Majina mengine ya ugonjwa huu ni
pamoja na AI, Flu, Influenza, Fowl plague. Ugonjwa huu husababishwa na virusi
na huathiri mfumo wa upumuaji wa kuku. Ugonjwa huu huwakumba kuku na jamii zote
za ndege.
Virusi wa Mafua ya ndege huishi
muda mrefu kwenye mazingira tofauti tofauti bila kupoteza uhai wake. Virusi
hawa wanaweza kuishi kwenye mazingira ya joto la kadiri au baridi kali, pia
wanaishi vizuri kwenye mazingira ya barafu iliyoganda. Hii hupelekea ugonjwa
huu kusambazwa kupitia kinyesi na mizoga ambayo haikuteketezwa vizuri.
Dalili za Ugonjwa
- Kuku wanakosa hamu ya kula.
- Kuku wanapata matatizo ya mfumo wa upumuaji kama kupiga chafya, kukohoa n.k
- Kuku wanaharisha sana
- Uzalishaji wa mayai hupungua kwa kasi sana
- Kuku wanavimba upanga wa juu na chini wa kichwa.
- Kuku wanakua na madoa mekundu au meupe kwenye miguu na upanga wa kichwani.
- Kunaweza kukawa na matone ya damu yayotoka puani
- Vifo huweza kuanzia asilimia chache hadi kukaribia asilimia 100%.
TAZAMA VIDEO HAPO CHINI KUONA DALILI ZA KUKU MGONJWA
Video credit: FieldVet Channel
Namna ugonjwa unavyosambazwa
- Ugonjwa huu husambazwa kupitia vifaa mbalimbali vilivyochafuliwa na majimaji au kinyesi cha kuku Mwenye ugonjwa kama viatu, nguo, trei za mayai, vifaa vya kulia na kunywea maji na vifaa vingine.
- Wadudu mbalimbali na panya wanaweza kusambaza ugonjwa huu kwa kubeba virusi kutoka weye mzoga wa kuku aliyekufa kwa ugonjwa huu.
Namna ya kudhibiti
- Ugonjwa huu hauna tiba, bali unachanjo. Pia dawa za Antibayotiki mbalimbali huweza kutumika kupunguza kasi ya ugonjwa kwa kuua bakteria wa magonjwa nyemerezi. Kuku wakipata nafuu kidogo huendelea kupunguza kasi ya virusi, lakini dawa hizi za Antibayotiki haziui virusi. Chanjo ya ugonjwa huu isitumike bila ruhusa maalum kutoka kwa wataalamu wa mifugo na serikali kwa ujumla.
- Udhibiti wa uingizwaji wa kuku na jamii nyingine za ndege ndani ya eneo husika hususani mipakani. Ugonjwa huu huathiri maeneo makubwa kama nchi nzima, mikoa au wilaya, hivyo taratibu za kuzuia uingizwaji au kutoa jamii ya ndege mbalimbali kwa eneo husika (Quarantine) hufanywa na taasisi mbalimbali za serikali hususani Wizara ya mifugo (kama Wizara ya mifugo na uvuvi nchini Tanzania)
- Teketeza kwa kuchoma moto mizoga ya kuku wote wenye ugonjwa huu (Hii ndio njia bora zaidi ya kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huu, ikifuatiwa na chanjo pamoja na kuzuia uingizwaji na utoaji wa jamii zote za ndege kwa eneo husika)
Muhimu*
Kama umegundua kwamba shamba lako
au banda lako la kuku lina ugonjwa huu, toa ripoti kwenye mamlaka husika hususani
Maafisa mifugo wa vijiji au Kata, kama maafisa hawapo kwenye maeneo yako toa
taarifa wilayani kwenye Idara ya mifugo.
10. INFECTIOUS CORYZA
Majina mengine ya ugonjwa huu ni
pamoja na Roup, cold, coryza. Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vya Bakteria
vinavyoitwa Haemophilus paragallinarum. Kuku ambao hawahudumiwi vizuri kiasi
kwamba wakawa wanaishi kwenye mazingira machafu yasiyofaa, wako hatarini sana
kukumbwa na ugonjwa huu.
Dalili za ugonjwa
- Kuku wanavimba usoni
- Wanapumua kwa shida
- Wanatoa harufu mbaya
- Wanatoa majimaji puani na machoni
- Macho yanatoa majimaji na kushikamana
- Wanaweza kuharisha
- Kuku wadogo wanadumaa
- Vifo vinanzia asilimia 20% hadi 50%
- Ugonjwa unaweza ukadumu siku chache au miezi michache inategemeana na kiwango cha magonjwa nyemelezi yaliyopo
TAZAMA VIDEO HAPO CHINI KUONA DALILI ZA KUKU MGONJWA
Video credit: FieldVet Channel
Namna ugonjwa unavyosambazwa
- Ugonjwa huu husambazwa kwa njia ya mgusano baina ya kuku na kuku. Pia kuku wanaweza kuambukizwa kupitia hewa, kwa kuvuta hewa yenye vimelea vya ugonjwa huu
- Vile vile kuku wanapata ugonjwa huu kwa kula vyakula na maji yaliyochafuliwa na uchafu wenye bakteria wa ugonjwa huu.
- Pia ugonjwa unaweza ukasambazwa endapo mizoga ya kuku wenye ugonjwa kuwekwa ndani ya banda la kuku. Pia kuku waliopona wanakua bado na vimelea hivi kwa maisha yao yote.
Namna ya kudhibiti
- Fuga kuku wako katika mazingira ya usafi, kwa sababu uchafu ndio chanzo cha mlipuko na kusambaa kwa vimelea hivi.
- Tumia dawa mbalimbli za antibayotiki kutibu ugonjwa huu, dawa hizi hufanya kazi vizuri kama utatibu mapema kuku wako, wakati maambukizi ndo yameanza. Dawa hizo ni zenye viua sumu vya erthyromycin, streptomycin na sulfonamides. Mfano wa dawa hizo kwa majina ya kibiashara ni kama Sulfadimethoxine (Albon®, Di-Methox™) hii dawa ndio inayopendekezwa sana. Kama dawa hii haipo au haifanyi kazi vizuri jaribu dawa hizi=> sulfamethazine (Sulfa-Max®, SulfaSure™), au erythromycin (gallimycin®), au tetracycline (Aureomycin®).
- Punguza msongamano wa kuku ndani ya banda, hii itasaidia kuruhusu hewa ya kutosha bandani.
- Kama kuna mlipuko mkubwa wa ugonjwa huu kwenye eneo lako, piga chanjo.
11. ASPERGILLOSIS
Majina mengine ya ugonjwa huu ni
pamoja na Brooder pneumonia, mycotic pneumonia, Aspergillus. Ugonjwa huu
husababishwa na fangasi. Kama chanzo cha vimelea ni viwanda vya kutotoreshea
vifaranga ugonjwa huu utaitwa brooder pneumonia. Ugonjwa huu ukiwapata kuku
wakubwa unaitwa Aspergillosis.
Dalili za Ugonjwa
- Ugonjwa huu huanza kuwa mkali sana kwa kuku wadogo na hukomaa sana kwa kuku wakubwa.
- Kuku wadogo hupumua kwa shida
- Wakati wa usiku au mchana kuku hawakoromi kama magonjwa mengine.
- Kuku wanakosa hamu ya kula
- kuku wanapalalaizi viungo na kulemaa kwa sababu ya sumu ya fangasi hao.
- Vifo vinaanzia asilimia 5% hadi 50%
- Kuku wakubwa wanapata matatizo ya kupumua na kukosa hamu ya kula.
- Kuku wanakua na rangi ya bluu na nyeusi kwenye ngozi (cyanosis)
- Kuku wanakua na matatizo ya neva za fahamu kama kupinda shingo.
- Vifo kwa kuku wakubwa huwa ni chini ya asilimia 5%.
TAZAMA VIDEO HAPO CHINI KUONA DALILI ZA KUKU MGONJWA
Video credit: FieldVet Channel
Namna ugonjwa unavyosambazwa
- Vimelea vya fangasi huzaliana kwa kasi kwenye joto la kawaida la bandani
- Vimelea hivi husambazwa kupitia masalia ya mimea yaliyowekwa juu ya sakafu la banda kama mapumba ya mpunga, malanda ya mbao na masalia mengine.
- Pia Kuku wanaambukizwa kupitia vyakula na maji yaliyochafuliwa na uchafu wenye vimelea hivi.
Namna ya kudhibiti
- Ugonjwa huu hauna tiba kwa kuku waliathirika
- Ugonjwa huu unazuiwa kwa kuhakikisha usafi wa banda kila wakati na kuruhusu hewa ya kutosha bandani.
- Ili kuondoa chanzo cha maambukizi, weka dawa za kuua hao fangasi kwenye chakula kama Mycostatin, Mold curb, Sodium, Calcium Propionate na Gentian violet), pia weka Copper sulfate au Acidified copper kwenye maji ya kunywa kwa siku tatu.
- Pulizia mapumba ya mpunga au malanda dawa ya kudhibiti vumbi na usambazaji wa vimelea vya fangasi, dawa hiyo inaitwa Germicide yenye mafuta (Oil-base germicide)
- Osha vifaa vya kulia na kunywea maji na kemikali zinazoua vimelea vya fangasi (Disinfectant).
12. GUMBORO (INFECTIOUS BURSAL
DISEASE)
Majina mengine ya Ugonjwa huu ni
kama IBD, Infectious bursitis na infectious avian nephrosis. Gumboro ni Ugonjwa
unaosababishwa na virusi, pia dalili za ugonjwa huu huonekana kwa kuku wenye
umri wa Zaidi ya wiki 3. Pia manyoya yanayozunguka sehemu ya hajakubwa huwa
yametapakaa kinyesi chenye muonekano wa chumvi chumvi.
Dalili za Ugonjwa
- Manyoya ya kuku huwa rafu
- Kuku wenye umri chini ya wiki tatu hawaonyeshi dalili zozote
- Kuku wanaishiwa nguvu halafu wanakaa mkao wa kubinua mgongo
- Kuku wanakosa hamu ya kula
- Wanatembea kwa shida
- Kuku wanaharisha muharo wa maji maji
- Wanakua ni kama wanajificha
Namna Ugonjwa unavyosambazwa
- Ugonjwa huu huenezwa kwa kugusana baina ya kuku na kuku, pia kupitia mgusano baina ya kuku na mtu au vifaa.
- Pia ugonjwa huu husambazwa kwa njia ya hewa kupitia vumbi iliyochafuliwa na majimaji ya kuku mgonjwa
- Mizoga ya kuku wenye virusi ndio chanzo kingine cha kusambaza ugonjwa huu, hakikisha unateketeza kuku wote waliokufa na ugonjwa huu.
TAZAMA VIDEO HAPO CHINI KUONA DALILI ZA KUKU MGONJWA
Video credit: FieldVet Channel
Video credit: Chicken Farm By Taimoor Channel
Namna ya kudhibiti
- Ugonjwa huu hauna tiba hivyo huzibitiwa kwa chanjo, ila unaweza ukatumia antibayotiki mbalimbali kupunguza makali ya ugonjwa huu au tumia dawa za salfa kama Sulfonamides, au tumia dawa zingine kama Nitrofurans n.k
- Teketeza kwa moto kuku wote waliokufa kwa ugonjwa huu.
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
إرسال تعليق