Kilimo bora cha Nyanya Chungu (Growing African Eggplant)


Nyanya chungu ni zao jamii ya mbogamboga linalotumika kwa matumizi mengi kama mboga, dawa n.k. Zao hili hustawi maeneo yenye halijoto tofauti tofauti nchini Tanzania.

MAZINGIRA
Zao hili hustawi vizuri maeneo yenye baridi ya wastani na joto la wastani kuanzia nyuzi joto 25°C hadi 35°C, hupendelea udongo tifu tifu usiotwamisha maji na wenye rutuba. Kama utaweza kutumia mbolea za samadi na mboji au mbolea za asili pamoja na mbolea za viwandani, basi nyanya chungu hustawi vizuri sana.

AINA
Kuna aina kuu mbili za nyanya chungu, nyanya chungu zinazopendelea hali ya joto na nyanya chungu zinazopendelea hali ya joto na baridi. Aina zote hizo mbili hulimwa nchini Tanzania.

KUANDAA KITALU
Mbegu za nyanya chungu huandaliwa kwenye kitalu kwanza kabla ya kupelekwa shambani. Yafuatayo ni maelekezo ya kuandaa kitalu cha nyanya chungu.
  • Chagua eneo la kuanzisha kitalu kwenye maeneo yanayopatikana maji kwa urahisi.
  • Inua udongo wa kitalu hadi kufikia kimo cha sm 20 na upana wa mita 1 na urefu wowote. Bonda bonda mabonge makubwa ya udongo ili kupata udongo laini.
  • Weka mbolea ya asili iliyooza vizuri, changanya ndoo moja kubwa ya lita 20 ya mbolea hiyo kwa eneo la mita 1 kwa mita 1 (1 m2). Kwa hiyo kama tuta lako la kitalu lina urefu wa mita 5 na upana mita 1, utaweka ndoo 5 za mbolea za asili.
  • Kama ni wakati wa kiangazi, mwagilia tuta lako kwa siku 3 mfululizo mpaka udongo uloane vizuri.

KUSIA MBEGU
Baada ya tuta lako kuloana vizuri, siku inayofuata usimwagie maji bali usie mbegu. Yafuatayo ni maelekezo ya namna ya kusia mbegu kwa usahihi.
  • Tengeneza vimifereji vyenye kina cha sm 2 kukatisha tuta, nafasi kati kimfereji kimoja na kingine ni sm 15 au nusu rula.
  • Sia mbegu zako ndani ya vimifereji hivyo, halafu funika na udongo laini.
  • Weka matandazo ya nyasi juu ya tuta ili kuzuia jua kali na matone ya maji ya moja kwa moja.
  • Mwagilia maji kitalu chako juu ya nyasi asubuhi na jioni kila siku. Ila inashauriwa kumwagilia kitalu chako maji wakati wa jioni.
  • Mbegu za nyanya chungu huota baada ya siku 10 hadi 14 tangu kusia. Baada ya mbegu kuota toa matandazo ya nyasi halafu yaweke matandazo hayo katikati ya mistari ya miche.
  • Tengeneza kivuli cha matandazo ya nyasi juu ya kitalu chenye kimo cha mita moja, kivuli hicho cha nyasi lazima kiwe kinapitisha mwanga wa jua walau kidogo ili kuruhusu mwanga kuifikia miche.

KUPANDIKIZA MICHE SHAMBANI
Miche huwa tayari kuhamishiwa shambani baada ya mwezi mmoja hadi mwezi mmoja na nusu tangu mbegu kuota. Nafasi ya kupandikiza nyanya chungu ni mita 1 kwa mita 1 (yaani mita 1 shina hadi shina na mita 1 mstari hadi mstari)

Kabla ya kupandikiza miche chimba mashimo yenye ukubwa kiasi, weka samadi iliyooza vizuri kiasi cha mkono mmoja uliojaa, halafu fukia udongo kiasi. Baada ya kufukia udongo pandikiza mche wako, kila shimo mche mmoja. Kama ni kipindi cha kiangazi pandikiza wakati wa jioni, baada ya kupandikiza mwagili maji vizuri.

