Kilimo cha Vitunguu - sehemu ya tatu (Growing Onions - Part three)



KILIMO CHA VITUNGUU SEHEMU YA 3

B. Wadudu waharibifu

a. Sota (Cutworms)
Hawa ni funza wenye rangi ya kijivu. Hupendelea kujichimbia katika udongo wakati wa mchana, na wakati wa usiku hukata miche michanga karibu na usawa wa ardhi.



Zuia wadudu hawa kwa kutumia majivu au dawa kama vile Sevin, Sumicidin na Decis mara baada ya kupanda. Kama mche utakatwa, mtoe mdudu kwa kumfukua na kumwua, kisha pandikiza mche mwingine.

Njia nyingine ya kumzuia mdudu huyu ni kuweka shamba na mazingira yake katika hali ya usafi ili wasiweze kuzaliana kwa wingi. Ikiwezekana tifua udongo bila kupanda zao lolote kwa muda wa mwezi mmoja.

b. Vithiripi (Onion Thrips)
Ni vidudu vidogo vyenye rangi ya kijivu iliyochanganyika na kikahawawia. Mashambulizi hufanywa na funza ambao wana rangi ya njano iliyopauka. Hushambulia majani na kuyasababisha kuwa na michirizi meupe inayong'aa. Mashambulizi yakizidi majani hunyauka na mwishowe mmea hukauka na kufa. 






Zuia vidudu hivi kwa kutumia dawa kama vile Actellic 50 EC, Sevin, Cypermethrin, Sumicidin na Dimecron.

KUVUNA
Vitunguu huwa tayari kwa kuvunwa baada ya miezi mitatu mpaka mitano (Siku 90 hadi 150) tangu kusia mbegu, kutegemea aina ya mbegu na hali ya hewa. Anza kuvuna vitunguu uonapo asilimia 50 ya vitunguu vimelegea na kunyauka. Ukivuna vitunguu kabla havijakomaa huharibika mapema. Wakati wa kuvuna, ng'oa shina zima na kata majani ya juu na mizizi. Baada ya kuvuna kausha vitunguu vizuri katika sehemu yenye hewa ya kutosha, na ambayo haina unyevu wala jua kali.

KUHIFADHI
Kabla ya kuhifadhi vitunguu, hakikisha vimekauka vizuri. Hifadhi vitunguu vilivyokauka vizuri katika sehemu yenye hewa ya kutosha, isiyokuwa na unyevu wala jua kali. Vitunguu visipokauka vizuri vitaoza. Hifadhi vitunguu kwa kutandaza juu ya chanja au funga pamoja mashina yake yaliyokauka na yaning'inize kwenye sehemu ya kuhifadhi ili vitunguu vikauke vizuri. Vitunguu vinaweza kuhifadhiwa kwa muda wa miezi mitatu hadi sita kama hali ya hewa haina unyevu. Aina ya vitunguu vidogo huweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu zaidi kuliko aina kubwa.

MAVUNO
Mavuno hutegemea utunzaji mzuri wa shamba, hali ya hewa na aina ya mbegu. Zao lililotunzwa vizuri huweza kutoa tani 30 hadi 40 kwa hekta.

KUBADILISHA MAZAO
Vitunguu ni zao linalotumia chakula kingi ardhini hivyo baada ya kuvuna lifuatiwe na zao linalotumia chakula kidogo ili kuhifadhi rutuba. Aidha baada ya kuvuna vitunguu, zao linalofuatia lisiwe la jamii moja na vitunguu kama vile vitunguu Saumu na Liki ili kuzuia kuenea kwa magonjwa na wadudu wanaoshambulia aina hii ya mazao.


*** MWISHO WA MAKALA HII ***

***ENDELEA KUFWATILIA MAKALA ZINGINE***

Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 27/11/2016

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم