Kilimo Bora cha Soya - Sehemu ya Kwanza (Growing Soyabean - Part One)


SEHEMU YA KWANZA

Soya, Maharage ya Soya (Glycine max) ni miongoni mwa mazao jamii ya mikunde kama maharage, kunde, mbaazi n.k. Zao hili ni muhimu sana kwa afya kutokana na kiwango kikubwa cha protini kilichonacho, kiwango chake cha protini ni kuanzia asilimia 35% hadi 40% na mafuta 15% hadi 22% vilevile zao hili lina virutubisho muhimu kama amino acids, vitamini mbalimbali na madini. Zao hili lina matumizi mbali mbali ikiwa ni pamoja na kutumika katika maandalizi ya vyakula mbalimbali vilivyo kawaida (fresh), vilivyochachushwa (fermented) na vikavu (dried) kama maziwa, maziwa ya soya, maharage n.k. Pia zao hili hutumika kama tiba ya maradhi mbalimbali pamoja na kuboresha utendaji kazi wa viungo muhimu vya mwili kama moyo, maini, figo, tumbo pamoja na utumbo. Zao hili pia hutumika kutengenezea mafuta ya kula na mafuta kwa matumizi ya viwandani. Vilevile hutumika kama kiambata muhimu sana wakati wa kutengeneza vyakula vya mifugo. 

MAZINGIRA
Zao hili hufanya vyema kwenye muinuko kuanzia m 0 hadi m 2000 kutoka usawa wa bahali, Zaidi ya mita 2000 muda wa kukomaa huongezeka na kufikia siku 180 (miezi 6). Kiwango cha joto kinachohitajika kwa zao hili ni kuanzia nyuzi joto 21°C hadi 32°C, nyuzi joto zaidi ya 32°C hupunguza utoaji wa maua na utengezwaji wa matunda (Soya). Kama kuna upatikanaji wa maji ya kutosha shambani kwako, zao hili huzalishwa muda wote kwa mwaka hususani kwa maeneo ya kitropiki. 

Kiasi cha mvua kinachohitajika na kuleta tija ni kuanzia mm 400 hadi 500 kwa mwaka. Maji huitajika sana kipindi cha kuota, kipindi cha kutoa maua na kipindi cha kutengeneza matunda (pod formation), ingawaje kiasi kidogo cha maji huitajika wakati wa kukomaa na kuiva matunda. 

Zao hili hupendelea udongo tifutifu usiotwamisha maji, kiwango cha tindikali ya udongo kinachohitajika ni kuanzia pH 6.0 hadi 6.5, pH ya udongo ikiwa ndogo (acidity) zao hili halifanyi vizuri. Kwa udongo wenye tindikali (acidity) tumia chokaa kudhibiti hali hiyo, ili kuongeza uzalishaji. 

AINA 
Kuna aina mbalimbali za mbegu za Soya, nchini Tanzania mbegu za Soya huzalishwa na taasisi za utafiti wa kilimo (TARI), mojawapo ya taasisi hizo ni pamoja na TARI Uyole iliyopo Mkoa wa Mbeya nchini Tanzania, mbegu bora ya soya inayozalishwa na taasisi hii ni pamoja na "Soya Uyole 1". Mbegu hii hupendelea maeneo yenye muinuko kuanzia m 1000 hadi 1800 kutoka usawa wa bahari, huvumilia sana meneo yanayotwamisha maji. 

KUPANDA 
Kama ilivyo kwa mazao mengine jamii ya mikunde zao hili hupandwa kwa mbegu, ingawaje mbegu za soya hupoteza uwezo wa kuota kuanzia miezi 6 hadi 10 tangu kuvunwa, itategemeana na aina ya mbegu na mazingira hususani maeneo yenye joto kali na vumbi. Kwa hiyo kabla ya kupanda inampasa mkulima afanye majaribio ili kubaini kama mbegu zina uwezo wa kuota au lah. Namna ya kujaribu uotaji wa mbegu hizo ni kama ifuatavyo; 
  • Chukua mbegu 100 kutoka sehemu 3 tofauti za kifurushi, chombo, au kiroba cha mbegu. 
  • Weka mbegu hizo kwenye glasi yamaji kwa masaa 24, halafu yatoe maji hayo kisha weka pamba au kitambaa chenye unyevu ndani ya glasi na mbegu zikae juu yake, hakikisha kitambaa hicho au pamba ina unyevu wakati wote.
  • Baada ya siku 3 hadi 4 mbegu huanza kuota, kwa hiyo zihesabu mbegu zilizoota kati ya zile 100 Kisha tafuta asilimia ya mbegu zilizoota, Asilimia kuanzia 85% na kuendelea huashiria mbegu zako ni nzuri kwa kupanda, chini ya asilimia 85% mbegu zako hazifai kupandwa. 
Zao la Soya hupandwa bila kulimwa kwenye majaruba ya mpunga baada tu ya kuvuna kwa nafasi ya sm 25 x sm 25 au sm 20 x sm 20. Kwa mashamba yaliyolimwa zao hili hupandwa kwa nafasi ya sm 40 - 45 mstari hadi mstari na sm 10 shina hadi shina. kiasi cha mbegu zinazohitajika ni Kilo 60 hadi 70 kwa hekta moja (sawa na kilo 24 hadi 28 kwa ekari moja). 

