Kilimo bora cha Karanga - Sehemu ya Pili (Growing Groundnuts - Part Two)


SEHEMU YA PILI

KUWEKA MBOLEA
Zao la karanga huhitaji mbolea kama yalivyo mazao mengine, Kama nilivyoeleza hapo awali kwamba kurejesha masalia ya mimea kwenye udongo baada ya kuvuna ni jambo muhimu sana kwani  husaidia kuboresha rutuba ya udongo.

Matumizi ya mbolea za asili kama Samadi na Mboji & matumizi ya mbolea za viwandani ni muhimu sana ili kupata mavuno mengi. Kirutubisho muhimu kwa zao la karanga ni Kalsiamu (Calcium) hususani kipindi cha kutoa karanga, kama ardhi ina unyevu wa kutosha kirutubisho hiki hufyonzwa moja kwa moja kwenye karanga zenyewe. Upungufu wa kirutubisho hiki kwenye udongo husababisha karanga kutokokua na matunda ndani (Empty pods). Kirutubisho cha Calcium (Ca) kinaongezwa kwenye udongo kwa kuongeza pH ya udongo, au kupunguza kiwango cha Asidi (acid) kwenye udongo kwa kuongeza Chokaa kwenye udongo kama udongo wako una Asidi nyingi. Pia namna nyingine ya kuongeza pH kwenye udongo ni kuhakisha ardhi yako unaweka mbolea za asili kama Samadi, mboji, pia kurudishia masalia ya mmea baada ya kuvuna kwenye udongo.  pH ikiongezeka kuna kuwa na kiwango kikubwa cha kirutubisho cha Calcium kwenye udongo.

NB:
Pengine msomaji utakua ukijiuliza kwamba neno pH maana yake nini? Neno pH ni kiwango cha Tindikali kwenye udongo aidha Asidi (Acid) au bezi (Alkaline). Kwa hiyo pH ikiongezeka ardhi inakua na Bezi (Alkaline), pH ikipungua ardhi inakua na Asidi (Acid).

Zao la karanga ni jamii ya mikunde (Legumes) haliitaji kirutubisho cha Nitrogen, hukidhi mahitaji hayo kwa kujitengenezea kirutubisho hicho yenyewe kwa kufyonza hewa ya Naitrojeni hewani na kutengeneza kirutubisho hicho kwenye udongo (Nitrogen fixation). Kirutubisho cha 'Nitrogen' kikizidi husababisha karanga kuwa na majani mengi kuliko karanga.

NB:
Mbolea zenye kirutubisho cha 'Nitrogen' ni pamoja na UREA, DAP, CAN, SA, NPS, NPS-Zn, N.P.K, Mbolea za kwenye majani kama BOOSTER n.k.

Karanga huhitaji Kirutubisho cha 'Nitrogen' katika kipindi cha awali cha ukuaji, Sharti ni kwamba mbolea hizo ziwekwe kwenye udongo kabla ya kupanda. Unaweza ukaweka mbolea kama DAP, TSP au SA, Mbolea ya SA (Sulphate of Ammonia) ni nzuri zaidi kwa sababu ina ziada ya kirutubisho cha Sulphur ambacho ni muhimu sana kwa zao la karanga.

NB:
Jambo lingine la muhimu ni kwamba, karanga zikishaota haziitaji tena kuweka mbolea za chumvi chumvi au mbolea za kwenye majani (Boosters) kwa sababu zitakua na majani mengi na uzalishaji utakua mdogo. Kwa hiyo mbolea ziwekwe kwenye udongo kabla ya kupanda kama nilivyoeleza hapo juu.

KUDHIBITI MAGUGU
Ili kupata mavuno mengi ya karanga, hakikisha unadhibiti magugu ipasavyo, Zao la karanga lina uwezo mdogo sana wa kushindana na magugu hususani kwa kipindi cha awali cha ukuaji. Ondoa magugu mapema kabla zao lako halijaanza kutoa karanga, wakati huo huo uwe unajaziliza udongo kwenye mashina (Earthing up) ili kusaidia karanga kujishikilia vizuri kwenye udongo na kutoa mavuno mengi. Karanga zikianza kushikilia kwenye udongo hususani kuanzia wiki ya sita tangu kupanda, fanya palizi kwa mkono usitumie jembe kwa sababu utaharibu karanga ndogo zinazoanza kukua au kuharibu maua. Hii ina maana kwamba fanya palizi kwa kutumia vijembe hadi kufikia wiki 6 tangu kupanda, baada ya hapo tumia mkono.

KIDHIBITI WADUDU WAHARIBIFU NA MAGONJWA

A: WADUDU WAHARIBIFU

1. White grubs (Schyzonycha spp.)
Hawa ni viwavi wa wadudu wanaoitwa Scarab "Chafer" beetles, wana rangi nyeupe na wana umbo linalofanana na herufi "C" pia wana vichwa vyenye rangi ya kahawia na miguu sita (Pea tatu za miguu).

