SEHEMU YA PILI
KUTUNZA SHAMBA
Vilevile miembe huhitaji kupunguziwa matawi ili kutengeneza muonekano mzuri wa mti, pia mara nyingine moshi huweza kutumika kudhibiti wadudu waharibifu na kushinikiza mmea kutoa maua vizuri. Kupunguzia matawi katika mwaka wa kwanza hutengeneza shepu ya mti huo. Katika mwaka wa kwanza punguzia mti wako katika kimo cha m 1 ili kutengeneza mtawanyiko mzuri wa matawi. Katika mwaka wa pili punguza matawi na kuacha matawi 4 hadi 5 yaliyoachana kwa nafasi nzuri, matawi haya yaliyobaki ndio yatakua matawi makuu ya baadae. Kuna faida nyingi za kupunguzia matawi kama ifuatavyo;
1)Mti huzalisha matunda makubwa
2)Matawi ya mti huwa na nafasi kurahisisha uvunaji
3)Matunda hukomaa vyema yakiwa mtini
4)Unaweza ukapanda mazao chini ya mti
5)Mti hupata faida ya mwanga wa jua na upepo, hii itasaidia kupunguza unyevu kwenye matawi na majani na kuepusha mazingira ya uwepo wa magonjwa.
6)Hudhibiti kimo cha mti na kuzuia mtawanyiko uliozidi wa matawi.
Vilevile baada ya kuvuna ni vyema kupunguzia matawi, matawi yanatakiwa yawe juu kimo cha kuanzia mita 1 kutoka ardhini. Ondoa matawi yaliyokufa na maotea kwenye tawi kuu, punguzia matawi hayo kiasi kwamba miale ya mwanga wa jua iweze kupenyeza na kufika chini ya mti.
Pia unaweza kuongeza uzalishaji wa matunda yako kwa kufanya yafuatayo;
1)Hakikisha shamba lako ni safi wakati wote
2)Ondoa matunda yaliyoiva na magugu kuzunguka mti
3)Miembe huaribiwa sana na upepo mkali, hivyo inatakiwa kupanda miti kukinga upepo kuzunguka shamba lako
PALIZI
Hakikisha unaondoa majani kuzunguka mti mara kwa mara na kuyatumia kama matandazo pale pale kwenye mti, hii itasaidia kuongeza unyevu na joto, pia kuzuia magugu yasiote.
KUFUKIZA MOSHI
Kufukiza moshi kwenye miti ya miembe ni muhimu sana kwa sababu njia hii husaidia kupunguza idadi ya wadudu waharibifu na kuboresha utengenezwaji wa matunda. Utaratibu huu hufanyika kwa kutumia kifaa maalumu au kopo lenye matundu chini ya kuingizia hewa, ndani yake huwa na vumbi la mbao, juu ya vumbi la mbao kunawekwa majani yanayotoa harufu mbaya (aromatic herbs) kama Michaichai (Lemongrass) n.k. Kopo hili huning’inizwa katikati ya mti wa mwembe ambapo moshi unaotoka husambaa sehemu yote ya mti na kuwafukuza wadudu.
Photo Credit: www.infonet-biovision.org, Shared under a Creative Commons License
Njia nyingine ya kufukiza moshi ni kwa kuchoma majani chini ya mti, cha msingi chunguza uelekeo wa upepo ili wakati wa kuchoma moshi uelekee kwenye mti. Kabla ya kuchoma majani chini ya mti, ongezea juu majani mabichi yanayotoa harufu mbaya kama michaichai, Lantana n.k, baada ya hapo choma majani yote na moto ili kutengeneza moshi. Yafahamu majani yenye harufu mbaya kama inavyoonekana kwenye picha hapa chini.
A: LANTANA
Picha: Lantana
Picha: Lantana
B: MCHAICHAI (LEMONGRASS)
Faida nyingine ya kufukiza moshi ni pamoja na kuharakisha mti wa mwembe kutoa maua.
WADUDU WAHARIBIFU NA MAGONJWA
A: WADUDU WAHARIBIFU
Wadudu waharibifu wanaoathiri sana zao hili ni pamoja na; Fruit flies, cotton scales, mealybugs, cicadas na black flies (hutengeneza utomvi kama asali). Wadudu hawa huleta uharibifu mkubwa sana, uzuri ni kwamba kuna wadudu rafiki wanaokula wadudu kama ladybird larvae, wasps, spiders na parasitic fungi (pamoja cicadas na black flies). Kwa ujumla udhibiti wa wadudu hawa hutegemea uwepo wa wadudu rafiki, wadudu hao rafiki (predators) huvutiwa na uwepo wa mazao tofauti ndani ya shamba la miembe, kadiri mazao tofauti yanavyopandwa ndio wadudu rafiki wanavyozidi kuongezeka shambani, pia pamoja na kutumia viuatilifu visivyoangamiza wadudu rafiki (non-broad spectrum insecticides).Yafuatayo ni maelezo ya kina kuhusiana na wadudu hawa;
1. Mango fruit flies (Ceratitis spp./ Bactrocera invadens)
Wadudu hawa hutaga mayai ndani ya ngozi ya tunda lililokomaa na tunda lililoiva, kwa aina nyingine ya wadudu hawa kama Bactrocera invadens hutaga mayai ndani ya ngozi ya tunda changa. Mayai hayo huanguliwa baada ya siku 1 hadi 2 tangu mayai kutagwa na kutoa viwavi weupe, viwavi hawa huanza kula tunda kwa ndani na kusababisha tunda kuoza. Baada ya siku 4 hadi 14, viwavi hawa huondoka ndani ya tunda kwa kupitia matundu waliyotoboa kwenye ngozi ya tunda. Baada ya hapo viwavi hao hubadilika na kuwa ‘buu’ na baadae mdudu kamili. Mdudu kamili huwa na ulefu wa mm 4 hadi 7.
Picha: Fruit fly (Ceratitis capitata)
Scott Bauer, USDA Agricultural Research Service, Bugwood.org
Picha: Fruit fly (Bactrocera invadens)
Florida Division of Plant Industry , Florida Department of Agriculture and Consumer Services, Bugwood.org
licensed under a Creative Commons Attribution 3.0 License.
Namna ya Kudhibiti
- Kusanya na teketeza matunda yote yaliyooza na kudondoka angalau mara mbili kwa wiki wakati wote wa msimu wa matunda. Wakati wa kuteketeza matunda hayo usiyatupe kwenye shamba lingine, badala yake yachome moto au yafukie kwenye shimo lenye kina la sm 50 kiasi kwamba mdudu kamili atakayezaliwa ashindwe kufika juu ya usawa wa ardhi.
- Chuma na yaondoe matunda yote yaliyoiva sana, kwa sababu huvutia wadudu hawa.
- Pia unaweza ukawanasa wadudu hawa kwa mitego maalumu (Fruit traps). Mitego hii hutengenezwa kwa kutumia chupa ya plastiki yenye matundu manne kuzunguka chupa upande wa juu, pia kunakua na mfuniko pamoja na waya wa kutundikia juu ya mti. Kopo hilo huwekwa chambo yenye mchanganyiko wa “Siki (vinegar) pamoja na sabuni au kipande cha ndizi”. Baada ya hapo tundika kopo hilo juu ya mti katikati ya matawi kimo cha mita 2 hadi 4 kutoka usawa wa ardhi. Kopo hili linatakiwa litundikwe eneo ambalo matawi na majani yapo karibu na yasiguse kopo. Mitego hii itundikwe kwa muachano was m 10 hadi 50 kutoka mtego mmoja hadi mwingine itategemeana na aina ya chambo. Kila wiki kusanya na uwaondoe wadudu ndani ya kopo na hakikisha chombo kinabakia safi.
2. Mango gall flies (Erosomyia mangifera)
Wadudu hawa wanafanana na mbu, wana urefu wa mm 1 hadi 2 wana miguu mirefu na antenna. Mdudu huyu hutaga mayai juu ya majani machanga, mayai hayo huanguliwa na kutoa viwavi ambao hushambulia majani. Mashambulizi hayo husababisha maumbile kama vipele au vichunusi kwenye majani (galls), kiwavi aliyekomaa huacha vipele hivyo na kudondoka kwenye udongo ili kuwa buu (pupae). Viwavi hawa pia huacha matundu madogo kwenye majani, matundu haya huwa sehemu ya kuingilia vimelea wa fangasi. Vipele vilivyopo kwenye majani husababisha tishu zilizozunguka vipele kufa, hali ikizidi husababisha majani kudondoka.
Picha: Vipele vya kwenye majani
Namna ya kudhibiti
- Watunze wadudu rafiki wanaokula vipele hivyo kama Parasitic wasps, kwa hiyo hakuna udhibiti mwingine unaohitajika.
- Maeneo mengine ambayo uharibifu wa wadudu hawa umezidi sana, eneo la udongo kuzunguka mti hufurishwa maji kabla ya mmea kutoa maua, hii husaidia kupunguza mdudu kamili kutoka kwenye udongo.
3. White flies and black flies (Aleurocanthus woglumi)
Wadudu hawa wana ukubwa wa mm 1 hadi 3 pia wana jora mbili za mabawa ambazo zimefunika mwili mzima, wadudu hawa hufanana na vipepeo wadogo. Wadudu hawa hufyonza majimaji ya chakula kutoka kwenye majani, wakiwa wengi husababisha mmea kudhoofika. Wakati wanafyonza majimaji hayo hutoa utomvu kama asali (honewdew), utomvu huo husababisha uvundo (mould) kwenye majani. Idadi ya wadudu hawa ikiongezeka husababisha majani kufunikwa utomvu mweusi kwenye majani, hali inayofanya mti mzima kuonekana mweusi. Hali hii husababisha mti kupunguza uwezo wake wa kujitengenezea chakula chake (Photosynthesis), pia baadae husababisha majani kudondoka.
A: MANGO WHITE FLIES
Picha: Whiteflies
B: BLACK WHITEFLIES
Picha: Black flies
Florida Division of Plant Industry , Florida Department of Agriculture and Consumer Services, Bugwood.org
licensed under a Creative Commons Attribution 3.0 License.
Picha: Black fly
Florida Division of Plant Industry , Florida Department of Agriculture and Consumer Services, Bugwood.org
Namna ya kudhibiti
- Watunze wadudu rafiki wanaokula wadudu hawa kama ladybird beetle, parasitic wasps n.k, kwa kutotumia viuatilifu, au kama utatumia basi tumia viuatilifu visivyoua wadudu wa aina zote (non-broad spectrum) insecticides.
- Tumia dawa za asili kama mwarobaini, tengeneza juisi ya mwarobaini kwa kutumia majani, matawi au magome ya mti wa mwarobaini alafu pulizia mti wako kwa kutumia pampu. Dawa hii husaidia kuzuia hatua za awali za ukuaji wa wadudu hawa, hupunguza idadi ya mayai na kufukuza wadudu kamili (Adults).
4. Mango aphid (Toxoptera odinae)
Wadudu hawa ni wadogo wenye urefu wa mm 1.1 hadi 2.5, wana rangi ya kahawia, nyeusi au nyekundu iliyochangamana na kahawia. Wadudu hawa huishi kwa makundi chini ya majani machanga, hufyonza maji maji ya chakula kwenye majani machanga, matawi machanga, vikonyo na kwenye matunda. Wakiwa wanafyonza husababisha majani na matawi kujikunja. Pia wadudu hawa hutengeneza utomvu kama asali (honeydew) kwenye majani, matawi na matawi, utomvu huo huleta uvundo kwenye majani, matawi na matunda. Hali hii husababisha mmea kupunguza uwezo wa kujitengenezea chakula kwasababu utomvu huo hufunika majani pia husabaisha matunda kupunguza ubora wake wa soko kwani utomvu huo pamoja na uvundo hufunika matunda.
Namna ya kudhibiti
- Watunze wadudu rafiki wanaokula wadudu hawa kama ladybird beetle, parasitic wasps n.k wadudu rafiki wanavutiwa kwa kupanda mazao ya aina tofauti ndani ya shamba la miembe kama mahindi, maharage n.k, hali hii itasababisha wadudu rafiki kuongezeka na kuwadhibiti wadudu waharibifu
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
إرسال تعليق