Kilimo bora cha Maembe - Sehemu ya Tatu (Growing Mango - Part Three)


SEHEMU YA TATU

5. Mango seed weevil (Sternochetus mangiferae)
Wadudu hawa hula majani, matawi machanga au machipukizi ya maua. Mdudu huyu jike hutaga mayai juu ya tunda changa na kuacha alama ndogo nyeusi juu ya ngozi ya tunda. Baade mayai hayo huanguliwa na kutoa viwavi ambao hutoboa ngozi ya tunda na kuingia ndani ya tunda, pia hufika mapaka kwenye mbegu ya tunda na kuua kabisa mbegu hiyo. Viwavi hao hustawi na kukua ndani ya mbegu ya tunda. Viwavi hao wakishakua hubadilika kuwa pupa na baadae mdudu kamili (beetle), baadae mdudu huyu hutoboa tundu kutokea ndani kuelekea nje ya tunda na kutoka. Baadae tundu hilo hukakamaa na kukauka, hali hii husababisha tunda kukosa ubora na kushindwa kuuzika.

Picha: Mango Seed weevil 
USDA APHIS PPQ , USDA APHIS PPQ, Bugwood.org

Picha: Tunda la embe lilioathiriwa na kiwavi wa 'mango seed weevil'
Lesley Ingram, Bugwood.org

Namna ya kudhibiti
  • Hakikisha shamba lako ni safi wakati wote, kusanya na ondoa matunda yaliyodondoka, pamoja na matawi yaliyodondoka na baadae yachome moto.
  • Fanya uchunguzi kwenye shamba lako kubaini matunda yenye alama nyeusi juu ya ngozi, baadae yakusanye na kuyachoma moto kwa wakati huo utakua umeangamiza viwavi, pupa na mdudu kamili (beetle)
6. Mealybugs (Rastrococcus spp.)
Hawa ni wadudu wadogo, wenye umbile bapa na mwili laini uliogawanyika, mwili wao umefunikwa na manyoya laini meupe kama ungaunga. Hufyonza majimaji ya chakula kwenye majani machanga, vikonyo na matunda. Majani yaliyoathiriwa sana na wadudu hawa hubadirika rangi kuwa njano na baadae kukauka. Hali hii husababisha mmea kupukutisha majani, maua na matunda machanga. Wadudu hawa hutoa utomvu kama asali ambao baadae huvunda na kutengeneza fangasi, utomvu huo baadae hufunika na majani, matawi na matunda na kuyafanya kuwa na rangi nyeusi. Hali hii hupunguza uwezo wa mmea kujitengenezea chakula chake wenyewe (Photosynthesis), hali ikizidi husababisha majani kupukutika na matunda kukosa ubora wa soko.

Picha: Mealybugs

Picha: Mealybugs

Namna ya kudhibiti
Matumizi ya viuatilifu havisaidii kudhibiti wadudu hawa hii ni kutokana na jinsi wadudu hawa wanavyotengeneza utomvu kwenye majani, matawi na matunda. Tumia njia zifuatazo kudhibiti wadudu hawa.
  • Ondoa matawi na majani yaliyoathiriwa na wadudu hawa, hususani matawi machanga kabla maua kuanza.
  • Dhibiti sisimizi wakubwa kwa wadogo (ants) kwa kutumia viutilifu vinavyoua sisimizi tu (non-broadspectrum insectcides) kwani sisimizi hawa ndio huwalinda wadudu hawa kwa sababu wanakula utomvu unaotengenezwa na wadudu hao. Sisimizi wakishaangamizwa itakuawa rahisi kwa wadudu rafiki kuwala wadudu hao (mealybugs).
  • Pulizia dawa za asili kama mwarobaini, sabuni (potassium soap) [asilimia 1 hadi 2%] na Mineral oil, waliotumia dawa hizi wamekili kupata matokeo mazuri kuwadhibiti wadudu hawa.
  • Watunze wadudu rafiki wanaokula wadudu hawa kama ladybird beetles, hover flies, lacewings na parasitic wasps kwa kuacha kupulizia viuatilifu vinavyoua wadudu wa aina zote (broad-spectrum), dawa hizi huangamiza wadudu rafiki.
7. Scales
Hawa ni wadudu wadogo wenye urefu wa mm 1 hadi mm 7, kiujumla hawatembei (immobile insects), wana rangi na shepu tofauti tofauti inategemeana na aina ya mdudu huyo. Mdudu huyu jike hana miguu wala mabawa, hufanana na gamba dogo lililobandikwa na gundi kwenye mmea. Wadudu hawa majike hutaga mayai chini yake, yakishaanguliwa magamba madogo (tiny scales) hutoka na kutembea kutafuta chakula, wakifika sehemu ya mmea waliyoridhika nayo hutulia hapo hapo na hawatembei tena. Wakiwa hapo hufyonza majimaji ya chakula juu ya mmea kama majani, matawi n.k.

Kuna aina mbili za wadudu hawa kwenye zao la maembe; wenye gamba laini (soft scales) na wenye gamba gumu (armoured scales). Wenye gamba laini (soft scales) hutoa utomvu kama asali, mfano wa wadudu hawa ni pamoja na wenye rangi ya kijani (soft green scales), Coccus viridis; wenye rangi ya kahawia (brown soft scales), Coccus hesperidum na wenye utomvu (wax scales), Ceroplastes spp. Wenye gamba gumu (armoured scale) ni pamoja na wenye rangi nyeupe (white scale), Aulacaspis tubercularis; mwili wake una rangi nyekundu inayochangamana na kahawia. Majike yamefunikwa na gamba jeupe la mviringo na madume yamefunikwa na gamba dogo la pembe nne.

Wadudu hawa wakianza kufyonza majimaji kwenye mmea husababisha majani kuwa ya njano na kudondoka, ukuaji duni (kudumaa), kufa kwa matawi, kudondoka kwa matunda na kusababisha mipasuko kwenye matunda. Mti ulioathiriwa sana na wadudu hawa huweza kufa, vilevile utomvu kama asali unaotolewa wadudu hawa wenye gamba laini (soft scales) husababisha uvundo kwenye majani, matawi na matunda. Hali hii husababisha maeneo hayo ya mmea kubadirika rangi na kuwa meusi, rangi hii nyeusi hupunguza uwezo wa mmea kujitengenezea chakula chake wenyewe (Photosynthetic Capacity). Matunda yaliyofunikwa na uvundo wa utomvu wa wadudu hawa hupoteza hadhi ya soko. Sisimizi wakubwa kwa wadogo (Ants) hupendelea kula utomvu uliotengenezwa na wadudu hawa, hali hii husaidia kupunguza ongezeko la utomvu huu, lakini sisimizi hawa huwalinda wadudu hawa dhidi ya wadudu wengine (natural enemies). Wadudu wenye gamba gumu (Armoured scales) hawatoi utomvu unaofanana na asali (honeydew).

Picha: Scales
Gerald J. Lenhard, Louisiana State University, Bugwood.org

Namna ya kudhibiti
Watunze wadudu rafiki wanaokula wadudu hawa kama parasitic wasps, ladybird beetles, lacewings n.k., kwa kutopulizia viuatilifu vinavyoua wadudu wa aina zote (broad-spectrum insectcides) pia kwa kupulizia baadhi ya mistari kwa zamu kila msimu. Hii itasaidia kuhifadhi wadudu rafiki kwa ile miti isiyopuliziwa dawa kwa msimu huo. Wadudu hawa rafiki huwadhibiti wadudu hawa kikamilifu. Kwa hatua za awali za ugojwa huu ondoa na choma moto matawi na majani yote yaliyoathirika

8. Bugs
Kuna aina nyingi za bugs ambao huathiri matunda, wote wakubwa kwa wadogo (nymphs) hula maeneo ya mti wa mwembe kwa kufyonza majimaji ya chakula kwa kutumia mdomo wake mwembamba kama mrija. Athari hiyo husababisha majani kufa na kunyauka mwishoni, matunda yaliyoathirika hudondoka na kuwa na shepu mbaya. Zifuatazo ni baadhi ya aina za wadudu hawa (Bugs);

8.1. Coconut bug (Pseudotheraptus wayi)
Wadudu hawa wana rangi nyekundu iliyochangamana na kahawia, wana urefu wa sm 1.5. Hutaga mayai juu ya matunda, matawi machanga, maua na vikonyo vya maua. Wadudu hawa wachanga huwa na rangi ya kahawia iliyopauka pamoja na antena ndefu.

Wadudu hawa hufyonza matunda, matunda machanga yaliyoathiriwa huonyesha rangi ya kahawia iliyochangamana na weusi au kijivu na mara yingi matunda haya hudondoka. Matunda makubwa yaliyoathirika huwa na makovu yenye majimaji.

Picha: Coconut bugs,    Photo Creditwww.inaturalist.org

8.2. Tip wilters (Anoplocnemis curvipes)
Hawa ni wadudu wakubwa wenye urefu wa sm 2.5 na rangi ya kahawia iliyochangamana na weusi. Miguu ya nyuma ya mdudu dume huwa mikubwa, wadudu wakubwa kwa wadogo hula majani machanga na vikonyo vya maua hali inayosababisha machipukizi ya majani au maua kunyauka na kufa.

Picha: Tip wilters,   Photo Credit: www.diark.org

8.3. Helopeltis bugs (Helopeltis schoutedeni and H. anacardii)
Hawa ni aina ya bugs ambao hufanana na mbu na huitwa mosquito bugs, ni wembamba wenye urefu wa mm 7 - 10 wana miguu mirefu na antena ndefu. Urefu wa antena hizo ni mara mbili ya urefu wa mwili wake. Mdudu jike ana rangi nyekundu na dume ana rangi ya njano iliyochangamana na wekundu. Hutaga mayai maeneo machanga na malaini ya mmea kama sehemu za juu za maua au matawi machanga. Wadudu hawa wakubwa kwa wadogo hula matawi machanga na matunda, hali hii husababisha matunda kuwa na madoa meusi yenye rangi ya kahawia katikati na matawi hufa.

Majani yaliyoathirika huaribika na kuwa na shepu mbaya pia huwa na michirizi, baadae majani hayo hudondoka kiasi kwamba yanaonekana kama yamevamiwa na wadudu wanaotoboa majani. Wakila mashina ya matawi husababisha michirizi mirefu yenye rangi ya kijani, maranyingine huambatana na utomvu.

Picha: Helopeltis bugsPhoto Credit: www.infonet-biovision.org

Mti ulioathirika sana na wadudu hawa hufa kwa sababu ya mate yao pamoja na uwepo wa fangasi ambao huingia kwenye mmea kupitia maeneo yam mea yaliyoliwa. Athari ikizidi sana mti huonekana kana kwamba umeiunguzwa na moto, mti mdogo ulioathirika huwa na madoa yaliyobonyea. Wadudu hawa husababisha mti kudumaa na utengenezwaji wa matunda kupungua, kudhibiti wadudu hawa ni kazi sana kwa sababu wanakula mazao yaliyomengi na wanatembea sana kutoka eneo moja hadi jingine. Kupunguza athari ya wadudu hawa fanya yafuatayo;

Namna ya kudhibiti bugs
  • Wakusanye kwa mkono na kuwaua hususani kwa miti yenye umri mdogo wakati kutoa machipukizi na wakati wa ukuaji wa matunda.
  • Watunze wadudu rafiki wanaokula wadudu hawa kama; assassin bugs, spiders, praying mantises na sisimizi wakubwa kwa wadogo. Sisimizi hawa ni tofauti na wale wanaoishi juu ya miti (weaver ants) ambao huwalinda wadudu hawa.
  • Fukiza moshi
  • Usipande miembe na mazao mengine yanayopendwa na bugs aina ya helopeltis (Helopeltis bugs) kama Pamba, Chai, viazi, mipera, korosho n.k. 
9. Mango leaf coating mite (Cisaberoptus kenyae)
Hawa ni wadudu wadogo wenye urefu wa mm 0.2, wana rangi mpauko na muonekano kama msokoto wa sigara au tumbaku. Huwezi kuwaona kwa macho ya kawaida maana ni wadogo sana, huishi kwa makundi chini ya utando mweupe juu ya majani. Utando huo mweupe huweza kuondolewa kirahisi kwa mkono, majani yaliyofunikwa na utando huu hubadirika rangi na kuwa njano na hudondoka yakiwa bado machanga. Kwa ujumla utando huu una athari ndogo sana kwa mavuno.

Picha: Mango leaf coating mite,  Photo Credit: www.infonet-biovision.org

Namna ya kudhibiti
Ondoa na teketeza majani yote yenye utando mweupe. Mara nyingi hakuna udhibiti mwingine unaohitajika zaidi ya huu.

<<< SEHEMU YA PILI
SEHEMU YA NNE >>>

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

1 تعليقات

  1. Hello mambo vipi, naitwa Nase ni web designer, naomba maongezi na wew
    nase9935@gmail.com
    0676219401

    ردحذف

إرسال تعليق

أحدث أقدم