Photo Credit: www.infonet-biovision.org

Athari:
  • Viwavi hawa huathiri hatua zote za ukuaji wa mmea, wanakula mizizi na matunda ya karanga. Kwa upande wa mizizi viwavi hawa hula mzizi mkuu (taproots) pamoja na mizizi ya pembeni (Peripheral roots) hali inayopelekea mmea kudumaa au kufa.
  • Pia majeraha yanayosababishwa na viwavi hawa kwenye mizizi husababisha maambikizi ya vimelea vya magonjwa ya ukungu (Fangasi au Kuvu) kwenye mizizi na mmea wote kwa ujumla.
  • Viwavi hawa hukata na kutoboa matunda machanga ya karanga.
Namna ya kudhibiti
  • Hakikisha udongo wa shamba lako umechanganyika vizuri na maozea au samadi kabla ya kupanda. Mbolea ya samadi au mboji ikizidi shambani huongeza athari ya viwavi hawa hususani mbolea hiyo ya samadi ikiwekwa wakati wa kupanda.
  • Lima shamba lako vizuri kwa kina cha kutosha ili kuanika peupe mayai au wadudu mbalimbali juu ya udongo hatimae mayai hayo kuharibiwa na jua na wadudu hao kuliwa na wadudu wengine (Predators). Hali itasaidia kupunguza idadi yao na uharibifu kwenye mmea wa karanga.
2. Mchwa (Termites)
Mchwa ni mdudu anaesababisha uharibifu mkubwa kwenye zao la karanga na mazao mengine kwa maeneo mengi barani Afrika. Aina za mchwa hawa ziko mbili; Mchwa wakubwa (Odontotermes or Macrotermes) na Mchwa wadogo (Microtermes).


Athari:
  • Mchwa wakubwa husababisha uharibifu kidogo, lakini mchwa wadogo ndio wabaya zaidi husababisha uharibifu mkubwa zaidi kwa sababu huenea kila mahali kwenye matunda ya karanga pamoja na mizizi. Hali hii husababisha mmea kunyauka na kufa.
  • Pia mizizi iliyoliwa na wadudu wengine kama viwavi (White grubs), inakua hatarini kuvamiwa na mchwa. Baadhi ya aina za mchwa kama Macrotermes spp na Hodotermes mossambicus (Mchwa wakubwa) hukata mashina ya karanga usawa wa ardhi na huweza kusababisha upotevu wa mavuno kuanzia asilimia 25% hadi 100%.
  • Uharibifu wa mchwa huongezeka sana kipindi cha mwisho cha kukomaa karanga, kuelekea kuvuna, na mara nyingi uharibifu huongezeka sana kipindi cha ukame.
Namna ya Kudhibiti
  • Ondoa masalia ya mazao jamii ya nafaka kama mahindi, ulezi na mtama. Kwani masalia hayo ni chakula kizuri cha mchwa, yakiwepo shambani husababisha mchwa kuvamia karanga. Kama utapenda kuyaacha masalia hayo shambani, basi hakikisha yameoza vizuri ndipo upande karanga.
  • Panda karanga zako mapema mwanzoni mwa msimu wa mvua ili kuepuka kipindi cha ukame. Kukiwa na ukame mchwa uharibu sana. Karanga hukomaa kuanzia miezi mitatu hadi minne inategemeana na aina ya mbegu, mara nyingi kwa maeneo ya nyanda za juu kusini nchini Tanzania karanga hupandwa mwezi wa 12 au wa 1.
  • Vuna karanga zako mapema mara tu zinapokomaa, utafiti unaonyesha kwamba athari ya mchwa huongezeka kadiri unavyochelewa kuvuna.
NB:
Maeneo mengi ya uzalisaji wa karanga barani Afrika yanakumbwa na ukame na joto jingi, hali hii hongeza kasi ya uharibifu wa mchwa shambani na ongezeko la fangasi wenye sumu kwenye matunda/mbegu za karanga wanaoitwa 'Aspergillus flavus' (A. flavus). Fangasi hawa hutengeneza sumu kwenye mbegu za karanga inayoitwa 'Aflatoxin'

Kwa aina ya mchwa wanaotengeneza vichuguu (mounds), hudhibitiwa kikamilifu kwa kubomoa au kuondosha kichuguu chote pamoja na malkia wao (Queen Termites). Usipobomoa kichuguu vizuri husababisha mchwa kuzaliana tena kwani malkia wa nyuki waliobaki huanzisha kizazi kingine.

Picha: Malkia wa nyuki            Photo Credit: www.pacificcoasttermite.com

Picha: Malkia wa nyuki         Photo Credit: www.phys.org

<<< SEHEMU YA KWANZA


Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم