Ufugaji wa Kuku wa Mayai - Sehemu ya Tatu (Layer Poultry Farming - Part Three)


SEHEMU YA TATU

3. MUSHY CHICK
Ugonjwa huu huathiri vifaranga, hutokana na bakteria wanaosababisha mfumo wa kitovu cha kifaranga kutokamilika vizuri akiwa kwenye yai. Pia visababishi vingine ni kama Kufanya makosa mbalimbali wakati wa kuangua vifaranga, Uchafu wa mazingira ya kuangulia mayai na Kuzidi kwa joto la mashine ya kuangulia vifaranga.

Namna unavyosambazwa
Ugonjwa huu huenezwa kutoka kifaranga hadi kifaranga au kutokana na uchafu ambao umetokana na kifaranga kilichoathirika. Hii ina maana kwamba kifaranga aliyeugua ugonjwa huu husambaza bakteria wa ugonjwa huu kwa kifaranga asiyeumwa kupitia kinyesi au majimaji aliyotoa.

Dalili za ugonjwa
  • Sehemu ya kitovu ya kuku ( Navel) huvimba na huwa na rangi ya bluu kwa mbali.
  • Kifaranga hutoa harufu mbaya na wanasinzia muda wote na wanakua dhaifu.

Namna ya kuzuia na Kutibu
  • Ugonjwa huu hauna chanjo, ingawaje mara nyingine dawa za antibayotiki hufanya kazi. Lakini ili kudhibiti uenezwaji wa ugonjwa huu hakikisha unawatenga vifaranga wote waliougua ili wasiambukize vifaranga wazima.
  • Wakati unatoa huduma kwa vifaranga wagonjwa, uwe muangalifu maana bakteria hawa aina ya Staphylococcus na streptococcus huwakumba binadamu.

4. BUMBLEFOOT
- Huu ni ugonjwa wa miguu, hutokana na ajari ndogo ndogo ambazo kuku anazipata akiwa mazingira ya ndani au nje ya banda hususani wakati akiparua chini kutafuta chakula, Kwenye mazingira hayo Kuku hujikata na kupata michubuko au vidonda ambavyo ndio mwanzo wa ugonjwa huu. Michubuko au vidonda hivyo ndio lango la vimelea vya magonjwa hatimae sehemu iliyokatwa huanza kuvimba, pia mara nyingine mguu mzima huvimba.

Dalili za Ugonjwa

  • Kidonda husababisha mguu wote kuvimba.
  • Kuku huchechemea au hatembei vizuri kama ilivyo kawaida.


Namna ya kuzuia na kutibu
  • Kuzuia ugonjwa huu ni kazi sana, kwa sababu mazingira ambayo kuku anapata michubuko au vidonda ni ya kawaida sana kiasi kwamba ni ngumu kudhibiti mazingira hayo. Chamsingi hapa ni kwamba jitahidi kuchunguza kuku wako mara kwa mara, ukiona kuku hatembei vizuri au anatembea kwa kuchechemea, mkamate na mchunguze kwenye nyayo za miguu.
  • Ukigundua kua ameumia mguuni, haraka sana osha kidonda hicho kwa maji safi alafu mpake antibayotiki (Disinfectant) ya kuzuia vimelea (Bakteria), ili kuepusha ugonjwa huu kutokea.
  • Tibu ugonjwa huu kwa kufanya oparesheni ndogo, muone afisa mifugo aliyekaribu yako ili afanye oparesheni hii. Kwa kuku aliyepata ugonjwa huu, ukiamuacha hivyo hivyo bila kuchukua hatua yoyote anaweza kufa.

5. QUAIL DISEASE
Ugonjwa huu husababishwa na bakteria aina ya Clostridium colinum, bakteria hawa husambazwa kutoka kwa kuku mgonjwa hadi kwa kuku asiyeumwa kupitia majimaji yanayotoka kwa kuku mgonjwa. Bakteria hawa ni sugu sana kwa antibayotiki za kuzuia vimelea (Disinfectant) na hustahimili mazingira ya aina mbalimbali.

Dalili za Ugonjwa
  • Baadhi ya kuku hufa ghafla wakiwa na afya nzuri (acute form of disease)
  • Kuku walioathirika na kuwa sugu na bakteria hawa, huishiwa nguvu, huwa na manyoya rafu, huharisha kinyesi cha majimaji meupe na wanapinda mgongo (Wanakua na kibyongo).
  • Kuku walioathirika hufa wakiwa wamekonda sana.
Namna ya kuzuia na kutibu
  • Tumia dawa za antibayotiki kwa kukinga na kutibu ugonjwa huu, Mfano wa dawa hizo ni BACITRACIN na PENICILLIN, dawa hizi zinafanya vizuri sana kukinga na kutibu ugonjwa huu.
  • Kama utatumia BACITRACIN changanya kwenye chakula kiasi cha grams 200 kwa tani moja ya chakula. Pia unaweza ukaweka kwenye maji ya kunywa kiasi cha kijiko kimoja cha chai kwa lita tano za maji, hii husaidia kuzuia mlipuko wa ugonjwa huu. Dawa hii ya BACITRACIN hudhibiti ugonjwa huu ndani ya wiki mbili. Dawa ya PENICILLIN nayo hutibu ugonjwa huu, hutumika pale ambapo BACITRACIN imeshindwa kutibu ugonjwa huu.
  • Pia ili kufanikisha matibabu kwa ufasaha zaidi, muone Afisa mifugo aliyekaribu yako kwa ushauri zaidi.
NB:
Magonjwa mengine mengi nimeyaelezea kwa kina kwenye makala ya ufugaji wa kuku wa kienyeji, Magonjwa mengi ya kuku wa kienyeji ni yaleyale kwa kuku wa kisasa. Bofya viunganishi vifuatavyo kusoma magonjwa mengine; SEHEMU YA 1, SEHEMU YA PILI, SEHEMU YA 3, SEHEMU YA 4.

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم