Ufugaji wa Kuku wa kienyeji - Sehemu ya kwanza (Indigenous Chicken Farming - Part one)


Kuku wa kienyeji wanafugwa na wananchi waliowengi nchini Tanzania, hii inatokana na urahisi wa kufuga pia hawaitaji miundombinu ya ghali sana. Mara nyingi kwenye mazingira yetu kuku hawa hufugwa kwa kuwaachia watafute chakula chao wenyewe (Free-range-system). Katika makala hii nitakueleza namna ya kufuga vizuri kuku wa kienyeji kwa njia za kisasa, ili uongeze uzalishaji na kukuza kipato chako.

KUANDAA BANDA
Kwa mazingira yetu ya Afrika mashariki, ambapo maeneo mengi ni joto unatakiwa ujenge banda lenye uwazi upande mmoja ili kuruhusu hewa kupita ndani ya banda. Kitu kingine cha msingi inatakiwa banda la kuku liwe uelekeo wa Mashariki-Magharibi, hii itapunguza mwangaza wa jua unaoingia ndani ya banda na kuweka hali ya ubaridi bandani. Kuku hawali chakula vizuri kwenye banda lenye joto kwa hiyo hali hii ikiwepo inatashusha uzalishaji.

Kuku wa Kienyeji wanapenda sana kuzunguka zungunga, na kuparua kwenye udongo, unapojenga banda ni vizuri kuacha eneo nje ya banda kwa ajili ya kuku kujitawala zaidi. Kwa usalama zaidi unaweza ukajenga wavu kuzunguka banda ili iwe sehemu kushinda kuku wakati wa mchana. Tazama picha za mabanda bora utakayoweza kujenga ili uboreshe mradi wako wa kuku.






KUCHAGUA KUKU WA MBEGU (BREEDING STOCK)

Kabla ya kuanza mradi wa kuku, ni vizuri uchague mbegu inayofaa kwa kuangalia yafuatayo;
1. Chagua jogoo mwenye afya na mwenye umbile kubwa na mwenye nguvu.
2. Chagua kuku jike (Temba) ambae hana tabia ya kususa mayai wakati wa kuatamia na anaewalea watoto wake vizuri.

NB:
Kama utatumia kifaa cha kutotoreshea mayai (Incubator) au mama kuku au kuku mwingine (broody hen), tumia mayai yaliyotagwa si zaidi ya siku 14 (wiki 2)

SABABU ZINAZOPUNGUZA UZALISHAJI WA KUKU WA KIENYEJI
1. Changamoto kubwa ya kuku hawa wa kienyeji ni kiwango kidogo cha kutaga mayai chini ya asilimia 60% na maranyingi hufika hatima ya kutaga haraka sana tofauti na kuku wa kisasa ambao utagaji mayai hufikia hadi asilimia 80%.
2. Kufuga kuku hawa kwa njia ya kisasa ni gharama sana na mara nyingine unakuta unashindwa kurudisha gharama za uzalishaji. Lakini kama mfugaji atajipanga vizuri kimkakati anaweza akapunguza hasara na kuongeza faida.

3. Ugonjwa wa Kideli (New castle disease) husababisha kuku wengi kufa kwa wakati mmoja, hivyo kuathiri kipato cha mfugaji kwa kiwango kikubwa
4. Ndui ya kuku (Fowl Pox/pimple head) husababisha uzalishaji kupungua.
5. Chawa, kupe na utitiri ambao jhusababishwa na uchafu bandani hupunguza uzalishaji wa kuku.
6. Minyoo inayosababishwa na majeraha yaliyotokana na ndege wengine
7. Damu inayoonekana kwenye kinyesi inayotokana na Muharo mwekundu (Coccidiosis), homa ya matumbo (Fowl typhoid) au homa ya kipindupindu (Fowl cholera) husababisha kuku kukua taratibu sana na kudumaa na kuwa dhaifu.
8. Utotoaji wa kiwango kidogo unaotokana na kuhifadhi mayai machafu (yenye damu au uchafu), pia kutumia mayai yenye umri zaidi ya siku 14 kutoka kwa kuku wenye mbegu za ubora wa chini.


Makala hii Imehaririwa Mara ya mwisho Tarehe: 13/07/2017

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم