Kilimo cha Bamia - Sehemu ya Pili (Growing Okra - Part Two)


SEHEMU YA PILI

Kudhibiti Wadudu waharibifu
Wafuatao ni wadudu waharibifu wanaoharibu zao la bamia, nimeeleza mambo mengi yanayomuhusu mdudu husika pamoja namna ya kumdhibiti.

1. Cutworms (Agrotis spp)
Hawa ni viwavi wenye rangi ya kijivu, wanakata mashina ya miche michanga usawa wa ardhi, wanafanya uharibifu huu wakati wa usiku na wakati wa mchana hujificha ndani ya udongo.

Picha: Kipepeo wa Cutworms, Photo Credit: www.extension.umn.edu

Picha: Cutworms jamii ya Kiwavi jeshi, Photo Credit: Joseph Berger, www.canolawatch.org

Picha: Cutworms wa kawaida, Photo Credit: John Obermeyer, Purdue University; www.almanac.com

Namna ya kuwadhibiti
  • Andaa au lima shamba lako vizuri ili kuwaacha viwavi hawa peupe au juu ya ardhi, ili waweze kuliwa na wadudu au wanyama wengine pia wakiwa juu ya ardhi wanakufa kwa jua. Kama shamba lako litapandwa muda mfupi baada ya kulimwa, kuna hatari ya hawa viwavi kuvamia miche ya bamia.
  • Hakikisha usafi wa shamba kila wakati kwani magugu yakiwa mengi yanavutia uwepo wa viwavi hawa.
2. Cotton Seed bugs (Oxucarenus spp)
Wadudu hawa ni wadogo wana urefu wa mm 4 hadi 6 na wana rangi nyeusi. Mabawa yao yanang'aa mfano wa kioo. Wadudu hawa wanakula matunda madogo yanayokua. Hatua ya ukuaji ya buu na mdudu kamili hufyonza maji maji na chakula kwenye mbegu za matunda machanga na kuzuia matunda kushindwa kukomaa. Mara nyingi wadudu hawa huonekana wakati wa kutoa maua, kuchanua maua na wakati wa kutengeneza matunda. Wadudu hawa hawaathiri sana uzalishaji wa bamia, kama ni wachache sana unaweza kuwaacha tu bila kuwadhibiti.

Picha: Cotton Seed bugs, Photo Credit: James D. Young, www.blogs.ifas.ufl.edu

Picha: Cotton Seeds bugs, Photo Credit: www.infonet-biovision.org

Namna ya kuwadhibiti
  • Hakuna haja ya kuwadhibiti kwani wana athari ndogo sana.
  • Unaweza kuwaondoa tu kwa kutingisha mmea ili kuwadondosha.
3. African bollworm (Helicoverpa armigera)
Viwavi hawa wanakula majani, maua na matunda. Athari kubwa sana huonekana kwenye maua na matunda ya bamia. Viwavi hawa huvamia maua na kusababisha maua kudondoka (Flowers abortion). Pia viwavi hawa hutoboa matundu ya mviringo kwenye matunda na kusabisha tunda la bamia kuoza kutokana na magonjwa nyemelezi.

Picha: African Bollworm, Photo Credit: www.infonet-biovision.org

Picha: African bollworm, Photo Credit: www.infonet-biovision.org

Namna ya kuwadhibiti
  • Piga dawa mbalimbali za kuua viwavi hawa zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.
  • Njia ya kibaolojia kwa kutumia viumbe wengine wanaokula viwavi kama Sisimizi, siafu na wengine.
  • Tembelea shamba lako mara kwa mara ili kubaini wadudu hawa, kadri unavyowadhibiti wakiwa wachache ndivyo jinsi wanavyopoteza uwezo wao wa kusambaa.
4. Spiny bollworm or Spotted bollworm (Earias spp)
Kiwavi huyu ndiye anaeathiri sana uzalishaji wa bamia, Akiwa mkubwa ana urefu wa mm 13 hadi 18 na upana wa mm 2.5. Wanakua na rangi tofauti kuanzia rangi ya kijivu iliyochangamana na rangi ya kaki, pia wanakua na rangi kijivu kwenda kijani iliyochangamana na mistari ya mpauko au myeupe. Mdudu kamili (Kipepeo) anakua na urefu wa mm 12 na upana wa majani wa mm 20 hadi 22. Mabawa yake ya mbele yanakua na rangi nyeupe, au kijani ya mng'ao au njano inategemeana na aina ya kipepeo.

Viwavi hawa wanatoboa matawi ya bamia changa na kusababisha maotea ya matawi kufa. Matunda ya bamia yakianza kuzalishwa viwavi hawa huvamia maua na matunda madogo ya bamia na baadae huvamia matunda makubwa. Maua na matunda yaliyoharibiwa hupukutika, hali inayopelekea kushuka kwa uzalishaji. Uwekaji wa kiasi kikubwa sana cha mbolea zenye Naitrojeni (N) huongeza athari za kiwavi huyu.