KILIMO MSETO 
Zao la soya huweza kupandwa pamoja na mazao mengine kama mahindi, mihogo, mtama, ndizi, miwa, mpira, michikichi, nazi na miti ya matunda. Kwa mashamba ya mahindi na mtama zao hili hupandwa mistari miwili katikati ya mistari mahindi au mtama. zao hili likipandwa pamoja na mahindi huwavutia wadudu rafiki kama 'Parasitic wasps' ambao huwadhibiti viwavi wa mahindi, African bollworm (Helicoverpa armigera), vilevile zao hili hufunika magugu na kuyafanya yasiote au kuyadumaza (weed cover). 

Zao hili halitakiwi kupandwa eneo moja zaidi ya miaka miwili, hii itasaidia kuzuia magonjwa kujijenga kwenye udongo (soil-borne diseases). Badirisha mazao kwa miaka 3 hadi 4 ili kudhibiti magonjwa. Soya hufanya vizuri kwenye shamba lilopandwa mahindi kabla, lakini haitakiwi kupanda shamba lililopandwa mazao jamii ya mikunde kama maharage, kunde n.k. 

KUTUNZA SHAMBA 
Kama ilivyo kwa mazao mengine zao hili pia linahitaji matunzo, ikiwa ni pamoja na uwepo wa maji, kuondoa magugu, matumizi ya mbolea, udhibiti wa wadudu waharibifu na magonjwa n.k. Udhibiti wa magugu shambani huanza mapema wakati wa kuaandaa shamba, shamba likiandaliwa vizuri basi magugu yatakua kidogo shambani na udhibiti wake utakua si wakutumia nguvu nyingi. Maji yanahitajika sana hususani kipindi cha maua na kipindi cha mmea kutoa matunda. kama udongo wako una kichanga badi inakupasa kumwagilia maji mara kwa mara, tofauti na udongo tifutifu au mfinyanzi ambao haupotezi maji kwa haraka. 

Soya ni miongoni mwa mazao jamii ya mikunde yenye uwezo wa kutengeneza kirutubisho cha naitrojeni (N) kwa kutumia bakteria maalumu waliopo kwenye mizizi yao (Nitrogen fixing bacteria), kwenye mizizi ya mmea utatambua uwepo wa bakteria hawa kwa kuona vinundu vinundu vidogo (nodules), bakteria hawa hutumia naitrojeni inayofyonzwa na mmea kutoka hewani na kutengeneza aina naitrojeni (N) inayoweza kuchukuliwa kirahisi kwenye udongo (Available Nitrogen) kwa kutumia mchakato unaoitwa "Nitrogen Fixation" 

Kama unataka kupanda soya kwenye shamba ambalo halikupandwa soya kabla, ni vyema ukazitibu mbegu zako na bakteria hao wanaotengeneza kirutubisho cha nitrogeni kwenye udongo wanaoitwa "Soyabean inoculum" (Rhizobium japonicum). Bakteria hawa wanazalishwa katika taasisi za utafiti wa kilimo Tanzania (TARI), miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na TARI Uyole iliyopo mkoani Mbeya nchini Tanzania. Kiasi cha gramu 100 za bakteria huitajika kwa kilo 15 za mbegu, mbegu zilizotibiwa na bakteria hawa husaidia mmea kuwa na uwezo wa kutengeneza kirutubisho cha naitrojeni kwa kiwango kikubwa sana wakati wote wa msimu. Kama utakosa bakteria hawa hakuna shida, panda hivyo hivyo. 

Picha: Shamba la Soya lililotunzwa vizuri

Mmea wenye bakteria wa kiwango cha kutosha huwa na vinundu 5 hadi 7 kwenye mzizi mkuu, kama mmea una vinundu vichache (fewer nodules) chunguza mimea yako kubaini ongezeko la vinundu hivi. Upungufu wa kirutubisho cha naitrojeni husababisha mmea kupungua umbijani (Chlorophyll), majani hubadirika rangi na kuwa kijani mpauko kama yanataka kuwa njano. Mmea wenye afya nzuri yaani wenye vinundu vya kutosha vyenye bakteria hauna haja ya kuongezewa mbolea zenye naitrojeni (N), kwani utakua unapoteza muda na hela yako kwa sababu mbolea unayoweka itasababisha vinundu (nodules) kujitengeneza vibaya tofauti na kiwango cha mbolea ulichoweka. 

Kwa muktadha huo mbolea zinazofaa kwa zao la Soya ni zile zenye Fosforasi (P), kwani mbolea hizi husaidia kuboresha mizizi. Mfano wa mbolea hizo ni pamoja na DAP, TSP, Rock Phosphate (Minjingu) n.k. Kiasi cha mbolea hizi kwa eneo lako, itategemeana na hali ya udongo wako. Kwa hiyo waone wataalamu wa kilimo waliopo Kwenye eneo lako ili waweze kupima udongo wako pia watakueleza kiasi cha mbolea kinachohitajika na jinsi gani utunze iafya ya udongo wako. Ingawaje kwa makadirio, kiasi cha kilo 100 - 150 za mbolea hizo huweza kutosha kwa hekta moja (ekari mbili na nusu) na kusaidia sana kuboresha mizizi.


Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم