SEHEMU YA PILI
KUANDAA SHAMBA
Baada ya kuandaa kitalu chako ni wakati muafaka wa kuandaa shamba, maandalizi ya shamba yanatofautiana yamegawanywa katika makundi mawili; mpunga unaomwagiliwa na mpunga unaotegemea mvua.
1) Mpunga unaomwagiliwa (Under irrigation)
Maandalizi ya shamba huanza kwa kufurisha maji shambani kina cha sm 10 na baadae shamba hilo lilimwe kwa trekta lenye nguvu kuanzia Horsepower 40 hadi 75. Shamba lililoandaliwa vizuri huharakisha ukuaji wa mmea na huleta mavuno mazuri tofauti na shamba lilioandaliwa vibaya.
Baada ya kuandaa shamba andaa majaruba ili kuweka ardhi iliyo tambalale, kisha chabanga udongo vizuri ili kulainisha udongo na mara moja furisha maji kwenye majaruba hayo na yaache yakae siku 15 kabla ya kupandikiza. Utaratibu huu huleta faida zifuatazo;
a) Kuepusha miche kuathiriwa na mlundikano wa sumu zitokanazo na maozo ya matamahuluku (organic matter) ndani ya maji yariyofurika (flooded).
b) Kuepusha upotevu wa kirutubisho cha Naitrojeni kinachotengenezwa na maozo za matamahuluku (organic matter) ndani ya maji (denitrification).
2) Mpunga unaotegemea mvua (Under rainfed situation)
Inatakiwa shamba lilimwe mara mbili na kufanyiwa halo mara moja, baada ya hapo tengeneza majaruba ili kuweka ardhi iliyotambalale itakayoruhusu maji yaliyofurishwa na mvua kukaa vizuri, pia mimea itakayopandikizwa kukua vizuri.
KUPANDIKIZA MICHE
Kabla ya kupandikiza miche furisha maji kitalu chako kina cha sm 10 siku moja kabla ya kupandikiza, hii itasaidia kuosha udongo ulioshikilia mizizi ya miche na pia kusaidia kung’oa miche kwa urahisi.
Miche huwa tayari kupandikizwa baada ya wiki 3 hadi 4 tangu kupanda itategemeana na aina ya mbegu, mwanga wa jua na joto.
Miche hupandikizwa kwa nafasi ya sm 20 x sm 10 au sm 20 x sm 20, miche ipandwe kina cha sm 3, ikipandikizwa zaidi ya kina cha sm 3 huchelewesha na kupunguza mche kutoa machipukizi (tillering), hali hii husababisha kuwa na uotaji usiofanana na kuiva kusikofanana pia husababisha upotevu wa mavuno. Hakikisha miche inapandikizwa ikiwa imenyooka vyema ili kurahisisha kutoa mizizi na machipukizi (tillering).
Miche inapandikizwa kwa mkono au kwa kutumia mashine, itategemeana na ukubwa wa shamba lako pia na mtaji wako. Kutumia mashine ni bora zaidi kwani hupunguza gharama ya vibarua na kuokoa muda.
Picha: Kupandikiza miche
Picha: Kuchambua na kupandikiza miche
"rice transplanting" flickr photo by dreamingyakker shared under a Creative Commons (BY-NC-ND) license
Picha: Kupandikiza miche
KUPANDA MBEGU MOJA KWA MOJA SHAMBANI
Utafiti unaonyesha kwamba upandaji wa moja kwa moja huwa na mavuno yaliyosawa na ule wa kupandikiza, utaratibu huu huokoa gharama za vibarua ingawaje una hasara zake ikiwa ni pamoja na ukuaji usiofanana, na uwepo wa magugu mengi shambani.
Ufuatao ni utaratibu wa kupanda moja kwa moja shambani hususani kwa mpunga unaolimwa kwa kutegemea mvua;
Panda mpunga wako mwanzoni mwa mvua zinavyoanza kunyesha hususani kabla ya mvua nyingi za masika. Wakulima wanashauliwa kutumia mbegu bora zilizothibitishwa kitaalamu ili kupata mavuno bora. Wakati wa kupanda tengeneza vimfereji vidogo vilivyoachana kwa upana was m 25 kwa mbegu fupi na sm 35 kwa mbegu ndefu, kisha panda mbegu zako. Kwa kupanda hivi, kiasi cha mbegu kinachohitajika kwa hekta 1 ni Kilo 50 (Kilo 20 kwa ekari moja). Kama utapanda kwa staili ya kurusha mbegu (broadcasting), kiasi cha kilo 75 kwa hekta kitatumika. (Kilo 30 kwa ekari moja)
Kuhudumia maji
Baada ya kupanda ni wakati wa kuweka maji shambani kwa matumizi ya mpunga wenyewe pia kusaidia kuondosha magugu, kwa muktadha huo ni muhimu kuweka kiwango sahihi cha maji yanayotakiwa wakati wote wa ukuaji wa mmea. Kama ni msimu wa masika dhibiti kiwango cha maji kwa kuruhusu maji kutoka au kuingia kwenye majaruba.