KUTUNZA SHAMBA
Mimea jamii ya mbogamboga ikiwemo nyanya chungu haipendi bugudha ya magugu shambani, kwa hiyo hakikisha unafanya palizi wakati wote kuakikisha magugu hayaathiri ustawi wa mmea.

Dhibiti magonjwa na wadudu mabalimbali wanaoathiri zao hili, kwa kutumia madawa mabalimbali na matumizi ya mbolea mbalimbali za kurutubisha mimea pale inapobidi kama Mbolea za chumvi chumvi ( UREA, NPK, CAN n.k) au Mbolea za maji (BOOSTER).

Muhimu*
Magonjwa mbalimbali na wadudu wanaoathiri zao hili nitayaongeza kipindi kijacho, endelea kutembelea blogi hii ili upate mambo mengi mazuri yatakayokujenga.

Picha: Shamba la nyanya chungu lililostawi vizuri

KUVUNA
Nyanya chungu huwa tayari kuvunwa ndani ya siku 90 hadi 120 tangu kupandikiza. Kutegemeana na uhitaji wa soko, nyanya chungu inaweza kuvunwa mara 1 au mara 2 kwa wiki. Mavuno ya nyanya chungu yanaweza kuendelea mpaka miezi sita kama utahudumia vizuri mimea yako. Matunda ya nyanya chungu yanatakiwa kuvunwa kabla hayajabadilika rangi kutoka nyeupe kwenda njano mpauko. Matunda ya nyanya chungu inatakiwa yavunwe kwa utaratibu mzuri ili kuongeza uzalishaji.

Matunda ya nyanya chungu yaliyovunwa yanatakiwa yatumike ndani ya wiki moja ya kuvunwa. Vilevile matunda haya ya nyanya chungu yanaweza kusindikwa kuwa unga. Ili kusindika nyanya chungu kuwa unga fwata hatua zifuatazo;
  • Chagua nyanya chungu bora na zioshe kwenye maji
  • Kata kata nyanya chungu hizo kutengeneza vipande vidogo dogo, halafu tandaza vipande hivyo kwenye mkeka au turubai safi
  • Anika vipande hivyo vya nyanya chungu juani hadi vikauke.
  • Baada ya vipande hivyo kukauka vizuri, visage kwa kutumia kinu au mashine ya mkono mpaka viwe unga.
  • Tunza unga huo kwenye chombo kisafi ambacho hakingizi hewa.
  • Unaweza kutumia unga huo kwenye maharage, karanga, nyama na mboga zingine, mboga iliyowekwa unga huu wa nyanya chungu inakua tamu mno na inakua na virutubisho vya kutosha.

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

5 تعليقات

  1. Nina Gogwe ila zinakauka zenyenyewe na mizizi iko kama imeliwa, nifanyeje au ni dawa gani nzuri ya kutumia?

    ردحذف
    الردود
    1. أزال المؤلف هذا التعليق.

      حذف
    2. Habari ndugu Frank S? Nimechelewa kukujibu kutokana na majukumu mbalimbali ya hapa na pale.

      Tatizo la nyanya chungu zako kunyauka husababishwa na vimelea na minyoo midogo inayoitwa 'root-knot nematodes'. minyoo hii midogo hukaa chini ya udongo maeneo ya mizizi.

      Namna nzuri ya kudhibiti hali hii ni KUBADILISHA MAZAO na USAFI WA SHAMBA (Kufanya palizi kwa wakati). Kubadilisha mazao maana yake Usipande nyanya chungu kwa muda mrefu kwenye shamba moja, jitahidi kubadirisha kwa kupanda mazao mengine ili kuharibu mzunguko wa maisha (Life cycle) wa vimelea hivi na hawa minyoo.

      Kama nilivyoeleza kwenye makala hii hapo juu, nitaweka magonjwa ya zao hili hapo baadae.

      Karibu sana!

      حذف
  2. Hakuna namna nyingine ya kuzuia huu mnyauko mbali na kubadulisha zao maana shamba kwa mfano mimi nimekodi.

    ردحذف

إرسال تعليق

أحدث أقدم