Tangawizi (Zingiber Officinale) ni zao lenye manufaa sana kwa afya ya binadamu kama kusaidia Kurekebisha mmeng'enyo wa chakula, kurudisha hamu ya kula, kutibu maumivu mwilini, kutibu mafua na kikohozi na manufaa mengine mengi.
Mzizi wa tangawizi (rhizome) unaweza kuliwa ukiwa ulivyo (mbichi), ukitengenezwa na kuwa unga, kama viungo vya mboga, pia katika hali ya juisi.
AINA (TYPES)
Kuna aina kuu mbili za Tangawizi; Tangawizi zenye mizizi mikubwa na Tangawizi zenye mizizi midogo.
MAZINGIRA (ENVIRONMENT)
Tangawizi inakubali vizuri kwenye udongo wa aina mbalimbali, cha msingi udongo lazima uwe tifu tifu, usiwe mfinyazi. Kama ilivyo kwa mazao mengine Tangawizi inapenda idongo wenye asidi kwa mbali wenye pH kati ya 6.1 - 6.5. Au udongo ambao mazao kama mahindi, maharage na mengine yakiota vizuri basi Tangawizi inaweza kuota vizuri. Tangawizi inapendelea hali ya joto la 22°C hadi 25°C.
KUPANDA (PLANTING)
Tangawizi hupandwa kwa kutumia mizizi yake (Rhizome) au tangawizi zenyewe. Mara nyingi mbegu ambazo zimetoa machipukizi (sprouts or buds) ndio nzuri kupanda.
Kuandaa mbegu kata vipande vidogo vidogo vyenye sentimita 2.5 - 3.7 venye chipukizi moja au mawili.
Kama unategemea mvua kwa zao la tangawizi, Panda mwishoni mwa kipindi cha kiangazi kama mwezi wa 10 au mwanzo mwa kipindi cha masika kama mwezi wa 11.
Panda Tangawizi kwa kutumia matuta yenye kimo cha entimita 15 - 20 na matuta hayo yaachane kwa urefu wa sentimita 20 - 25 tuta hadi tuta. Tangawizi hupandwa kwa uachano wa sentimita 30 shina hadi shina. Wakati wa kupanda fanya yafuatayo;
1. Kipindi cha kuaandaa matuta jaziliza udongo wenye kimo cha sentimita 5 kwenye matuta yote.
2.Tandaza mbegu zako kwa kufwata uachano wa sentimita 30 mbegu hadi mbegu.
3. Jaziliza udongo kwenye hizo mbegu ili ukamilishe tuta lenye kimo cha sentimita 15 - 20.
4. Baada ya hatua no. 3 hapo juu, Mwagia maji kiasi (Usimwagie maji mengi).
MATUMIZI YA MBOLEA (FERTILIZER USE)
Mbolea ya samadi iliyooza vizuri inafaa sana kwa kilomo cha Tangawizi, kwa hekta moja Tani 5 - 6 za mbolea ya samadi huitajika. Kirutubisho aina ya Phosphate huitajika sana kwa Tangawizi, Unaweza ukatumia mbolea ya DAP au TSP. Mfuko mmoja wa kilo 50 unatosha kwa ekari moja.
Pia unaweza ukatumia mbolea za maji (Foliar fertilizer) kama Booster na nyinginezo.
Shamba la Tangawizi lililohudumiwa vizuri;
MAGONJWA (DISEASES)Shamba la Tangawizi lililohudumiwa vizuri;
Photo: http://www.africa-uganda-business-travel-guide.com/
Soft rot au Rhizome ni ugonjwa mkuu sana wa tangawizi, Ugonjwa huu huozesha mizizi ya tangawizi (rhizome) na kisababisha mmea kufa. Ugonjwa huu husababishwa na ukungu (Fungi).
Kudhibiti Ugonjwa (Disease Control)
1. Chagua eneo la shamba lisilotwamisha maji, hali ya kutwamisha maji hupelekea tangawizi kupata ugonjwa.
2. Tumia njia mbali mbali kwa pamoja kudhibiti ugonjwa huu (Integrated disease management) kama; usafi wa shamba, matumizi ya dawa za kudhibiti magonjwa ya ukungu na nyinginezo.
WADUDU WAHARIBIFU (INSECT PEST)
Black cutworm ni kiwavi wa kipepeo anaeathiri miche ya mazao yaliyo mengi ya mboga mboga. Ni mdudu hatari sana kwa miche michanga. Mara nyingi anakata mche wa tangawizi kwa usawa wa udongo au anakula shina kidogo na kukata sehemu ya kati ya shina hatimae husababisha majsni kukauka, na hubadirika kuwa rangi ya njano na mmea hufa ghafra.
Kudhibiti Mdudu huyu (Insect pest Control)
1. Weka shamba katika hali ya usafi, kwa kuondoa magugu.
NB:
Kwenye makala hii nimeelezea ugonjwa mmoja na mdudu mmoja, siku zinazokuja nitaongeza magonjwa mengine na wadudu wengine waharibifu. Endelea kuwa nami.
KUVUNA (HARVESTING)
Tangawizi inakuwa tayari kwa kuvunwa baada ya miezi 8 hadi 10, itategemea na aina ya mbegu na hali ya hewa. Tangawizi iliyokomaa, majani yake huwa ya njano na huanza kukauka na kuanguka.
Wakati wa kuvuna uwe muangalifu sana tumia koleo (spade or digging fork) kutoa tangawizi kwenye udongo. Tenganisha tangawizi na majani makavu.
Unashauriwa kuacha tangawizi shambani bila kuvuna kwa mwaka wa kwanza ili Uvune kwa mwaka wa pili, hii itasaidia kuchipua tena na kuongeza mavuno kwa kwa mwaka wa pili.
Mavuno ya Tangawizi yanatofautiana kutokana na sababu nyingi ikiwemo Rutuba ya udongo, hali ya hewa (Mvua), aina ya mbegu na sababu nyinginezo. Kama utalima vizuri na hali ya hewa ikawa nzuri utavuna Tani 2 hadi Tani 8 kwa ekari au Tani 15 - 25 kwa hekta moja.
Makala hii imehaririwa Mara ya mwisho tarehe: 12/07/2017
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
إرسال تعليق