Upotevu wa maji shambani hudhibitiwa kwa njia zifuatazo;
1) Kukarabati matuta ya majaruba yaliyobomoka
2) Kuondoa magugu shambani kwani husababisha kupunguza maji yatakayotumiwa na mpunga
3) Kuongeza kimo cha matuta ya majaruba ili kuzuia maji yaliyojaa shambani yasipite juu ya majaruba.
Hatua za ukuaji wa mmea ambazo maji huitajika kwa kiwango kikubwa, ni kama ifuatavyo;
1) Kipindi cha siku 3 hadi 7 baada ya kupandikiza
Wakati huu hakikisha unaweka maji shambani kiasi cha asilimia 80% ya kimo cha miche ya mpunga. Hii itasaidia kupunguza upotevu wa maji kupitia mche wa mpunga (majani au mashina), hii itasaidia mmea kutengeneza mizizi mipya na pia kusaidia mizizi hiyo kuchukua maji ya kutosha kwenye udongo.
2) Kipindi cha kufunga na kuchanua mpunga (Booting and heading stage)
Kipindi hiki ndio wakati wa uzalishaji, mashina ya mpunga hutoa mbegu. Kipindi hiki maji yanahitajika sana kwa ajili ya kutengeneza mbegu, maji yakipungua mpunga hutengeneza mapepe (mbegu za mpunga zisizokua na kitu).
KUTUNZA SHAMBA
Kama ilivyo kwa mazao mengine zao la mpunga nalo huhitaji matunzo mazuri ili kupata mavuno mengi, ikiwa pamoja na matumizi ya mbolea, usafi wa shamba, kudhibiti wadudu waharibifu na magonjwa n.k.
Kwa upande wa matumizi ya mbolea, mbolea za asili nazo hufaa sana kama samadi, mboji, minjingu rock phosphate n.k. Pia mbolea za viwandani huweza pia kutumika kuongeza uzalishaji, kiasi cha Kilo 80 za Nitrojeni zinahitajika kwa Hekta moja (80KgN/ha, sawa na Kilo 174 za mbolea ya UREA. Kwa mifuko ya urea yenye ujazo wa Kg 50 tutakua na mifuko 3 na nusu. Pia Kirutubisho cha phosphorus nacho huitajika sana kwa uzalishaji wa zao hili, kiasi cha Kilo 58 za phosphorus huitajika kwa hekta moja (58KgP2O5/ha) sawa na Kilo 126 za Mbolea ya DAP. Kwa mifuko ya mbolea ya DAP yenye ukubwa wa Kg 50 tutakua na mifuko 2 na nusu.
Viwango hivi vya mbolea ni makadilio tu, lakini kupata kiwango sahihi cha virutubisho kinachohitajika kwenye shamba lako, unapaswa upime udongo ili kubaini mapungufu ya virutubisho. Kama unahitaji kupima udongo wa shamba lako waone wataalamu wa kilimo waliopo kwenye maeneo yako.
Kulima zao la mpunga pekee kwa muda mrefu husababisha upungufu mkubwa wa rutuba ya udongo kutokana na kutegemea sana mbolea za viwandani na kuharibika kwa asili ya udongo pamoja na kupotea kwa viumbe wadogo kwenye udongo wanaoozesha masalia ya mimea na wanyama (microbial organism).
Kudhibiti hali hiyo ya upungufu wa rutuba, inakupasa ubadirishe mazao kwa kupanda mazao jamii ya mikunde kama maharage ya soya au maharage ya kawaida kipindi cha kiangazi au baada ya kuvuna mpunga wako. Pia unaweza ukabadirisha na mazao kama ndizi au miwa.
Pia inashauriwa kwamba ni muhimu kuacha masalia ya mpunga shambani baada ya kuvuna yaoze pamoja na kuweka mbolea za samadi ili kuboresha afya ya udongo, yaani kuongeza uwezo wa udongo kufanya kazi. Pia kama una mbolea ya Minjingu (Rock phosphate) unaweza ukaimwaga na kuivuruga shambani, pia hii itasaidia kuboresha afya ya udongo na kuongeza uzalishaji.
SEHEMU YA TATU >>>
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
إرسال تعليق