SEHEMU YA PILI
WADUDU WAHARIBIFU NA MAGONJWA
A: WADUDU WAHARIBIFU
1. Root-knot nematodes (Meloidogyne spp.)
Hawa ni minyoo wadogo wanaoathriri mizizi ya mmea, kwenye makala zangu nyingi za nyuma nimekwishaeleza kwa kina kuhusiana na wadudu hawa. wadudu hawa husababisha mizizi ya mmea kuvimba na kuwa na vivimbe au vinundu. Athari yake husababisha mmea kudumaa na majani yake kuwa ya njano, hali ikizidi mmea hunyauka na kufa.
© Howard F. Schwartz, Colorado State University, Bugwood.org
Picha: Root-Knot nematodes
Namna ya kudhibiti
- Panda aina ya Soya inayovumilia athari za wadudu hawa.
- Badilisha mazao kwa miaka 3 hadi 4 kwa kupanda mazao ya nafaka kama mahindi, mtama n.k.
- Tumia dawa za asili zitokanazo na mti wa mwarobaini (neem extracts).
2. Bugs
Hawa ni wadudu wakuu kwa zao hili, hula matunda na maeneo laini ya mmea wa soya. Wakati wanakula hupenyeza sumu ambazo husabisha tishu za matunda au za mbegu kufa. Mfano mzuri wa wadudu hawa ni pamoja na Green stink bug (Nezara viridula), Legume stink bug (Piezodorus hybneri), Riptortus bugs (Riptortus dentipes), Giant coreid bugs (Anoplocnemis curvipes), na Spiny brown bugs (Clavigralla spp.).
Athari ya wadudu hawa ikizidi husababisha mmea kusimamisha utengenezwaji wa matunda ya maharage ya soya na hatimae mbegu za soya kuharibika. Hali hii ikiendelea husababisha mmea kubakia na majani pekee bila matunda (Pods), majani yakiwa mengi bila matunda uzalishaji hupungua.
Bugs aina ya Green stink bug (Nezara viridula) vilevile hupenyeza vimelea wa fungus aina ya Nematospora coryli kwenye mbegu za soya zinazoendelea kukua na hii ndio hupelekea ugonjwa wa madoa madoa (Yeast spot disease).
Vile vile mmea wa soya ukivamiwa na aina ya bugs wanaotoa harufu mbaya (stink bugs) husababisha mbegu za mmea husika kupunguza uwezo wa kuota. Pia wadudu hawa wakivamia matunda ya soya, husababisha uzalishaji kupungua.
© Johnny N. Dell, Bugwood.org
Picha: Green Stink bugs (Nezara Viridula)
© Merle Shepard, Gerald R.Carner, and P.A.C Ooi, Bugwood.org
Picha: Legume stink bug (Piezodorus hybneri)
© brisbaneinsects.com
Picha: Riptortus bugs (Riptortus dentipes)
Bugs hawa ni vigumu sana kuwadhibiti, kwani wanatembea sana na wanaweza wakavamia mazao yaliyopo jirani. Ili kupunguza athari tumia njia zifuatazo;
Namna ya Kudhibiti
- Watunze wadudu rafiki kama Parasitic Wasps na assassin bugs, tazama picha hapo chini kuwafahamu
- Tumia dawa za asili kama zile zitokanazo na mti wa mwarobaini (Neem-based pesticides).
- Utafiti unaonyesha kwamba kupanda mmea aina ya Sesbania Rostrata husaidia kuwavutia bugs upande wake na kufanya waondoke kwenye mmea wa soya. Mmea huu ni mrefu kuliko soya na huchukua muda mrefu kukomaa, hali hii huwavutia bugs kwa muda mrefu. vilevile mmea huu siyo chakula kizuri kwa bugs wadogo (nymp) hivyo husaidia kupunguza idadi yao. Mmea huu hupandwa pande mbili tofauti za shamba la soya.
- Utafiti unaonyesha kwamba kupulizia soya na juisi ya majani au matawi ya mimea yenye harufu mbaya kama Gums, Lantana, Khaki weed n. k. husaidia kuwafukuza bugs.
NB:
Ni muhimu kufahamu kwamba kipindi cha awali cha mmea kuanza kutengeneza watoto/matunda ni wakati ambao bugs wakivamia husuani Stink bugs (Nezara Viridula) husababisha maharage ya soya kupoteza ubora na mavuno kupungua. Kwa hiyo udhibiti wa wadudu hawa ufanyike kabla ya hatua ya kutengeneza watoto kufika. Mara baada ya watoto kujaa mbegu na kukomaa, mmea wa soya hauwezi kuathirika na wadudu hawa pia hakuna haja ya kufanya udhibiti wowote.
3. Inzi wa Maharage [Beanflies] (Ophiomyia centrosematis and O. phaseoli)
Hawa ni wadudu wenye urefu wa mm 2 wana rangi nyeusi iliyochangamana na bluu yenye kung'aa. Wadudu hawa hufyonza uteute kwenye majani machanga na kusababisha madoa ya njano kwenye majani, hii ni ishara muhimu sana ya mapema kuhusiana na uwepo wa wadudu hawa shambani. Wadudu hawa jike hutaga mayai kwenye majani machanga, baada ya muda mayai hayo huanguliwa na kuwa viwavi.
Viwavi hao huondoka kwenye majani na kupenyeza wakiwa wanakula ndani ya shina hadi chini ya shina usawa wa ardhi ambapo hukamilisha hatua za ukuaji na kuwa mdudu kamili. Ulaji wa viwavi hawa husababisha shina kuvimba na kupasuka hali inayopelekea kupunguza utengenezwaji wa mizizi.
Mimea michanga iliyoathirika na wadudu hawa hunyauka na kufa, Mimea iliyokomaa huweza kuvumia athari za wadudu hawa lakini hubadilika rangi na kuwa njano, pia hudumaa na uzalishaji hupungua.
Athari huwa kubwa sana kwa mmea uliopandwa kwenye mazingira yenye ukame na udongo usiokuwa na rutuba. Mmea uliopandwa kwenye mazingira mazuri angalau huweza kupunguza athari ya wadudu hawa na pia uzalishaji hauwezi kupungua.
© Merle Shepard, Gerald R.Carner, and P.A.C Ooi, Bugwood.org
Picha: Beanfly
© Merle Shepard, Gerald R.Carner, and P.A.C Ooi, Bugwood.org
Picha: Mmea ulioathiriwa na inzi wa maharage (Beanfly)
Namna ya kudhibiti
- Panda mapema mara tu msimu unapoanza. wadudu hawa mara nyingi huwa wachache kipindi cha awali cha ukuaji wa mmea na huanza kuongezeka kadiri muda unavyokwenda.
- Hudumia mimea yako vizuri ili ipate afya bora, hali hii husaidia mimea kuvumilia mashambulizi ya wadudu hawa.
- Epuka kupanda soya zako karibu na shamba la mbaazi na mimea mingine jamii ya mikunde, kwani huwa ni chanzo cha wadudu hawa.
- Ondoa na teketeza masalia yote ya mimea na sehemu zote za mmea zenye dalili ya uvamizi wa wadudu hawa.
- Chunguza mimea yako mara tu baada ya kuota, weka tuta kwenye mimea yako wiki 2 hadi 3 baada ya kuota. Hii itasaidia kufunika mizizi iliyoharibiwa na wadudu hawa.
- Pia unaweza ukapulizia mimea yako na juisi ya majani au megu za mwarobaini (neem extracts). Ukipulizia Mara kwa mara italeta matokeo mazuri.
4. Vidukari Mafuta [Cotton aphids] (Aphis gossypii)
Huyu ni mdudu anaesumbua sana zao la soya, akiwa mkubwa huwa na urefu wa mm 1 hadi 1.5. wadudu hawa hujikusanya kwenye makundi makundi, huvamia mashina, matawi, majani (Chini ya majani) na matunda machanga. Wadudu hawa husambaza ugonjwa unaoitwa "Bean Yellow Mosaic Virus"
© Ronald Smith, Auburn University, Bugwood.org
Picha: Vidukari mafuta (Aphids)
© Mississippi State University , Mississippi State University, Bugwood.org
Picha: Vidukari mafuta (Aphids)
Namna ya kudhibiti
- Chunguza mara kwa mara uwepo wa wadudu hawa, hii itakusaidia kuwadhibiti mapema katika hatua za awali.
- Tumia dawa za asili kama mwarobaini (tengeneza juisi ya mbegu au majani ya mwarobaini) alafu pulizia kwenye mimea yako.
5. Viwavi wanaokula Majani (Leaf-feeding caterpillars)
Hawa ni viwavi, viwavi hawa hawana athari sana kwenye zao la soya, kwamba uharibifu wao hauna athari sana kwenye uzalishaji. Viwavi hawa ni pamoja na cotton leafworm (Spodoptera littoralis), Beet armyworm (Spodoptera exigua), Tomato looper (Chrysodeixis chalcites) na Bean leaf webworm (Omiodes indicata)
© O. Heikinheimo, Bugwood.org
Picha: Kipepeo (Cotton leafworm butterfly)
© Biologische Bundesanstalt für Land- und Forstwirtschaft , Biologische Bundesanstalt für Land- und Forstwirtschaft, Bugwood.org
Picha: Kiwavi wa Kipepeo (Spodoptera littoralis)
© Robert J. Bauernfeind, Kansas State University, Bugwood.org
Picha: Kipepeo (Beet armyworm butterfly)
© Perry Hampson, Bugwood.org
Picha: Kipepeo (Tomato looper butterfly)
Picha: Kipepeo (Bean leaf webworm / soybean leaffolder - Omiodes indicata)
Picha: Bean leaf webworm / soybean leaffolder (Omiodes indicata)
Wadudu hawa hula majani kwa kukwangua sehemu ya juu ya majani, hali hii huathiri uzalishaji japo kwa kiwango kidogo. Wadudu rafiki husaidia sana kupunguza kasi ya wadudu hawa.
Namna ya kudhibiti
- Chunguza wadudu hawa kila mara ili kubaini uwepo wake, hatua hii itasaidia udhibiti kufanyika mapema.
- Tumia dawa za asili kama Mwarobaini (Tengeneza juisi ya mwarobaini kwa kutumia mbegu au majani yake, kisha pulizia mimea)
- Watunze wadudu rafiki wanaokula wadudu hawa kama Parasitic wasps, bakteria wanaosababisha magonjwa (pathogens) n.k.
6. Leafmining caterpillars
Hawa ni viwavi wenye urefu mm 6 hadi mm 8, huanguliwa kutoka kwenye mayai yaliyotagwa chini ya majani na aina ya kipepeo anayeitwa "groundnut leafminer (Aproaerema modicella), mimea inayoathirika na wadudu hawa ni pamoja Karanga, Maharage ya Soya (Soyabean), na mimea mingine jamii ya mikunde. Viwavi hawa hula kwa kukwangua sehemu ya juu ya majani. Mdudu huyu akishakula majani baadae huendelea na hatua nyingine ya ukuaji "Pupa" na hatimae "Mdudu Kamili", mdudu kamili huyu huendelea kutaga mayai kwenye matawi na majani mengine.
Majani yaliyoathirika hubadirika rangi na kuwa kahawia, pia majani hujiviringa na kukauka, hali hii hupelekea mmea kupukutisha majani. Hali hii huathiri ukuaji wa mmea pamoja na uzalishaji.
Viwavi hawa huathiri sana zao la karanga na Soya maeneo ya kusini mwa bara la Asia. wadudu hawa pia wamevamia nchi kadhaa barani afrika ikiwemo Afrika mashariki, wamekua wakiathiri sana zao la karanga na imeripotiwa kuathiri zao la soya. Baadhi ya wakulima wameripoti upotevu wa mavuno mpaka asilimia 30%.
Namna ya kudhibiti
- Panda mimea yako mapema mara tu baada ya mvua za masika kuanza kunyesha, wakati huo kunakua na idadi ndogo ya wadudu hawa.
- Epuka kuishtua mimea yako kwa ukosefu wa maji shambani, mimea iliyopo kwenye maeneo ya ukame huathirika sana na wadudu hawa.
- Chunguza mimea yako mara kwa mara ili kubaini uwepo wa wadudu hawa, hususani kama itapandwa pamoja au karibu na karanga. Baadhi ya nchi kama India zao la soya hutumika kama sumaku (trap crops) kuwaondoa wadudu hawa kutoka kwenye karanga.
- Tumia dawa za asili zitokanazo na mwarobaini; pulizia juisi ya mbegu au majani ya mwarobaini mara tu wadudu wanapoanza. Utumiaji mapema wa dawa hizi huasaidia kuwaangamiza mapema wadudu hawa.
7. Pod borers
Hawa ni viwavi wanaotokana na aina fulani ya vipepeo wapo wa aina tatu; Legume pod borer (Maruca vitrata), Lima bean pod borer (Etiella zinckenella) na African bollworm (Helicoverpa armigera). Hawa ni wadudu wakuu wa zao la soya huvamia matunda ya soya (pods). Vipepeo wa viwavi hawa hutafuta chakula wakati wa usiku na mchana hupumzika (nocturnal). Viwavi wanaotokana na vipepeo hawa hula maua na matunda ya soya, hutoboa ngozi ya tunda la soya (Pod) huingia ndani na kuharibu mbegu za soya zinazokua.
© Don Herbison-Evans, University of Sydney, Bugwood.org
Picha: Kipepeo (Legume pod borer butterfly)
© Merle Shepard, Gerald R.Carner, and P.A.C Ooi, Bugwood.org
Picha: Kipepeo (Legume pod borer)
© Natasha Wright, Braman Termite & Pest Elimination, Bugwood.org
Picha: Kipepeo (Limabean pod butter fly) [Etiella zinckenella]
© SRPV, Ile de France , Les Services Régionaux de la Protection des Végétaux, Bugwood.org
Picha: African bollworm (Helicoverpa armigera)
Namna ya kudhibiti
- Chunguza mara kwa mara uwepo wa wadudu hawa shambani.
- Pulizia juisi ya mbegu na majani ya mwarobaini, ni mmuhimu kutumia dawa hii mapema kabla viwavi hawa hawajaingia ndani ya matunda ya soya (Pods). Mara tu viwavi hao wakifanikiwa kutoboa na kuingia ndani ya maharage ya soya, inakua vigumu sana kuwadhibiti hivyo kubakia wakifanya uharibifu.
8. Cowpea seed beetle / Cowpea weevil (Callosobruchus maculatus)
Hawa ni wadudu wanaoathiri soya baada ya kuvuna, yaani wanaharibu maharage ya soya yaliyohifadhiwa (Wanabungua). Wanaitwa "Cowpea seed beetle" kwa sababu huharibu sana mbegu za Mbaazi (Cowpea). Wadudu hawa huweza kuharibu mpaka asilimia 100% za mbegu za soya zilizohifadhiwa ndani ya miezi 3 hadi 6 katika mazingira ya kawaida. Utafiti unaonyesha kwamba udhibiti mzuri wa wadudu wanaovamia matunda ya soya (Pods) husaidia sana kupunguza kiwango cha wadudu wanabungua soya wakati wa uhifadhi.
© Clemson University - USDA Cooperative Extension Slide Series , Bugwood.org
Picha: Cowpea seed beetle (Cowpea weevil)
© Natasha Wright, Braman Termite & Pest Elimination, Bugwood.org
Picha: Cowpea seed beetle (Cowpea weevil)
© Natasha Wright, Braman Termite & Pest Elimination, Bugwood.org
Picha: Cowpea seed beetle (Cowpea weevil)
Namna ya kudhibiti
- Kabla ya kuvuna soya zako hakikisha zimekauka vizuri, kama ilivyo kwa mazao mengine maharage ya soya yakikauka vizuri hayabungui mapema. (Hakikisha unahifadhi soya zako zikiwa na unyevu chini ya asilimia 13%)
- Tumia mbegu au majani ya mwarobaini
- Tumia majivu ya pumba za mpunga. Utafiti unaonyesha kwamba matumizi ya majivu ya pumba za mpunga husaidia kuzuia mdudu aina ya 'Bruchid beetles (Callosobruchus analis)'. Kiwango cha majivu ya pumba kinachotakiwa ni asilimia 1% ya uzito wa soya. Kwa mfano kama soya zako ni kilo 20 basi kiasi cha majivu ya pumba kinachotakiwa ni kilo 0.2 (gramu 200). Changanya kwa kutumia mkono majivu haya ya pumba vizuri, taratibu pamoja na mbegu za soya zilizokauka vizuri ndani ya ndoo yenye ukubwa wa lita 6 hadi 18. Baada ya hapo funga mfuniko wa ndoo na ubane vizuri, kisha iweke ndoo hiyo mahara penye ubaridi na kwenye giza.
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
إرسال تعليق