Picha: Kipepeo wa Spiny bollworm

Picha: Spiny bollworm akiwa kwenye tunda la bamia, Photo Credit: Nigel Cattlin; www.visualsunlimited.photoshelter.com

Namna ya kuwadhibiti
  • Tembelea shamba lako mara kwa mara ili kubaini athari za viwavi hawa.
  • Tumia dawa mbalimbali za kemikali zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.
  • Weka mbolea za viwandani kwa kiwango kinachofaa; epuka kuweka kiwango kikubwa sana cha mbolea zenye Nitrojeni.
  • Usiwaangamize wadudu wanaokula viwavi hawa kama sisimizi, siafu, beetle na wengine kwani wanadhibiti kasi ya viwavi hawa.
  • Tumia dawa za asili kama Mwarobaini, au dawa zingine za viwandani zilizotengenezwa kwa Mwarobaini (Biopesticides-Neem based pesticides)
  • Teketeza masalia ya mimea ya bamia baada ya kuvuna.
  • Pia unaweza ukawaua kwa kutumia mkono kama shamba lako ni dogo.
5. Spider Mites (Tetranychus spp)
Wadudu hawa wanafanana na buibui, tofauti yao ni kwamba wadudu hawa ni wadogo sana na wana rangi nyekundu au njano iliyokolea. Buibui hawa wadogo huvamia majani na kutandaza utando na kuanza kuzaliana, wakiwa kwenye majani hufyonza majimaji na chakula kwenye mmea.

Majani yaliyoathiriwa yanaonyesha rangi nyeupe hadi njano, athari ikizidi sana majani yanabadilika rangi na kuwa mekundu sana. Rangi hii nyekundu ni muonekano wa buibui hawa wakiwa wengi. Athari ikiwa kubwa majani yanajikunja baadae hukauka na hatimae hudondoka, hali itakayopelekea mmea kupukutisha najani. Athari ikizidi sana buibui hawa wekundu huvamia matunda. Hali inayovutia kuutokea na kuzaliana kwa hawa wadudu ni Joto na hali ya ukame au kiangazi, kuondoshwa kwa wadudu wanaokula buibui hawa (Natural enemies) na kuwepo kwa mimea mingine iliyohalibiwa sana na wadudu wengine au magonjwa kama Pamba, Nyanya n.k, hali hii pia huvutia uwepo na kuzaliana kwa buibui hawa.

Picha: Red spider mites wakishambulia mmea, Photo Credit: www.researchgate.net

Picha: Muonekano wa Red spider mites kwa kutumia hadubini (Microscope); Photo credit: www.thebeatsheet.com.au

Namna ya kuwadhibiti
  • Tembelea shamba lako mara kwa mara ili kubaini kiwango wa wadudu hawa, hii itakusaidia kujua wakati gani muafaka wa kuanza kupiga dawa.
  • Hakikisha shamba lako linakua safi wakati wote kwa kuondoa magugu na kuchoma moto mabaki ya mimea yenye magonjwa na wadudu mara tu baada ya kuvuna.
  • Usipande mimea mipya ya bamia karibu na shamba liloathiriwa na wadudu hawa, kama utapanda hakikisha unateketeza masalia yote ya mimea iliyoathiriwa.
  • Tumia dawa mbalimbali za kemikali zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.
6. Thrips (Frankliniella spp)
Wadudu hawa au Vithripsi wanakula sehemu ya chini ya Jani, Maua na Matunda. Hatua mbili za ukuaji wa mdudu huyu yaani Kiwavi na Mdudu kamili huathiri mmea wa bamia. Wanachofanya wanafyonza majimaji ya mmea yenye chakula, hatimae huathiri ukuaji na uzalishaji wa mmea.

Majani yaliyoathiriwa na wadudu hawa hujikunja na kukakamaa, baadae hukauka. Mazingira yoyote yatakayodhoofisha afya ya mmea husababisha wadudu hawa kuzaliana kwa kasi na kuongeza mashambulizi kwenye mmea.

Wadudu hawa wakivamia miche michanga ya bamia husababisha mimea kudumaa. Wakivamia maua husababisha matunda kupinda au kuwa na sura mbaya. Pia wakivamia matunda ya bamia hutengeneza makovu kwenye matunda ambayo huaribu ubora na soko la bamia hiyo.

Picha: Muonekano wa Vithripsi kwa kutumia Hadubini (Microscope), Photo Credit: Lance Osborne; www.entnemdept.ufl.edu

Photo Credit: www.infonet-biovision.org

Picha: Mabaka au makovu yaliyosababishwa na Thrips; Photo Credit: www.researchgate.net

Picha: Mabaka au makovu yaliyosababishwa na Thrips; Photo Credit: www.researchgate.net

Namna ya Kuwadhibiti
  • Andaa shamba lako kwa kulima na kusawazisha vizuri mabonge ya udongo, hii itasaidia kuwaacha peupe Pupa wa Thrips (Hii ni hatua ya tatu ya ukuaji wa mdudu), Pupa hawa watakufa kwa kupigwa na jua au kwa kuliwa na wadudu wengine.
  • Kama watakua wengi, piga dawa za kibaolojia (Biopesticides), Dawa hizi hutengenezwa kwa bakteria maalum ambao husababisha ugonjwa kwa hawa thrips hatimae thrips hufa. Mfano wa dawa hii ni SPINOSAD, Sharti la dawa hii ni kwamba unatakiwa upulizie mapema wakati maua yameanza kutoka. Ukipulizia baadae sana au wakati matunda yameanza kutoka, husababisha kuwepo kwa masalia ya sumu kwenye matunda.
  • Tumia dawa nyingine za kemikali zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.
<<< SEHEMU YA KWANZA
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم