Kilimo cha matikiti - Sehemu ya pili (Growing Watermelons - Part two)


KILIMO CHA MATIKITI SEHEMU YA PILI

AINA ZINGINE ZA MATIKITI

8. Sugar Baby 
Aina hii inakomaa kwa siku 75, ni tamu sana inakua na uzito hadi kufikia kilogram 4, ni nyekundu kwa ndani na inavutia, mashina yake ni mafupi ambayo ni mazuri ukiwa na eneo dogo la kupanda.


9. Moon and Stars 
Aina hii inakomaa kwa siku 95, ina rangi ya kijani iliyochangamana na weusi pamoja madoa ya njano yanayofanana na mwezi pamoja na nyota zikiwa angani wakati wa usiku, pia ni matikiti matamu yenye rangi nyekundu au pinki kwa ndani. Uzito wake unafikia kilogramu 18.


10. Yellow Crimson 
Aina hii inakomaa kwa siku 80, ina umbo la mviringo na hufikia uzito wa kilogramu 9, kwa ndani yana rangi ya njano mpauko na mbegu nyeusi pia ni matamu sana.


11. Orange Tendersweet 
Aina hii inakomaa kwa siku 85, kwa ndani yana rangi ya njano mpauko na mbegu zake ni nyeupe, ni matamu na laini, Uzito wake hufikia kilogramu 11.


12. Kleckley’s Sweet 
Aina hii inakomaa kwa siku 85, ni tamu sana na kwa ndani yana rangi nyekundu na mbegu nyeupe, Uzito wake hufikia kilogramu 18.



13. Big Crimson
Aina hii inakomaa kwa siku 90, yana rangi ya kijani iliyochangamana na nyeusi, kwa ndani yana rangi nyekundu na ni matamu sana. Uzito wake hufikia kilogramu 13.


14. Louisiana Sweet
Aina hii hukomaa kwa siku 90, kwa ndani zina rangi nyekundu mpauko, ni tamu sana na zina mbegu nyeusi. Uzito wake hufikia kilogramu 11.


15. Georgia Rattlesnake
Aina hii hukomaa kwa siku 90, matunda yake yana michrizi ya rangi ya kijani mpauko inayofanana na ngozi ya nyoka, kwa ndani yana rangi ya pinki na ni matamu sana. Uzito wake hufikia kilogramu 13.

....Picha yake itakujia hivi karibuni.

16. Congo
Aina hii hukomaa kwa siku 90, yana umbile la mviringo, kwa nje yana michirizi ya kijani, kwa ndani ya rangi nyekundu, ngozi nene ya ndani na matamu sana. Uzito wake hufikia kilogramu 16.

....Picha yake itakujia hivi karibuni.

17. Snack Pack
Aina hii hukomaa kwa siku 75, matunda yake yana ngozi ngumu yenye rangi ya kijani iliyochangamana na nyeusi na yana umbile la mviringo, kwa ndani yana rangi nyekundu, hayana mbegu na ni matamu. Uzito wake hufikia kilogramu 1 hadi 2.

....Picha yake itakujia hivi karibuni.

18. Sugarlee
Aina hii hukomaa kwa siku 85, yanahimili sana magonjwa, yana michirizi ya kijani, kwa ndani yana rangi nyekundu na ni matamu sana. Uzito wake hufikia kilogramu 7.



MAZINGIRA
Matikiti maji hayapendi hali ya ubaridi, ila yanapenda hali ya joto kuanzia nyuzi joto 18 mpaka 35 za sentigredi (18 – 35 ºC). Nyuzi joto Zaidi ya 35ºC au chini ya 10ºC husababisha matikiti kukua kwa kusuasua na kutokuzaa matunda yanayofaa. Matikiti maji yanahitaji udongo tifutifu usiotwamisha maji. Udongo wenye mchanga mwingi haufa kwa zao hili kwani unakuwa na uwezo mdogo wa kutunza maji.

KUANDAA SHAMBA
Andaa shamba vizuri na lima kina cha kutosha mpaka sentimita 30, ili kuufanya udongo uwe na uwezo wa kuupa mmea virutubisho vya kutosha. Unapoandaa shamba la Matikiti, ukubwa wa shamba ni jambo la msingi sana kuzingatia kwa sababu shina la tikiti lina matawi mengi sana yanayotambaa. Matawi hayo hukua hadi kufikia urefu wa mita 4 – 5.

KUPANDA
Wakati wa kupanda matikiti, mbegu hupandwa moja kwa moja shambani. Mmea wa matikiti haupendi kubugudhiwa mizizi yake, kwa hiyo kupandikiza miche ya matikiti hupelekea miche kushindwa kukua na hatimae kufa.

Mbegu za Matikiti Maji hupandwa Moja kwa Moja shambani, Nafasi inayofaa kwa matikiti ya aina zote ni mita 1.5 hadi 2 kutoka mstali hadi mstali na mita 1 kutoka mche hadi mche. Matikiti hukua vizuri maeneo yenye joto kwa kutumia umwagiliaji au mvua. Pia matikiti yanafanya vizuri maeneo yenye mwinuko hasa kipindi cha joto au kiangazi kwa kutumia umwagiliaji.

Unapotumia umwagiliaji hakikisha umeweka miundombinu mizuri itakayohakikisha upatikanaji wa maji muda wote, kwa sababu ukosefu wa maji kwa kipindi kidogo tu hufanya matunda kupata mshituko na kuathiri ukuaji wake.

Kipindi cha kupanda ni vizuri kutumia mbolea za asili kama samadi kwa kuiweka chini ya udongo na kuichanganya vizuri. Matikiti maji yanakua vizuri kwenye udongo wenye Alkali nyingi. Kwa hiyo inashauriwa kuongeza madini ya chokaa kwenye udongo ili kudumisha hali ya Alkali, hii inatakiwa ifanywe kila baada ya miaka 3.

Mbegu za matikiti huota baada ya siku 7 na matunda yanaanza kuonekana baada ya siku 30. Pia inaaminika kwamba virutubisho aina ya Boron husaidia mmea kutengeneza matunda matamu, kwa hiyo mkulima atumie mbolea za maji za wenye majani (Foliar fertilizer) zenye virutubisho vya Boron pamoja na virutubisho vingine ili kuboresha ustawi wa mmea.

MAJI
Matikiti maji yanahitaji maji ya kutosha na rutuba nyingi. Kwa hiyo inatakiwa mkulima awe na chanzo cha uhakika cha maji pia udongo wa shamba lake uwe na rutuba ya kutosha. Pia mkulima anashauriwa atumie mbolea za asili kwenye shamba lake.

MWANGA WA JUA
Kama unavyojua kwamba Matikiti yanahitaji maji mengi basi pia yanahitaji Jua la kutosha. Ni vizuri kutambua kwamba matikiti maji hayapendi hari ya hewa hatarishi kama baridi kali au joto kali yanahitaji joto la wastani kuanzia 20°C hadi 25°C, hali hii ya joto ni nzuri kwa kukuza na kuivisha matikiti. Unyevu unyevu mwingi na baridi kali au joto kali husababisha magonjwa ya ukungu.


Makala hii Imehaririwa mara ya mwaisho tarehe 05/07/2017

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم