huvunwa zingali na rangi yake ya kijani kibichi inayong'aa. Zile za kusindika kiwandani huvunwa zikiwa zimekomaa na zenye rangi nyekundu. Matunda yakivunwa yangali machanga hunyauka kwa urahisi, husinyaa na kupunguza wingi wa mazao. Wastani wa mavuno kwa hekta ni tani 30 hadi 45.


*** MWISHO WA MAKALA HII ***

***ENDELEA KUFWATILIA MAKALA ZINGINE***

Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 27/11/2016

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم