Kilimo bora cha Uyoga - Sehemu ya Kwanza (Growing Mushroom - Part One)


KILIMO CHA UYOGA SEHEMU YA KWANZA

Zao la uyoga (mushroom) hutumika maeneo mengi afrika mashariki na barani afrika kwa ujumla kama chakula. Upatikanaji wa zao hili ni wa kubahatisha kwani hujiotea wenyewe mashambani, wakulima wengi hawana utamaduni wa kupanda zao hili kama ilivyo kwa mazao mengine. Sababu za wakulima wengi kutokulima zao hili ni nyingi, sababu kubwa ni ukosefu wa elimu ya kilimo hiki. Kwenye makala hii utajifunza hatua kwa hatua namna ya kulima kilimo hiki, nifwate nikujuze, karibu sana!.

Zao hili lina faida nyingi kiafya ikiwa ni pamoja na kuupatia mwili virutubisho mbalimbali Kama; Wanga, Mafuta, Protini, Calcium, Phosphorus, Iron (Madini ya chuma), Potassium, Vitamini A, Vitamini B6, Vitamini B12, Thiamine, Riboflavin n.k. Zao hili ni muhimu sana kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari na magonjwa mengine mengi ikiwa ni pamoja na wale wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) husaidia kuongeza kinga zao za mwili.

Zao hili la uyoga huota Kwenye maozo ya mimea mbalimbali, maozo ya mimea hiyo huitwa 'Substrate' kwa lugha ya kitaalamu. Mimea iliyo mingi hutegemea mwanga wa jua ili kutengeneza chakula chake na kukua, lakini kwa uyoga ni tofauti sana, hautegemei mwanga wa jua ili kukua.

Uyoga ni fangasi wanaoota kwenye masalia ya mimea iliyooza inayoitwa “substrate” kwa lugha ya kimombo, uyoga huanza kama mbegu ndogo sana inayoitwa spores kwa lugha ya kimombo. Spores ni mbegu ndogo sana za mimea jamii ya fanji (fungi). Mbegu hizo ndogo za fungi (spores) huota kwenye masalia ya mimea hiyo iliyooza (substrate) na kutengeneza uyoga.

AINA
Kuna aina kuu mbili za uyoga ambazo huzalishwa na wakulima walio wengi, aina hizo ni kama ifuatavyo;

1. Bottom mushrooms (Agaricus spp.)
Aina hii hupandwa na wakulima wakubwa kwani huitaji tekinolojia kubwa kuzalishwa.

2Oyster mushrooms (Pleurotus spp.)
Aina hii hupandwa na wakulima wadogo kwani huitaji tekinolojia rahisi kuzalishwa, mkulima anatumia malighafi zinazopatikana kwenye mazingira yake.

MUHIMU
Kabla ya kuanza uzalishaji wa uyoga inampasa mkulima kuzingatia yafuatayo;

1) Uwepo wa soko la bidhaa hii
2) Upatikanaji wa mbegu bora za uyoga (Spawn)
3) Upatikanaji wa masalia ya mimea yatakayotumika kuzalisha uyoga (substrate)
4) Upatikanaji wa vionjo (supplements), vionjo hivi huongeza virutubisho kwenye masalia ya mimea (substrate)
5) Mpango kazi wa uzalishaji ili kuhakikisha uzalishaji endelevu.

MASOKO
Kama unataka kuzalisha uyoga kibiashara inakupasa kufahamu na kuzingatia yafuatayo;

1) Aina ya uyoga na kiasi kinachohitajika sokoni
2) Bei ya uyoga sokoni na upatikanaji wake
3) Wasambazaji wa uyoga waliopo na kama kuna uwezekano wa kutengeneza urafiki wa kibiashara.
4) Uwezekano wa kuongeza thamani ya bidhaa hiyo (uyoga)

Kabla ya kuanza uzalishaji, wakulima wadogo wanashauriwa kutafuta mahala watakapoweza kuuza uyoga watakaozalisha hususani kwa masoko yaliyopo karibu na maeneo yao.

MPANGO KAZI WA UZALISHAJI
Mkulima anatakiwa apange uzalishaji wake kiasi kwamba aweze kuzalisha kiasi ambacho anaweza kuuza, anaweza kugawanya uzalishaji wake kwa sehemu nne tofauti kulingana na hatua za ukuaji au muda wa kupanda. Hii ina maana kwamba usipande uyoga mwingi kwa wakati mmoja, bali panda kwa muachano wa muda fulani ili kuhakikisha upatikanaji wa uyoga kwa muda wote.

VITU MUHIMU VYA KUFAHAMU

1) Mbegu za uyoga (spawn)
Hizi ni mbegu za kuzalisha uyoga ambazo hutengenezwa maabara kutokana na uyoga wenyewe (mycelium), hutengenezwa kwenye mazingira ya usafi sana ili kuhakikisha ubora wake. Kiasi cha mbegu za uyoga zinazohitajika ni sawa na asilimia 4-6% ya uzito wa masalia ya mimea itayotumika kuzalisha uyoga (substrate). Kwa mfano kama uzito wa masalia ya mimea ni Kilo 60, kiasi cha mbegu za uyoga zinazohitajika ni kilo 2.4-3.6%.

2) Masalia ya mimea (Substrate)
Haya ni masalia ya mimea yanayotumika kuotesha uyoga, Masalia mazuri ni yale yenye virutubisho vingi, yenye uwezo wa kupitisha hewa na kutunza maji. Masalia ya mimea yanayotumika sana kuoteshea uyoga ni kama ifuatavyo;

- Masalia yanayotokana na mazao ya nafaka (Mtama, mahindi, mpunga na shayiri ‘barley’)
- Mabaki ya pamba
- Mabunzi ya mahindi
- Majani ya kahawa
- Vumbi la mbao
- Sukari guru
-Water hyacinth, matumizi ya water hyacinth kuoteshea uyoga yalifanyika na kutangazwa kwa mara ya kwanza na chuo kikuu cha Hong Kong nchini China na baadae kufanywa barani Afrika na Chuo kikuu cha Mutare nchini Zimbabwe. Water hyacinth ni aina ya magugu maji yanayoziba maeneo yanayopita maji barani Afrika, uzuri magugu haya gharama za kuyaandaa ili kuoteshea uyoga huwa ni ndogo.

NB:
Masalia ya mimea jamii ya nafaka (cereal straws) hutumika mara nyingi na ni mazuri hususani masalia ya zao la mtama kwa sababu ya virutubisho vingi ambavyo huitajika na Uyoga na huarakisha uotaji na ukuaji.

>>> SEHEMU YA PILI

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم